Pigo kwa wasichana wajawazito Burundi | Masuala ya Jamii | DW | 05.07.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Pigo kwa wasichana wajawazito Burundi

Mashirika ya haki za binadamu yamekosoa hatua ya Burundi ya kuwapiga marufuku wasichana wajawazito na wavulana waliowapa ujauzito huo kurudi shuleni, yakisema hatua hiyo ni ukiukaji dhidi wa haki za elimu kwa watoto.

Mashirika hayo pia yanasema kuwa hatua hiyo ni ubaguzi dhidi ya mtoto wa kike. Juma lililopita serikali ya Burundi ilitoa agizo kwa serikali za mikoa ikisema kuwa wasichana wajawazito pamoja na wavulana waliosababisha ujaouzito huo hawana haki ya kuwa sehemu ya mfumo wa elimu nchini humo.

Katika barua ilioandikwa Juni 26 kwa wakurugenzi wote wa elimu mikoani, waziri wa elimu Janvière Ndirahisha alisema hata hivyo kuwa wanafunzi hao wataruhusiwa kuhudhuria mafunzo ya kiufundi na kozi za kitaaluma.

Agizo ni la ubaguzi 

Lakini makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa kuwazuia watoto kuhudhuria masomo kutakuwa na athari mbaya kwa elimu yao kwenye taifa ambalo asilimia 11 ya wasichana kati ya umri wa miaka 15-19 wanajihusisha na vitendo vya ngono. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu.

Baadhi ya watoto wakicheza, Burundi

Baadhi ya watoto wakicheza, Burundi

Marufuku hiyo ya taifa hilo la Afrika Mashariki, inalenga kuwazuia wasichana zaidi ya watoto wa kiume, wanasema wanaharakati wakiongoza kuwa ni rahisi kugundua kuwa mtoto wa kike ni mja mzito, lakini ni vigumu kutambua aliyempa mimba.

Wakili wa kikundi kinachopigana dhidi ya marufuku hiyo Naitore Nyamu-Mathenge, anasema marufuku hiyo inamnyima mtoto wa kike elimu pamoja na kuegemea zaidi upande wake.

Anauliza, "serikali inapanga kuthibitisha vipi kuwa mvulana fulani ndiye msichana fulani mimba, na je itakuaje kwa visa ambavyo walimu na watu wazima katika jamii wamehusika, je serikali itawachukulia hatua pia?"

Juma Eduard ni msemaji katika wizara ya ellimu nchini Burundi, anasema, "tunajiandaa kutekeleza agizo hilo kwa sasa tunasubiri mwelekeo kutoka kwa wizara ya elimu."

Utekelezaji utakuwa na changamoto

Hata hivyo afisa mmoja wa serikali alithibitisha marufuko hiyo, akaongeza kusema kuwa huenda marufuku hiyo isitekelezwe, hata hivyo hakutaka kutambuliwa.

Msichana mdogo akitumia kompyuta

Msichana mdogo akitumia kompyuta

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu UNFPA, asilimia 40 ya watu waliodhalilishwa kingono au kujeruhiwa nchini Burundi ni wasichana. Takriban asilimia saba ya wasichana wa umri wa miaka 15-19 wameza angalau mtoto mmoja. Aidha mmoja kati ya wanawake watano walio chini ya umri wa miaka 18 wameolewa nchini humo.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch linasema kuwa maelfu ya watoto wa kike barani Afrika hutungwa mimba kila mwaka licha ya kuwa wengi wao hawana elimu ya uzazi na katika visa vingine wasichana hao huwa wamebakwa ama kunajisiwa.

Katika mataifa mengine kama vile Tanzania, Sierra Leone na Guinea ya Ikweta, wasichana wajawazito hufukuzwa shuleni kwa lengo la kuzuia vijana kushiriki vitendo vya ngono.

Na mataifa mengine kama vile Morocco na Sudan, hutumia sheria dhidi ya maadili kuwashtaki wasichana waliobaleghe kwa uzinzi, ukiukaji wa maadili au kushiriki ngona nje ya ndoa.

Ripoti hiyo ya Human Rights Watch inaongeza kusema kuwa kila mwaka maelfu ya wasichana hubebeshwa mimba wakati wanastahili kuwa wakijifunza hesabu ya aljebra, historia na stadi za maisha darasani.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com