1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin awataka matajiri Urusi kuchangia bajeti ya nchi hiyo

27 Machi 2026

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewataka matajiri nchini humo kuchangia katika bajeti ya nchi hiyo kwa lengo la kuimarisha uchumi huku akiendeleza mapigano yake nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/5BEp7
Urusi Moscow 2026 | Vladimir Putin katika mkutano na gavana wa eneo la Orenburg Evgeny Solntsev
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Gavriil Grigorov/Sputnik/Kremlin Pool Photo/AP Photo/picture alliance

Shirika la habari la The Bell limeripoti bila kutaja vyanzo vyake kwamba Putin alikutana na wafanyabiashara wakuu wa Urusi faraghani na kuzungumzia kuhusu ufadhili wa kijeshi na muendelezo wa vita hivyo ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka minne sasa.

The Bell pia imeripoti kuwa wakati wa mkutano huo na Putin, bilionea Suleiman Kerimov aliahidi kuchangia dola bilioni 1.23. Hata hivyo Reuters haikuweza kuthibitisha ripoti hiyo kwa njia huru.

Gazeti la Financial Times pia lilichapisha ripoti kama hiyo na kutaja vyanzo vitatu vya karibu na suala hilo.

Urusi kuendeleza vita Ukraine hadi kutimiza malengo 

Ripoti hiyo imeongeza kuwa Putin amesema Urusi itaendelea kupigana hadi itakapokamata maeneo yaliobaki katika mkoa wa mashariki wa Donbas nchini Ukraine ambayo hayako chini ya udhibiti wake.

Huku hayo yakijiri, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema hazina ya dola milioni 25 kusaidia kurejesha watoto wa Ukraine waliohamishiwa kwa nguvu nchini Urusi itatumika kuwatambua, kuwarejesha na kuwapa msaada wa ushauri watoto na vijana ambao wamekuwa mbali na familia na jamaa zao.

Ukraine Kiev 2026 | Zelensky akihutubia viongozi wa Uloaya kwa njia ya video mnamo Machi 19, 2026
Rais wa Ukraine , Volodymyr ZelenskyPicha: Ukrainian Presidential Press Service/AFP

Taarifa ya wizara hiyo imesema hazina hiyo pia itasaidia mipango ya aina mbili. Kwanza kuwatambua na kuwafuatilia watoto waliohamishwa, na kusaidia kuunganishwa tena katika jamii.

Kupitia chapisho kwenye mtandao wa X, mke wa Rais wa Ukraine Olena Zelenska amepongeza hatua hiyo na kusema lazima watoto wote wa Ukraine warudishwe nchini humo.

Ukraine yasema watoto wake 20,000 wako Urusi

Zelenska, alikutana mjini Washington na maafisa wawili wakuu wa wizara ya mambo ya nje, Riley Barnes na Jeremy Lewin, ambao wanasimamia haki na misaada ya kibinadamu.

Kulingana na Ukraine , takriban watoto wake 20,000 walihamishwa kwa nguvu hadi Urusi wakati wa uvamizi wa mwezi Februari mwaka 2022.

Kwa upande wake, Urusi inasisitiza kuwa iliwahamisha watoto hao wa Ukraine kutoka maeneo yaliyotekwa kwa ajili ya usalama wao wenyewe na iko tayari kuwarejesha kwa familia zao hali itakapoimarika.