Paralympics Beijing. | Michezo | DW | 08.09.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Paralympics Beijing.

Wanariadha walemavu na michezo yao ya Olimpik Beijing.

default

Ufunguzi wa paralympics

Michezo ya olimpik ya walemavu inaendelea Beijing na mabingwa wanasema zana mpya za kiufundi zimenyanyua hadhi ya paralympics-

Brazil imerudi kwenye mkondo wake wa kukata tiketi ya kombe lijalo la dunia nchini Afrika Kusni 2010 baada ya kuizaba jana Chile mabao 3:0.

Tanzania yaikomea Mauritius mabao 4:1 katika kinyanganyiro cha kuania tikiti za kombe la dunia na Zanzibar yafungua mkutano wa kanda wa micheuzo kwa amani.

►◄

Timu mbali mbali za kitaifa ziliteremka uwanjani mwishoni mwa wiki tena katika mabara yote kuania tiketi zao kwa Kombe la dunia 2010 -la kwanza barani Afrika.Kwanza tuanze na maandalizi ya kombe hilo.Kiongozi wa Kamati ya maandalio ya kombe hilo la dunia Danny Jordaan,amezima uvumi kuwa FIFA italihamishia kombe la dunia hilo nchi nyengine.

Jordaan,ameliambia gazeti la BILd la Ujerumani lililotoka leo kwamba ni upumbavu kuzungumzia mahala pengine popote kulihamishia kombe hilo.

Rais wa FIFA Sepp Blatter, atakaezuru Afrika Kusini kukagua zana na viwanja atapofanya ziara ya siku 4 jumapili ijayo,amekuwa akizungumzia "mpango B" endapo wenyeji-Afrika kusini-wakishindwa kulisadikisha Shirikisho la dimba la Dunia FIFA ina uwezo kweli wa kuandaa kombe hilo ipasavyo.

Jordaan alisema hakuna nchi yoyote na hata si Ujerumani itakayomudu kubeba jukumu hilo la kuandaa kombe la dunia kwa muda mfupi uliosalia .Hii haihusiani na kuwa na zana tayari bali matayarisho ya kisheria yanayohusiana na kuandaa kombe la dunia.

Bw.Danny Jordaan akaongeza maandalio ya Afrika Kusini yanasonga mbele kama ilivyopangwa na waandazi wataweza wiki ijayo kumuonesha Bw.Blatter maendeleo yaliofanyika.Viwanja vyote 10 vitakavyochezewa kombe hilo la dunia vitakuwa tayari ifikapo Oktoba 31,mwakani 2009.Muda wa mwisho uliowekwa.

Basi kwa jicho la ahadi hiyo, timu za mabara yote pamoja na Afrika,asia na Ulaya, zilikuwa uwanjani mwishoni mwa wiki kuania tiketi zao:

makamo-bingwa wa Ulaya-Ujerumani hawakuwa na kibarua kigumu jumamosi walipoikomea Lichtenstein mabao 6 bila majibu.Wakati Wales waliitoa katika kundi hili Azerbaijan kwa bao 1:0.Chipukizi wa bayern Munich anaelilia kuihama klabu hiyo,Lukas podolski alitia mabao 2 kati ya 6 ya Ujerumani.

Ujerumani sasa ina miadi na Finland na inaelewa haitajipatia mteremko kama wa jumamosi kutoka kwa nchi ndogo ya Lichtenstein.

Mabingwa wa dunia Itali chini ya kocha wake mpya na wa zamani Marcello Lippi bila ya shaka atafanya mabgeuzi katika kikosi chake kitakachopambana na Georgia hapo jumatano.Kwani, jumamosi Itali ilimudu m,abao 2-1 mbele ya chipukizi Cyprus.Itali haikuweza kutamba pengine kwa kuwa imecheza bila walinzi wake Alessandro Gamberini na Fabio Grosso walioumia.Hata Gattuso ameumia mkono wakati wa mazowezi.

Jumatano hii Itali itakapokutana na Georgia ,kocha Lippi atazamiwa kumwita Antonio Necerino wa Palermo kujaza nafasi ya mchezaji wa kuingo wa AC Milan.

Mabingwa wa Ulaya -Spain chini ya uongozi wa kocha mpya Vicente del Bosque wanajiwinda pia kwa changamoto yao ya jumatano hii na Armenia baada ya kuizaba Bosnia mwishoni mwa wiki bao 1:0.Wabosnia hawakuwapa hatahivyo mteremko wa Spian hadi pale David Villa alipolifumania lango lao mnamo dakika ya 57 ya mchezo.Spian itarajie pia changamoto kali kutoka kwa warmenia waliolazwa na waturuki watakapoonana nao jumatano.

Katika Kanda ya Amerika kusini, mabingwa mara kadhaa wa dunia Brazil,hawakutaka kuvunja rekodi yao ya kutoshiriki katika kombe la dunia,kwani hawakuwahi kukosa kutimiza jukumu hilo tangu lilipoanzishwa Montevideo,Uruguay, 1930.Ingawa kulikua na shaka shaka safari hii, Brazil ilizaba jana Chile mabao 3:0 na hivyo kujiunga tena na safu ya timu 4 au 5 za kanda ya Amerika kusini kwa kombe la dunia.hapo kabla ilionesha kana kwamba Brazil mara hii ingelikosa tiketi yake ya kombe la dunia.

Baada ya mapambano 7,Paraguay ndio iliopo kileleni ikiwa na pointi 14 ikifuatwa sasa na Brazil na Argentina zenye pointi 12 kila moja.Uruguay ina pointi 11 wakati Chile na Columbia zina pointi 10.Robinho aliueleza mpambano wa jana kuwa ni miongoni mwa mchezo bora kabisa Brazil iliounesha.

Katika kanda ya Afrika,Tanzania isio na matumaini ya kwenda Afrika kusini kwa kombe la dunia,hatahivyo ilikuwa na miadi na Mauritius.Baada ya kutoka suluhu nyumbani Dar-es-salaam, mara hii Taifa Stars ilitamba kwa mabao 4:1.

Hii ilimpa kocha wao mbrazil Maximo matumaini kwa changamoto ijayo na Sudan .

Michezo ya olimpik ya walemavu ilifznguliwa rasmi na kwa shangwe na shamra shamra takriban kama ile tuliojionea August 8 mjini Beijing.

Rais wa Ujerumani Horst Kłhler, alihudhuria sherehe hizo za ufunguzi hapo jumamosi

Alisema:

"Daima ilikua muhimu kwangu kuhudhuria michezo hii ya walemavu ya olimpik.Nimempongeza rais wa China kwa sherehe maridadi na za kuvutia za ufunguzi na tunakubaliana kuwa michezo hii itumikie lengo lake na sio tu kwa China pekee bali kwa ulimwengu mzima kutoa ishara kwa walemavu kwamba mchango wao pia unahitajika kuonesha uhodari wao na kutambuliwa."

Alisema rais Kłhler wa Ujerumani huko Beijing.

Medali zimeshaanza kutolewa na alao moja kutoka mashindano ya kupanda farasi imekuja Ujerumani.

Kwa jumla zana zinazotumiwa na walemavu zimeongoza katika maendeleo makubwa ya michezo hii ya "paralympics" mnamo miaka michache iliopita.Kimsingi michezo ya walemavu imefanyiwa mapinduzi makubwa kwa matumizi ya vigari vya kukalia vya magurudumu-wheelchair. Vigari vya aina mbali mbali vimetengezwa kuandamana na mchezo wenyewe.Kunavigari vyakuwawezesha walemavu kushindana katika mchezo wa Tennis.katika mbio za baiskeli za kuendesha kwa mkpno-handbike pia yamefanyika maendeleo.

Maendeleo makubwa kabisa mnamo miaka 15 iliopita bila shaka ni chombo kinachomuwezesha mwanariadha kiwete wa Afrika kusini kukimbia kwa kasi sana kana kwsamba ana miguu 2 ya kawaida.Mwanariadha Oscar Pisttorius amekuwa akigonga vichwa vya habari huku wengine wakidai zana anazotumia zinampa nafuu zaidi kupita wenzake.

"Blade Runner" kama anavyoitwa muafrika kusini huyo alitaka kushiriki katika mbio za mita 400 za Beijing.Hii inafuatia ushindi wake katika mashindano ya riadha ya kitaifa ya Afrika kusini mwaka uliopita.Alishindwa kuchaguliwa katika timu ya olimpik ya Afrika kusini,hatahivyo amebakiwa na kiu cha kutaka kushiriki katika michezo ya Olimpik ijayo mjini London, 2012.Hii inaonesha jinsi maendeleo ya kiufundi yalivyofikia kumwezesha mwanariadha mlemavu kuweza kufikia uwezo wa kukimbia na hata kuwashinda wanariadha wasiowalemavu.

Maendeleo ya kiufundi katika zana mbali mbali za michezo kwa walemavu zitawasaidia walemavu kushindana barabara na kuwapa nao fursa ya kufurahia michezo kama wenzao wasio walemavu badala ya kukaa nje ya chaki za viwanja kama zamani.

Michezo hii ya walemavu ya olimpik, inaendelea hadi Septemba 17 na wenyeji China, wanatarajiwa kunyakua medali nyingi kabisa za dhahabu pengine hata kupita zile 51 walizotwaa wiki 2 zilizopita wakati wa michezo ya 29 ya Olimpik ya majira ya kiangazi.

USA-OPEN-WOMEN TENNIS:

Msichana wa Kimarekani Serena Williams ametamba tena baada ya jana kumtimua nje Jelena Jankovic kwa seti mbili: 6-4 na 7-5 na kutwaa sio tu taji la US Open bali pia la malkia nambari 1 wa Tennis duniani kwa kumpiku Ana Ivanovic.

Hii ni mara ya 9 kwa malkia 2 wa Tennis kugombea taji la "Grand slam" ili kuparamia kileleni mwa ngazi ya dunia.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com