Obama awahutubia waislam | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.06.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama awahutubia waislam

Rais awasihi waislam waweke kando hitilafu za miongo iliyopita na washirikiane na Marekani

Rais Barack Obama akiwahutubia waislam wa dunia mjini Cairo

Rais Barack Obama akiwahutubia waislam wa dunia mjini Cairo

Katika hotuba yake katika chuo kikuu cha Cairo hii leo,rais Barack Obama ameshauri ufungwe "ukurasa wa enzi za kutoaminiana na kutoelewana" katika uhusiano kati ya Marekani na ulimwengu wa kiislam na kumaliza ugonvi kati ya Israel na Palastina.

Baada ya kushukuria mapokezi mema aliyoyapata nchini Misri,rais Barack Obama alianza hotuba yake katika chuo kikuu cha Al Azhar mjini Cairo, kwa waislaam zaidi ya bilioni moja na nusu duniani kwa kuwatolea salam na kusema:

Assalam Aleykum"..........

Rais Obama amehimiza enzi za kutoaminiana na kutoelewana zikome:

"Nimekuja kutafuta njia mpya ya kufuatwa na Marekani na waislam kote ulimwenguni.Njia itayakojengeka katika misingi ya masilahi ya pamoja na kuheshimiana.Njia itakayojengeka katika misingi ya ukweli ambayo haiitenganishi Marekani na dini ya kiislam na wala haileti mashindano kati yao.Badala yake inaleta uwiano na kushadidia misingi ya pamoja ambayo ni misingi ya haki,maendeleo,ustahamalivu na hadhi ya binaadam".

Akinukuu Qoraani Obama amesema anataka kuelezea ukweli kuhusu masuala yote yanayozusha mijadala au yaliyozusha mfarakano kati ya Marekani,na ulimwengu wa kiarabu na kiislam.Rais Barack Obama amesema:

"Kama Qoraan inavyosema,mche Mungu na daima sema ukweli"

Mfarakano ulipata nguvu baada ya vita vya Irak,kashfa ya jela ya Abu Ghraib nchini Irak,kambi ya Guantanamo na sera za rais wa zamani wa Marekani George W. Bush baada ya mashambulio ya kigaidi ya seeptember 11 mwaka 2001.

Rais Obama amezungumzia pia umuhimu kwa nchi za kiislam kuondokana na "hisia za uwovu dhidi ya Marekani.Amegusia pia masuala ya haki za binaadam,na haki ya wakinamama kujichagulia wenyewe wakitakacho katika jamii ya kiislam."

Barack Obama in Cairo

Rais Obama anakumbusha kilichotajwa ndani ya Qoraan

Kuhusu suala tete la ugonvi kati ya Israel na wapalastina,rais Obama amezungumzia umuhimu wa kupatikana ufumbuzi wa madola mawili akisisitiza "hiyo ndiyo njia pekee baada ya miongo ya mivutano ,vilio na damu kumwagika."

Na huku akiwasuta wale wanaoshuku mauwaji ya halaiki ya wayahudi Holocaust na kushadidia mafungamano yasiyotetereka kati ya nchi yake na Israel,rais Obama amesema hata hivyo "wakati umewadia wa kusitishwa ujenzi wa makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi katika ukingo wa magharibi.

Na ingawa rais Obama ametetea sera za Marekani na washirika wake nchini Afghanistan,hata hivyo ameonekana kukosoa kwa namna fulani vita vya Irak na kuahidi nchi yake itaendeleza demokrasia ya uwazi inayotanguliza mbele mashauriano.

Rais Barack Obama amezitolea mwito pande zote mbili,Marekani na ulimwengu wa kiislam,zishirikiane katika kupambana kwa pamoja na wafuasi wa itikadi kali wa pande zote mbili.

Na kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran,ameitolea mwito Iran iachane na miongo kadhaa ya kutoaminiana,akikiri wakati huo huo makosa yaliyofanywa zamani na Marekani.

"Tunapendelea kusonga mbele bila ya masharti kwa misingi ya kuheshimiana" amesema rais Obama.

Ziara ya saa sabaa ya rais Obama mjini Cairo,ambayo vyombo vya habari vya Misri vinaitaja kua ni ya kihistoria itamalizika baadae leo usiku,wakati atakapoondoka Mashariki ya kati na kuelekea Ujerumani.


Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman

 • Tarehe 04.06.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/I3WL
 • Tarehe 04.06.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/I3WL
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com