Rais Musharraf afikiria kujiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Musharraf afikiria kujiuzulu

Rais wa Paksitan Pervez Musharraf anafikiria kujiuzulu. Leo kiongozi wa upinzani nchini Pakistan, Benazir Bhutto, ameendeleza juhudi zake za kuunda muungano dhidi ya rais Musharraf huku Marekani nayo ikizidi kumshinikiza jenerali huyo amalize utawala wa kijeshi.

Jenerali Pervez Musharraf

Jenerali Pervez Musharraf

Televisheni ya Uingereza Sky News, imetangaza hii leo kwamba rais wa Pakistan, Pervez Musharraf, anafikiria kujiuzulu wadhifa wake. Katika mahojiano yake na televisheni hiyo, yatakayoonyeshwa baadaye leo, rais Musharraf amesema alifikiria sana juu ya cheo chake lakini sasa anahisi yeye ndiye mtu pekee anayeweza kuingoza Pakistan kuelekea demokrasia.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Marekani, Tom Casey, amesema, ´Nadhani kuna mabadiliko yaliyotokea katika msimamo wa kwanza wa rais Musharraf ingawa bila shaka hautoshi kwa sisi kuridhika kwamba sasa Pakistan imerejea katika njia ya demokrasia tunayoitaka ielekee.´

Wakati haya yakiarifiwa, kiongozi wa upinzani nchini Pakistan Benazir Bhutto, ameanza mazungumzo na viongozi wengine wa upinzani nchini humo waliokosana na rais Musharraf kwa kumuomba ajiuzulu na kuapa hawatafanya kazi katika serikali atakayoiongoza. Benazir Bhutto amebakia katika kizuizi cha nyumbani huko mjini Lahore, ambako maafisa 1,000 wa polisi wanashika doria kwenye makazi yake yaliyozungushiwa waya wa sing´eng´e na vizuizi.

Habari zaidi kutoka Lahore zinasema kiongozi wa upinzani Imran Khan amejitokeza leo kwenye maandamano ya wanafunzi ya kupinga utawala wa hali ya hatari. Chama chake kimesema Imran Khan ametiwa mbaroni na polisi.

Wanafunzi takriban 200 walimshangilia Imran Khan na kumbeba aliposhuka kutoka kwa motokaa yake katika chuo kikuu kimoja kilicho mashariki mwa mjini Lahore. Imran Khan, mchezaji mashuhuri wa zamani wa mchezo wa cricket, anayeongoza chama kidogo cha upinzani, alijificha mara tu rais Pervez Musharraf alaipotangaza hali ya hatari.

Sambamba na hayo, Marekani ambayo inaiona Pakistan kuwa mshirika muhimu katika vita dhidi ya ugaidi, inamtuma naibu waziri wa mashauri ya kigeni, John Negroponte, kwenda Islamabad baadaye wiki hii. Negroponte, ambaye atakuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya ju wa Marekani kuzuru Pakistan tangu mgogoro ulipoanza, atataka utawala wa hali ya hatari umalizike.

Alipoulizwa ikiwa rais Bush na Marekani kwa jumla ina ushawishi wa kutosha dhidi ya rais Musharaf, mkurugenzi wa muungano wa mahakimu nchini Pakistan, bwana T. Kumar, ambaye pia ni mwanachama wa shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, amesema ni mchache.

´Hautoshi! Ni maneno matupu tu! Rais Bush na ikulu ya Marekani wanaangalia kwa macho yanayoendelea nchini Pakistan. Tunataka sisi shirika la kutetea haki za binadamu pamoja na mashirika mengine makubwa ya kimataifa yanayopigania haki za binadamu, kwamba msaada wote wa usalama pamoja na misaada ya kijeshi isitishwe mpaka rais Musharaf awaachie huru wote aliowatia korokoroni ikiwa ni pamoja na jaji mkuu na majaji wengine.´

Na ikiwa uchaguzi alioahidi rais Musharraf utaleta demokrasia ya kweli nchini Pakistan, bwana Kumar amesema, ´Hapana! Hali ya haki za binadamu nchini Pakistan itaboreka wakati mahakimu watakapoachiliwa na kurejeshwa kazini na uhuru wa kujieleza utakapohakikishwa. Huwezi kuhakikisha chochote nchini Pakistan. Ni utawala mbaya wa kigaidi unaoendelea nchini Pakistan kwla kisingizio cha kupambana na ugaidi.´

Makundi kadhaa ya kutetea haki za binadamu leo yamemtaka rais George W Bush asitishe msaada wa kijeshi kwa Pakistan ikiwa rais Musharraf atakaa kumaliza utawala wa hali ya hatari na kuwaachia huru wanasiasa, mawakili na watetezi wa haki za binadamu wanaozuiliwa nchini Pakistan.

 • Tarehe 14.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH6x
 • Tarehe 14.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH6x

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com