Olimpik Beijing isusiwe ? | Michezo | DW | 24.03.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Olimpik Beijing isusiwe ?

Vilio vya kuisusia michezo ya olimpik ya Beijing vinahanikiza kutokana na mkomoto wa China huko Tibet.

Dalai Lama atetea haki za watibeti.

Dalai Lama atetea haki za watibeti.

Mwenge wa michezo ijayo ya olimpik mjini Beijing uliashwa jana huko Olympia,Ugiriki,asili ya michezo hii na umeanza safarfi yake ndefu hadi utakapowasili Beijing,siku 2 kabla ufunguzi rasmi wa michezo hiyo hapo August,8.

Sherehe ya jana huko Ugiriki ilichafuliwa na waandamanaji 2 walioingia uwanjani huko Olympia wakati wa sheherhe ya kuasha mwenge huo.

Kisa hicho kilitokea pale mwenyekiti wa Kamati ya maandalio ya olimpik mjini Beijing, Liu Qi akihutubia.

Vilio vimekua vikisikika tangu kutoka kwa wakereketwa wa haki za binadamu hata wanasiasa kudai michezo ya Olimpik ya Beijing isusiwe.Kuna wengine wanaodai usichanganye siasa na michezo.

Wale wanaotetea kutoingizwa siasa katika olimpik kama vile rais wa zamani wa Halmashauri Kuu ya olimpik ulimwenguni (IOC ) marehemu Avery Brundage wa Marekani ,wakiwakumbusha walimwengu kwamba katika zama za kale za olimpik uhasama wowote uliokuwapo kati ya makabila ukiwekwa kando ili kuruhusu michezo hii kufanyika.Amani ikitanda.

Leo hii wanadamu wanaweka olimpik kando,alisema Brundage,ili kupigana vita -kinyume cha maadili ya olimpik.

Siasa na olimpik kwa kweli,ilianzia katika michezo ya kwanza kabisa ya kisasa ya olimpik ilioandaliwa Athens,mji mkuu wa Ugiriki.Wagiriki binafsi walichagua siku ya ufunguzi wa michezo hiyo ile siku ya kutimu mwaka wa 100 tangu Ugiriki kukombolewa kutoka utawala wa waturuki.Kwanini siku hiyo-ikiwa si kuingiza siasa katika olimpik ?

Labda karibuni kabisa ni michezo ya Olimpik ya Mexico City, 1968 pale nchi za kiafrika zilipotishia kuisusia michezo ile ikiwa Afrika kusini ,moja kati ya nchi zilizoasisi michezo ya kisasa ya olimpik,1896, ingeruhusiwa kushiriki kutokana na siasa zake za ubaguzi hata katika spoti.(Aparthied).

Waamerika 2 weusi John Carlos na mwenzake baada ya kumaliza washjindi wa kwanza na wapilikatika mita 200,walitoa black-power-salute wakiviringa ngumi hewani

huku wakiwa jukwaani.

Halmashauri kuu ya olimpik ikikasirika na kitendo chao iliwatimua nje ya Olimpik ,lakini Afrika kusini haikushiriki.Huo ukawa ushindi wa kwanza kwa afrika na washirika wao katika kucheza siasa katika medani ya olimpik.

Wakitiwa shime kwa ushindi huo,nchi za kiafrika zikiwakilishwa na Baraza kuu la michezo barani Afrika-The Supreme Council for Sports in Africa- zikatumia tena silaha ya kuisusia michezo ya olimpik ya Munich,1972 ikiwa mara hii Rhodesia ya Ian Smith (leo Zimbabwe) ingeruhusiwa kushiriki.

Kwa mara nyengine tena kama Mexico 1968,Afrika na washirima wao ilifanikiwa.

Utamu wa kucheza siasa katika olimpik ulipowakolea ,waafrika wakajaribu tena mara ya 3 kususia michezo ya Olimpik ya 1996 mjini Montreal kanada.

Mojawapo ya changamoto za mashindano yale ilikua mpambano katika mita 1.500 (metric mile) kati ya mtanzania Philbert Bayi na Mnew Zealand,John Walker.

Mara hii ilikua kuisusia New Zealand isishiriki kwenye Olimpik kwa kuwa timu yake ya rugby-All-Blacks" ilikwenda kucheza rugby Afrika kusini mara tu baada ya machafuko ya Soweto.

Ikikosa kuungwamkono na washirika walioiungamkono Afrika huko Mexico na Munich, ilikua Afrika iliokaa nje ya olimpik huko Montreal 1976.

Hii ilizusha athari kubwa kwa nguvu za wanariadha wa Afrika kama vile akina Henry Rono na Mike Boit wa Kenya lakini pia John Akii-bua wa Uganda -bingwa wa Olimpik wa Munich alietaka kutetea taji lake.Nusu ya mataifa ya afrika yalisusia Montreal.

1980 mchango wa siasa katika Olimpik ulitolewa na Marekani na baadhi ya washirika wake kususia michezo ya olimpik ya Moscow.sababu ni uvamizi wa 1979 wa Urusi nchini Afghanistan.

Urusi na washirika wake wakalipiza kisasi miaka 4 baadae,pale michezo ya olimpik ilipohamia Los Angeles,1984.

Ni kuanzia hapo -michezo ya olimpik ya Seoul 1988 hadi ijayo ya beijing 2008 ndipo jiinamizi la siasa na olimpik lajitokeza tena:

Akijitahidi kuzima kitisho cha mgomo rais wa sasa wa IOC-Halmashauri kuu ya olimpik ulimwenguni,Jacques Rogge alisema jana kwamba haoni ishara ya mwito wa kususia michezo ya olimpik ya beijing mwaka huu kuungwamkono ulimwenguni kwa kuwa China inakanyaga haki za binadamu huko Tibet.

Rogge,mbelgiji, alikumbusha kwamba hata vigogo vikubwa vya kisiasa vinapinga kususia michezo ya Beijing:

"Bush wa Marekani hataki mgomo;Sarkozy wa Ufaransa vivyo hivyo kama waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown."

Vikundi vya wakereketwa vimepanga mipango ya kuichafua michezo ya beijing kwa tuhuma za kuwa China inakanyaga ama haki za binadamu huko Tibet na hata kwa kutomshinikiza mshirika wake Sudan kwa kukanyaga haki za binadamu mkoani Dafur.

Mvutano kati ya wale wanaoungamkono kususia michezo ya olimpik ya Beijing na wale wanaopinga kutia siasa katika michezo utaendelea kama historia ya michezo hii iliofufuliwa na mfaransa Pierre Coubertin,ilivyoonesha.

Pande zote mbili zisisahau mila na maadili ya olimpik : "wakati wa olimpik uhasama huwekwa kando alao kwa muda wa olimpik na amani hutanda."