Rais Toure awasilisha rasmi barua ya kujiuzulu | Matukio ya Afrika | DW | 09.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais Toure awasilisha rasmi barua ya kujiuzulu

Rais wa Mali aliyeondoshwa madarakani, Amadou Toumani Toure, amewasilisha rasmi barua ya kujiuzulu kwa viongozi wa kijeshi, ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kumaliza mkwamo wa kisiasa nchini humo.

Rais Amadou Toumani Touré.

Rais Amadou Toumani Touré.

Kutokea mafichoni ambako amekuwako tangu kupinduliwa wiki tatu zilizopita, Rais Toure, au ATT kama anavyofahamika na watu wake, amesaini barua ya kujiuzulu na kuikabidhi kwa mjumbe maalum ambaye naye aliiwasilisha kwa viongozi wapya wa Mali hapo jana.

Hatua hii inafungua njia kwa Mali kumtaja rais mpya wa muda, ikiwa ni katika utaratibu wa kuirudisha nchi hiyo katika utawala wa kidemokrasia. Ilikuwa imebakia miezi michache tu kwa Rais Toure kumaliza rasmi muhula wake madarakani, pale wanajeshi wa ngazi za chini walipoyavamia makazi yake hapo Machi 21 na kumuodoa madarakani.

Tangu hapo, hapakuwa na taarifa za kutosha kuhusu kiongozi huyo, ambaye mwenyewe aliwahi kuingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi, kabla ya kuchaguliwa kidemokrasia.

Waandishi wa habari wa televisheni ya taifa na ile ya France 24 ya Ufaransa waliruhusiwa kwenda kumpiga picha Rais Toure kando kidogo ya mji mkuu, Bamako, ambako amekuwa akijificha muda wote huo.

"Najiuzulu kwa hiari yangu"

Spika wa Bunge la Mali, Dioncounda Traore (katikati).

Spika wa Bunge la Mali, Dioncounda Traore (katikati).

Waandishi hao wanasema Rais Toure, mwenye miaka 63, anaonekana amedhoofu kidogo kuliko alivyokuwa kabla ya kupinduliwa, lakini alijitokeza akiwa amevaa vazi la kitaifa la nchi yake, kanzu na kofia, akisema kwamba anajiuzulu kwa ridhaa yake mwenyewe.

"Leo hii katika kutafuta suluhisho, uamuzi wa ECOWAS na jumuiya ya kimataifa ni wa kuhakikisha kuwa lazima Mali ibakie kwa msingi wa katiba yake ya Februari 1992. Kwa uamuzi niliochukuwa ni wa hiyari yangu, ninafanya kwa imani yangu na bila ya shinikizo lolote. Ninafanya haya kwa imani safi na zaidi kwa mapenzi ya nchi yangu. Nimeamua kuwasilisha barua ya kujiuzulu."

Hatua hii ya Rais Toure inafuatia makubaliano ya kuondoka kwa utawala mpya wa kijeshi, yanayosimamiwa na Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS. Chini ya makubaliano hayo yaliyosainiwa hap Ijumaa wa kijeshi, Kapteni Amadou Sanogo, wanajeshi hao wataondoka madarakani na kumuachia spika wa bunge la nchi hiyo, Dioncounda Traore, kuongoza serikali ya kipindi cha mpito, ambayo itasimamia uchaguzi mkuu, kwa mujibu wa kipengele cha 36 cha katiba ya Mali.

Hata hivyo, ili kipengele hicho cha katiba kitekelezwe kikamilifu, kinahitaji mahakama ya katiba nchini Mali kuthibitisha kwamba rais hawezi kutekeleza majukumu yake.

Wanajeshi wapinda magoti mbele ya vikwazo vya kimataifa

Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Amadou Haya Sanogo.

Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Amadou Haya Sanogo.

Wanajeshi waliamua kukubaliana na shinikizo la kimataifa dhidi yao, baada ya vikwazo dhidi yao kuanza kuonekana makali yake. Mji mkuu Bamako, umeanza kukosa umeme kwa kipindi cha 12 kwa siku, kunakotokana na vikwazo vya kiuchumi na kifedha vilivyowekwa na nchi jirani za Mali, ambayo yenyewe haina mpaka wa bahari.

Wanajeshi waliochukuwa madaraka siku karibuni wiki tatu zilizopita, walisema wanafanya hivyo kutokana na Rais Toure kushindwa kuudhibiti uasi wa kaskazini mwa nchi hiyo ulioanza mwezi Januari. Umashuhuri wa Toure ulishuka sana kwa sababu ya kile kilichoonekana ukosefu wa ushupavu dhidi ya mashambulizi ya Tuareg, ambayo yalisababisha maafa makubwa kwa jeshi la Mali lisilo na vifaa vya kutosha.

Hivi sasa, waasi wa Tuareg wanalidhibiti eneo zima la kaskazini na kujitangazia uhuru wa kile wanachokiita Azawad, ikiwemo miji mitatu maarufu ya Timbuktu, Gao na Kidal. Eneo ambalo sasa limo ndani ya mikono ya waasi ni kubwa zaidi kuliko sehemu ya nchi iliyobakia.

Hata hivyo, kunaripotiwa mgawanyiko wa kiitikadi ndani ya waasi waliochukuwa udhibiti wa eneo hilo, baina ya Waislamu wenye msimamo mkali na wale wa wasiopendelea mfumo wa siasa kufuata dini. Tayari wanamgambo wa Kiislamu wameanza kuweka taasisi za utawala katika eneo hilo, huku wakiwalazimisha wakaazi wake kufuata mfumo wa Sharia.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza