Rais Sarkozy ziarani Emireti | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.05.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais Sarkozy ziarani Emireti

Ufaransa yafungua kambi za kijeshi katika nchi za Emireti

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa anatazamiwa kuwasili katika falme za nchi za kiarabu baadae leo usiku kwa lengo la kuimarisha nafasi ya kijeshi ya Ufaransa katika eneo la mashariki ya kati na pia kuyapa moyo makampuni ya nchi yake yanayopigania kujipatia kandarasi kubwa kubwa katika sekta ya ulinzi na nishati ya kinuklea.

Akifuatana na mawaziri wanne wa serikali yake na kundi kubwa la wanaviwanda, rais Nicolas Sarkozy atafanya ziara ya zaidi ya saa 20 huko Abu Dhabi na kuhudhuria karamu ya chakula cha usiku pamoja na mwanamfalme Sheikh Mohammed Ben Zayyed Al-Nahyan. Kesho Jumanne rais huyo wa Ufaransa amepangiwa kufungua kambi mpya na ya kudumu ya jeshi la Ufaransa, ya kwanza ya aina yake kufunguliwa na Ufaransa nchi za ng'ambo, tangu makoloni yake ya zamani ya Afrika yalipojipatia uhuru.

Kama alivyosema rais Nicolas Sarkozy wakati wa mahojiano na shirika la habari la Emirati, Wam, kambi hiyo ya wanajeshi wa Ufaransa karibu na ujia wa maji wa Ormuz inadhihirisha masilahi ya Ufaransa katika eneo hilo linalopakana na Iran inakopitia asilimia 40 ya mafuta ya dunia.

Rais Nicolas Sarkozy amesema tunanukuu, "Kwa namna hii Ufaransa inadhihirisha iko tayari kubeba majukumu yake yote ili kudhamini utulivu katika eneo hilo muhimu kwa wezani wa dunia." Mwisho wa kumnukuu.

Katika wakati ambapo ulimwengu wa magharibi unaituhumu Iran kutaka kujitengenezea silaha za kinuklea,kambi hiyo ya kijeshi ya Ufaransa inaweza kuchukua sura ya risala ya kisiasa kwa majirani zake wa kiarabu wanaofuata msimamo wa wastani."Kwa kufungua kambi hiyo ya kudumu ya kiijeshi,Ufaransa inadhihirisha mafungamano yake pamoja na marafiki zake wa Emirat kwaajili ya usalama wao:"Amesisitiza kiongozi huyo wa Ufaransa.

Kambi hiyo inafunguliwa kutokana na maombi ya nchi za Emirat .Makubaliano mepya ya ulinzi yatakayochukua nafasi ya yale ya mwaka1995 kati ya nchi hizi mbili yanatazamiwa kutiwa saini kesho .

Kambi hiyo ya kijeshi ilichojengwa mwaka mmoja na nusu uliopita na kupewa jina "Kambi ya amani",itakua na wanajeshi kati ya 400 hadi 500 watakaowekwa katika vituo vitatu.Kituo cha jeshi la wanamaji karibu na bandari ya Abu Dhabi,kituo cha jeshi la wanaanga na kambi ya mazoezi ya kijeshi.

Mkuu wa kambi hiyo,kanali Hervé Cherel anasema kambi hiyo itatumika kuwasaidia wanajeshi wa Ufaransa katika bahari ya Hindi na pia kuimarisha ushirikiano wa kijeshi wa pande mbili.

Rais Sarkozy anategemea pia kambi hiyo itasaidia kuwazindua viongozi wa Emirat watambue ubora wa zana za kijeshi za Ufaransa.

Kiongozi huyo wa Ufaransa anapanga pia kuitumia ziara yake hii ya Abu Dhabi kuyapatia soko makampuni ya nishati ya nchi yake yanayoshindana na makampuni ya Marekani na yale ya Korea ya kusini katika kuzipatia nishati ya kinuklea nchi za Emirat.

Mwandishi: Hamidou, Oumilkher

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 25.05.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Hx9j
 • Tarehe 25.05.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Hx9j
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com