Obama kufanya ziara ya kistoria nchini Cuba | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.02.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama kufanya ziara ya kistoria nchini Cuba

Rais Barrack Obama ametangaza kwamba atafanya ziara ya kihistoria nchini Cuba kuanzia wiki zijazo. Obama atakuwa rais wa kwanza wa Marekani aliyeko madarakani kukanyaga ardhi ya nchi hiyo baada ya miongo saba.

Rasi wa Cuba Raul Castro na mwenzake wa Marekani Barrack Obama

Rasi wa Cuba Raul Castro na mwenzake wa Marekani Barrack Obama

Ziara hiyo fupi inayotarajiwa kufanyika mwezi Machi mwaka huu inaonekana kufungua ukurasa mpya katika mahusiano baina ya Marekani na Cuba, taifa la kikomunisti lililokata mahusiano yake na Marekani kwa muda wa zaidi ya nusu karne, hadi pale Obama na rais wa Cuba Raul Castro walipochukua hatua za kufufua mahusiano hayo mwaka uliopita.

Tangu wakati huo mataifa yote mawili yamefungua balozi zake mjini Washington na Havana na wamejaribu kufufua safari za ndege huku ziara ya rais Obama ikiangaliwa kama hatua muhimu ya kumaliza tofauti zilizopo.

Rais wa Cuba Raul Castro

Rais wa Cuba Raul Castro

Ziara hiyo fupi ya rais Obama mjini Cuba, ni sehemu ya ratiba ndefu ya ziara katika mataifa ya Amerika Kusini mwezi ujao.

Japokuwa Obama alitarajiwa kufanya ziara yake nchini Cuba katika mwaka wake wa mwisho wa utawala wake, mipango ya ziara yake hiyo ilipingwa kutoka kwa wapinzani wake wanaopinga mahusiano mema kati ya Marekani na Cuba, akiwemo wagombea wa urais wa chama cha Republikan.

Seneta wa Texas Ted Cruz, ambaye babake alitorokea Marekani kutoka Cuba mwaka wa 1950 amesema Obama hapaswi kutembelea taifa hilo wakati familia ya Castro ikiwa bado madarakani.

Naye seneta wa Florida Marco Rubio, mtoto mwengine wa mhamiaji wa Marekani kutoka Cuba alimshambulia rais kwa kile alichokisema kuwa Obama anapanga kufanya ziara katika nchi ya kidikteta isiyoipenda Marekani.

Obama ana nia ya kufufua mahusiano ya kiuchumi na kidiplomasia na Cuba

Huku rais huyo wa Marekani akibakiwa na chini ya mwaka mmoja madarakani amekuwa na hamu ya kupiga hatua za haraka za kufufua mahusiano ya kiuchumi na kidiplomasia ili kuanzisha rasmi mahusiano mema kati ya taifa hilo na utawala wa Marekani.

Kufuatia majadiliano ya kisiri kati ya serikali za nchi hizo mbili Obama na Castro walitangaza mwishoni mwa mwaka wa 2014 kwamba wataanza kusawazisha mahusiano yao na miezi michache baadaye wakawa na mkutano wa ana kwa ana kati ya rais wa Marekani na Cuba tangu mwaka wa 1958.

Rais wa Marekani Barrack Obama

Rais wa Marekani Barrack Obama

Aidha upinzani unasema kuiondolea Cuba vikwazo ni kuizawadia nchi ambayo bado inaendelea na udhalilishwaji wa haki za binaadamu na kuweka vikwazo katika hatua za kidemokrasia.

Aidha kwa Obama kufungua njia za kidiplomasia inaashirikia mafanikio makubwa katika sera yake ya kigeni iliyowekwa kwa kuamini kwamba ni lazima Marekani ijaribu njia ya kupunguza uhasama na maadui zake wa zamani.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com