1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa DRC walalamikia kupanda kwa gharama za maisha

Jean Noël Ba-Mweze
1 Novemba 2021

Katika siku za hivi karibuni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inakumbwa na malalamiko ya kijamii. Wanainchi wanalalamika sana kuhusu maisha magumu na ya gharama kubwa, pia matatizo mengine yanayotokana na hali hiyo.

https://p.dw.com/p/42RAU
Der Ampelroboter von Kinshasa
Picha: D. Kannah/AFP/Getty Images

Wakongomani wengi wanaamini kwamba wanasiasa hawajali umaskini wa raia ila wanafikiria tu maslahi yao wenyewe. Haya yamejiri huku uteuzi wa timu isiyokubaliwa na wengi kuiongoza Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI) ukileta utata.

Miezi michache iliyopita, serikali ilitangaza kushusha bei ya baadhi ya bidhaa maarufu za vyakula hapa nchini. Lakini kinyume na hiyo, bidhaa hizo kuongezeka bei katika soko, ingawa fedha hazipatikani.

Watumishi wengi wamefanya kazi kwa miezi kadhaa bila kulipwa na wengine hupokea mishahara isiyoridhisha. Kwenye elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ufundi kwa mfano, maelfu ya walimu wanaoitwa vitengo vipya (NU) na wale wasiopokea mishahara (NP) wamekuwa wakifanya kazi kwa miaka kadhaa bila malipo.

Hali ni ngumu ambayo haijawahi kutokea hapa nchini, kama alivyoeleza Alex Tshimba, mmoja wa wafanyakazi wanaokabiliwa na hali hii ya kutolipwa; ''Hali ni janga kabisa. Kila mtu analia mitaani. Kutolipwa mishahara pamoja na ubadhirifu, yote yamezidisha hali ya umaskini hapa  Kongo. Nadhani mamlaka zetu haziipendi nchi hii. Kila kiongozi angekuwa na nia nzuri, tusingekuwa hivi tulivyo leo.''

Frankreich Kongo Felix Tshisekedi  und Emmanuel Macron
Rais Felix Tshisekedi na Emmanuel Macron Picha: Thomas Padilla/dpa/picture alliance

Hata hivyo, hali hiyo inamtia wasiwasi Rais Félix Tshisekedi, ambaye anataka kuboresha  maisha ya Wakongomani. Ni kwa lengo hilo ndiyo anafanya safari katika nchi mbalimbali, lakini Wakongomani, akiwemo mkaazi huyu wa Kinshasa ambaye hakutaka jina lake litajwe, hawana subira au tumaini; ''Safari hizo zote, ikiwa ni lazima kuzihesabu zitagharimu kiasi gani cha fedha. Fedha hizo zinazopotea kwenye safari, kwa nini hazingetumiwa mfano kuwalipa watumishi wa serikali? Ndiye rais wa kwanza ambaye amesafiri sana duniani. Anaweza kupunguza hizo safari na kuweka fedha hizo kwa manufaa ya wananchi, kwani kwa kweli wanainchi hawafaidiki.''

Wakongomani kadhaa ambao wamezungumza na DW wanaamini kuwa utawala uliopo haujaleta mabadiliko yoyote mazuri kwenye kapu la akinamama nyumbani hadi sasa. Hali inazidi kuzorota, kama alivyoeleza mkazi mwengine, Joël Kakoloboka, akijutia hata kuondoka kwa rais wa zamani Joseph Kabila.''Hakuna kitu, hakuna kitu kinachoendelea. Walikuwa wakisema Kabila alikuwa hafanyi chochote, lakini leo, hakuna kitu. Namkumbuka Kabila. Ni bora Kabila angerudi, lakini, alifanya kazi na kutimiza alichoahidi. Kabila angeweza kufanya mengi lakini alipingwa sana. Leo tuna upinzani madarakani, lakini ni zaidi ya Kabila. Hakika ni janga.''

Ni baada ya kuapishwa timu ya Denis Kadima ili kuiongoza Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) ndiyo baadhi ya Wakongomani walionyesha kutoridhika kwao. Rais Tshisekedi anapanga kuwania muhula wa pili mwaka 2023, lakini baadhi ya wachambuzi wanashauri aitumikie kwanza jamii wa Wakongomani. Baadhi ya wakaazi waliotueleza wanaunga mkono kazi ya Rais Tshisekedi, ingawa hawakutaka sauti zao kusikika.