1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pashinyian kuungwa mkono na chama tawala Armenia

3 Mei 2018

Chama cha Republican kimesema ikiwa kiongozi wa upinzani atasitisha maandamano huenda kikamuunga mkono kutwaa nafasi ya waziri mkuu anayoigombania

https://p.dw.com/p/2x7pN
Armenien Oppositionsführer Nikol Pashinian
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Grits

Mwanasiasa wa ngazi ya juu kutoka chama tawala nchini Armenia amesema chama hicho kitamuunga mkono kiongozi wa upinzani Niko Pahinyan kuwa waziri mkuu ikiwa atawazuia wafuasi wake kuingia mitaani kuandamana. Katika hali ya kutuliza mvutano na vurugu za kisiasa zilizoikumba Armenia kwa kipindi cha wiki kadhaa sasa chama tawala cha Republican kilisema awali kwamba kitamuunga mkono mgombea yeyote aliyeteuliwa kwa thuluthi mora ya kura za wabunge kutwaa nafasi ya waziri mkuu, kiwango ambacho kufikia sasa Pashinyan anadai ameshakipata. Baade Pashinyan aliwatolea mwito wafuasi wake kusimamisha maandamano.

Naibu kiongozi wa chama tawala Armen Ashotyan akihojiwa na shirika la habari la Associated Press alisema tutamsaidia kuhakikisha anachaguliwa ikiwa mitaani maandamano yatasitishwa na kuendelea kuwepo utulivu.Sambamba na hayo kiongozi wa chama hicho tawala leo akasema kwamba nchi hiyo itapata waziri mkuu mpya Mei 8 baada ya wiki mbili za maandamano yaliyoikumba nchi hiyo ambayo ni mshirika wa karibu wa Urusi.

Armenien Opposition Protest in Jerewan
Picha: Reuters/G. Garanich

Matamshi ya Vahram Baghasaryan huenda yakaongeza matumaini ya kupatikana njia ya amani ya kuutatua mgogoro wa kisiasa ambao pia umeitia wasiwasi Urusi.

Kauli hiyo ya Baghdasaryan imekuja baada ya kukutana na Nikol Pashinyan kiongozi wa upinzani ambaye amekuwa akiongoza maandamano dhidi ya kundi la watu wa chache katika chama tawala wanaong'ang'ania madaraka. Chama hicho tawala kimeonekana kubadili msimamo hasa kutokana mwanzoni kumpinga Pashinyan kugombea nafasi hiyo ya waziri mkuu.

Armenien Armenier wählen neues Parlament
Picha: Getty Images/AFP/K. Minasyan

 Msimamo huo mpya wa Republican unaonekana siku moja baada ya wananchi kuitikisa nchi kwa maandamano siku ya Jumatano kwa kuzifunga barabara na njia za reli hatua ambayo ilisababisha sehemu kadhaa za nchi hiyo kushindwa kuendelea na shughuli za maisha. Kwa mujibu wa Baghdasaryan chama cha Republican sasa hakitosimamisha mgombea kuwania nafasi hiyo ya waziri mkuu na badala yake kitamuunga mkono mgombea yoyote atakayeungwa mkono thuluthi moja ya wabunge iwe ni Pashinyan au mtu mwingine yoyote na kufikia tarehe 8 mwezi huu,waziri mkuu mpya atatangazwa. Endapo bunge litashindwa katika jaribio la pili la kumchagua waziri mkuu mpya  tarehe 8 bunge litavunjwa na uchaguzi wa bunge wa mapema utaitishwa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW