1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGuatemala

Rais wa Guatemala atangaza hali ya hatari

19 Januari 2026

Rais Bernardo Arevalo wa Guatemala ametangaza hali ya hatari ili kukabiliana na magenge yaliyouwa maafisa wanane wa polisi

https://p.dw.com/p/571wK
Rais wa Guatemala wa Bernardo Arevalo
Rais Bernardo Arevalo wa Guatemala alisema hali ya hatari ingelidumu kwa siku 30 kuanzia Januari 19, 2026.Picha: Johan Ordonez/AFP

Rais Arevalo alisema kuwa tarayi vyombo vya usalama vimerejesha udhibiti wa magereza matatu yaliyokuwa yametwaliwa na magenge hayo mwishoni mwa wiki.

Akihutubia taifa usiku wa kuamkia Jumatatu (Januari 19), Arevalo alisema hali hiyo ya hatari itadumu kwa siku 30 nchi nzima.

Hatua hiyo inavisitisha kwa muda baadhi ya vifungu vya katiba, wakati taifa hilo la Amerika ya Kusini likipambana na magenge mawili ya Barrio 18 na Mara Salvatrucha, au M-13.

Magenge hayo yanatambuliwa kuwa makundi ya kigaidi nchini Guatemalana Marekani na yanatuhumiwa kwa mauaji ya kupanga, upotezaji watu na biashara ya madawa ya kulevya.

Mamlaka nchini Guatemala zinayatuhumu magenge hayo kwa mauaji ya polisi wanane siku ya Jumapili (Januari 18) kulipiza kisasi kwa serikali iliyokataa kuwahamishia viongozi wao kwenye gereza lenye kiwango kidogo cha ulinzi.

Mauaji hayo yalifanyika kwenye mji mkuu wa Guatemala pamoja na maeneo ya karibu, siku moja baada ya wafungwa wenye mafungamano na magenge hayo kuwateka watu 46 kwenye magereza matatu nchi nzima.