1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Beni waipinga serikali

27 Novemba 2019

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imepiga marufuku kutembea kwa wakaazi ifikapo saa kumi na mbili jioni. Hatua hii inalenga kuwaepusha wakaazi kutokana na mauwaji ya waasi.

https://p.dw.com/p/3To1A
Demokratische Republik Kongo Beni
Picha: Imago Images/Afrikimages/K. Musayi

Serikali imepiga marufuku kutembea nyakati hizo katika maeneo ya Beni mjini, Mavivi, Mbau, Oicha, Kokola, Mayimoya na Eringeti katika wilaya ya Beni. 

Katika baadhi ya mitaa ya Beni, vijana, wazee na pia akina mama wanapiga doria na kuwasha moto katika njiapanda mbalimbali ili kujilindia usalama wao.

Wakizungumza na DW usiku wa kuamkia leo vijana hawa wanaopinga hatua ya serikali ya kuwaomba wakaazi wa eneo hili kutotembea ifikapo saa kumi na mbili jioni walisema hatua hiyo ndio imewafanya kuchukua uamuzi huo wa kukesha mabarabarani usiku kucha.

Hatua hiyo haikupingwa tu na raia wa kawaida, bali hata wazee wa busara wa mji wa Beni wameupinga uamuzi wa serikali wa kuwaomba watu kutotoka nje ifikapo saa kumi na mbili jioni.

Demokratische Republik Kongo | Überfall auf UN-Lager in Beni
Wakazi wanapinga hatua hiyo kwa sababu wanasema, nyakati za jioni ndio hutoka makwao na kutafuta maeneo salama ya kulalaPicha: Getty Images/AFP/U. Mwendapeke Eliezaire

Omar Kavota ni mmoja wa wazee wa busara katika mji wa Beni anadhani kwamba ni uamuzi ambao huenda ukasababisha maafa mengi kwani, nyakati za jioni ndio wakaazi wanaondoka makwao na kwenda kulala katika maeneo wanayodhani kuwa kuna usalama.

Kwa upande wake naibu waziri ambaye pia ni waziri wa mambo ya ndani Gilbert Kankonde, akiwa ziarani katika mkoa huu wa Kivu ya kaskazini, ametetea uamuzi huo wa serikali.

Alinukuliwa akisema "Hatua hii ya watu kutotembea usiku inalenga kuhakikisha usalama wa raia, ili nyakati za usiku tuepushe kutembea usiku kwa wakaazi wema, ili tuwaepushe na vitendo vya kinyama vya wauwaji wanaoendesha vitendo vyao nyakati za giza, ili kuendesha vitendo vyao vitakavyopelekea watu kuzungumzia vitendo hivyo."

Na wakati hatua mbalimbali zinachukuliwa ili kuwaepusha wakaazi wa mji pamoja na wilaya ya Beni na mauwaji yanayofanywa na waasi kutoka Uganda ADF, ripoti toka Oicha, kilomita thelathini kaskazini mwa mji wa Beni zinadokeza, kuwa ADF wamewauwa tena watu wanne usiku wa kuamkia leo katika kijiji cha Maleki kilichopo kilomita tisa magharibi mwa mji mdogo wa Oicha.

Tangu Novemba tano watu si chini ya themanini wameshauawa na ADF katika mji na wilaya ya Beni na bado haijulikani ni lini mauwaji hayo yatakomeshwa.