1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Zanzibar ajibu tuhuma za ufisadi

Tatu Karema
28 Februari 2023

Rais Hussein Mwinyi wa Zanzibar ametumia mkutano wake na waandishi wa habari kujibu tuhuma nzito dhidi ya ufisadi yaliyotolewa na viongozi wa chama mshirika mdogo serikalini, ACT Wazalendo

https://p.dw.com/p/4O5DZ
Sansibar | President Dr Hussein Mwinyi
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Akizungumza na waandishi wa habari hivi leo katika Ikulu ya Mnazi Mmoja hapa mjini Zanzibar, Rais Mwinyi ametupilia mbali shutuma na tuhuma zilizotolewa na washirika wake serikalini, akisema ni madai matupu yasiyo ushahidi zaidi ya kuwapotosha wananchi. Mwinyi asema utendaji katika maeneo yalikuwa na changamoto nyingi za upotevu wa fedha lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa.

Mwinyi azungumzia mabadiliko makubwa

Akijibu makhasusi kabisa juu ya kile kinachodaiwa na ACT Wazalendo kuwa ni harufu ya ufisadi na utendaji mbaya wa kazi katika njia kuu za uchumi wa Zanzibar, bandari na uwanja wa ndege, rais huyo aliyezungumza kwa hasira alisema wakati anaingia madarakani utendaji katika maeneo yalikuwa na changamoto nyingi za upotevu wa fedha lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa yanayotia moyo kutokana na mageuzi makubwa anayoyasimamia, ambayo wapinzani wake wanayajuwa lakini hawayasemi.

Tansania Afrika Zitto Kabwe
Zitto Kabwe - Kiongozi mkuu wa ACTPicha: privat

Hii ni mara ya kwanza kwa chama cha ACT Wazalendo kufanya mkutano wake wa hadhara baada ya miaka saba ya zuio lililowekwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na aliyekuwa rais wa wakati huo, Hayati John Pombe Magufuli. Lakini si mara ya kwanza kwa chama hicho kuyazungumzia haya, tangu kujiunga na serikali ya Umoja wa Kitaifa kufuatia uchaguzi wa 2020.

Viongozi waangazia mapungufu kwenye bandari

Wakizungumza katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika Nungwi, kaskazini mwa kisiwa cha Unguja, viongozi wa chama hicho waliangazia zaidi mapungufu yaliyopo kwenye bandari, uwanja wa ndege na utoaji wa zabuni, wakisema umekosekana uwazi na kumekuwapo upendeleo mkubwa, ambao matokeo yake ni kupotea kwa fedha za umma kama ilivyobainishwa na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali mwaka jana.

Zitto Kabwe, kiongozi mkuu wa ACT, alisema gharama za bandari zimekuwa kubwa sana kwa wafanyabiashara na hivyo biashara inahama Zanzibar na kwenda bandari ya Dar es Salaam. Kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara inatoa nafasi kwa vyama vya upinzani kufuatilia na kukosoa serikali iliyopo madarakani Bara na Zanzibar, lakini jambo linalosubiriwa na wananchi ni kwa kiasi gani serikali zote mbili zitaendelea kuwa na uvumilivu katika ukosoaji huo.