Operesheni ya kuwasaka washukiwa wa ugaidi yashika kasi | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.01.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Operesheni ya kuwasaka washukiwa wa ugaidi yashika kasi

Washukiwa wawili wanaodaiwa kushambulia jarida la Charlie Hebdo nchini Ufaransa na kusababisha vifo vya watu 12 wanasemekana kuiba gari moja na kuelekea Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Baadhi ya wanajeshi wanaowasaka washukiwa wa shambulio dhidi ya Charlie Hebdo

Baadhi ya wanajeshi wanaowasaka washukiwa wa shambulio dhidi ya Charlie Hebdo

Maafisa wanasema Ndugu hao wawili wanaoaminika kuwa na mafungamano na kundi la al Qaida waliiba gari aina ya Peugeot hii leo asubuhi katika mji wa Montagny Sainte Felicite, ulioko umbali wa kilomita 50 kaskazini-mashariki mwa mji mkuu wa Ufaransa Paris.

Aidha kituo kimoja cha televisheni nchini Ufaransa BFM kimeripoti kuchukuliwa mateka kwa mtu mmoja mjini Dammartin-en-Goele na kuripoti pia juu ya ufayatulianaji risasi kati ya polisi na watu ambao wanadaiwa kuwa washukiwa wa shambulio la kigaidi dhidi ya Jarida la Charlie Hebdo.

Wanajeshi wa angani pia wameshiriki katika juhudi za kuwatafuta washukiwa wa Ugaidi

Wanajeshi wa angani pia wameshiriki katika juhudi za kuwatafuta washukiwa wa Ugaidi

Kituo hicho pia kimeripoti kuuwawa kwa mtu mmoja katika mapambano hayo lakini waendesha mashtaka wa Ufaransa wamekanusha madai hayo. Polisi kwa upande wao wanasema wanajaribu kuzuwiya shambulizi jengine kutekelezwa na ndugu hao wanaosemekana kuwa hatari na waliojihami kwa silaha.

Mkaazi mmoja wa eneo hilo amesema kile anachokiona kwa sasa ni kama eneo la vita kufuatia helikopta tano kupaa angani huku magari ya polisi yakienda kwa kasi kote katika kijiji hicho, huku polisi na wanajeshi wengine wakiingia katika maeneo yote ya kijiji hicho kuwasaka washukiwa walioshambulia jarida la Charlie Hebdo siku ya Jumatano.

Vitisho kwa Jarida la Charlie Hebdo

Jarida hilo la kila wiki limekuwa likitishwa mara kwa mara baada ya kuchora kibonzo kilichomkejeli mtume wa dini ya kiislamu, mtume Mohammad. Wakati wa shambulizi hilo siku ya Jumatano washukiwa hao walisema wamelipiza kisasi kufuatia kuchorwa kwa kibonzo hicho.

Afisa mkuu wa Marekani amesema Said Kouachi aliwahi kusafiri nchini Yemen lakini haijajulikana wazi iwapo alikuwa huko kujiunga na makundi yalio na itikadi kali kama Al Qaida katika rasi ya kiarabu ambao wapo katika eneo.

Ujumbe unaosema mimi ni Charlie JE SUIS CHARLIE

Ujumbe unaosema mimi ni Charlie "JE SUIS CHARLIE"

Kakaake Cherif Kouachi alitiwa hatiani mwaka 2008 kwa makosa ya kuhusika katika visa vya ugaidi kwa kutuma wapiganaji nchini Iraq kupambana na wanajeshi wa Marekani. Wote walikuwa katika orodha ya marekani ya watu wasiokubalika kusafiri nchini humo.

Katika kisa hiki mshambuliaji wa tatu kijana aliye na miaka 18 Mourad Hamyd, alijisalimisha kwa polisi baada ya kugundua kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwamba jina lake lilitajwa kuwa miongoni mwa washambuliaji wa ofisi za jarida la Charlie Hebdo. Mahusiano yake na washukiwa hao wawili bado hayajajulikana.

Maelfu ya wanajeshina polisi washiriki katika oparesheni ya kuwatafuta magaidi

Zaidi ya polisi na wanajeshi 88,000 wamesambazwa katika maeneo tofauti nchini Ufaransa ili kuwatafuta washukiwa Cherif Kouachi, aliye na miaka 32, na kakaake Said Kouachi, aliye na miaka 34.

Hadi sasa watu tisa wa familia ya washukiwa hao wanazuiliwa na kuhojiwa na polisi. Kulingana na Waziri wa ndani wa ufaransa Bernard Cazeneuve, watu wengine 90 wengi wao walioshuhudia shambulio la siku ya Jumatano wamehojiwa ili kutoa habari zaidi juu ya washambuliaji.

Washukia wa shambulio dhidi ya Charlie Hebdo Cherif Kouachi na Said Kouachi

Washukia wa shambulio dhidi ya Charlie Hebdo Cherif Kouachi na Said Kouachi

"Hatua hizi zimetuongoza kwa siku nzima hapo jana kupata habari muhimu katika uchunguzi wetu. Operesheni ya kuwasaka inaendelea kwa sasa katika eneo la Dammartin en Goele, inavilete pamoja vikosi vyote husika katika eneo hilo," alisema Waziri Bernard Cazeneuve.

Huku hayo yakiarifiwa Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameendelea kutoa wito wa kuvumiliana baada ya shambulio hilo alilolitaja kuwa baya zaidi kutokea nchini humo baada ya miongo kadhaa. Kwengineko Umoja wa Ulaya umepanga kujadili jinsi ya kuongeza juhudi za kukabiliana na ugaidi katika mkutano wake unaotarajiwa kufanyika tarehe 12 mwezi huu.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/dpa/Reuters

Mhariri Iddi Ssessanga

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com