Rais Karzai aapishwa | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 19.11.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Rais Karzai aapishwa

Sherehe za kuapishwa zimefanyika leo mjini Kabul na kuhudhuriwa na viongozi wa kitaifa na kimataifa.

default

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan ameapishwa leo kwa awamu ya pili ya miaka mitano madarakani na kuahidi kukabiliana na tatizo la rushwa nchini humo pamoja na kuwataka mahasimu wake wakubwa wajiunge katika serikali atakayoiunda ya umoja wa kitaifa.

''Kwa jina la Mwenyezi Mungu ninaapa kulinda maadili ya dini ya Kiislamu, kuilinda katiba na sheria nyingine za Afghanistan na kusimamia utekelezwaji wake na kuheshimu sheria ya Afghanistan.''

Hicho ni kiapo kilichotolewa na Rais Karzai hii leo wakati akiapishwa na Jaji Mkuu wa Afghanistan, Abdul Salam Azimi, sherehe zilizofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul na kuhudhuriwa na mamia ya viongozi wa kikabila, mawaziri wa Afghanistan na mawaziri wa kigeni. Baada ya kuapishwa, Rais Karzai kisha na yeye aliwaapisha makamu wake wawili, Mohammad Qasim Fahim na Mohammad Karim Khalili.

Ahadi alizotoa

Akizungumza baada ya kuapishwa Rais Karzai aliahidi kukabiliana na tatizo la rushwa na kusema kuwa vikosi vya usalama vya nchi yake lazima viwe tayari kuwajibika kutokana na kukosekana kwa hali ya usalama katika nchi hiyo. Rais Karzai ameapishwa wakati Marekani ikiendelea kumkosoa kuhusiana na nchi yake kugubikwa na rushwa. Hata hivyo Marekani imesema iko tayari kuiunga mkono nchi hiyo, lakini hadi serikali mpya itakapopambana kikamilifu na rushwa na endapo serikali hiyo itafanya kazi yake katika uwazi. Rais Karzai, alisema rushwa ni hatari na kwamba hivi karibuni wataandaa mkutano mjini Kabul utakaozungumzia njia na mikakati ya kukabiliana na tatizo la rushwa.

Aidha, Rais Karzai amemkaribisha mpinzani wake mkuu, Abdullah Abdullah kufanya kazi katika serikali ya umoja wa kitaifa na kuahidi kukabiliana na uuzaji wa dawa za kulevya na kuongeza ajira. Rais Karzai alitangazwa mshindi baada ya Bwana Abdullah kujiondoa katika duru ya pili ya uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 7 ya mwezi huu wa Novemba. Uchaguzi wa duru ya kwanza ulikabiliwa na udanganyifu jambo lililosababisha uchaguzi huo kurejewa tena.

Viongozi wa kimataifa

Viongozi waliohudhuria sherehe za kuapishwa Rais Karzai ni pamoja na Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan na Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton, ambaye alisema, ''Kwa sasa kuna uwezekano wa Rais Karzai na serikali yake kufanya mapatano mapya na watu wa Afghanistan kuonyesha wazi kwamba tutawajibika ipasavyo na kutoa matokeo kamili.''

Wengine ni mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa, Guido Westerwelle, David Miliband na Bernard Kouchner pamoja na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/DPAE)

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 19.11.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KayJ
 • Tarehe 19.11.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KayJ
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com