1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni kulia ama kucheka kipute cha PL kinapomalizika

26 Julai 2020

Chelsea, Manchester United na Leicester City wanachuana vikali kusaka nafasi ya kushiriki michuano ya klabu bingwa Ulaya, huku Aston Villa, Watford na Bournamouth wakipambana kuepuka kushuka daraja.

https://p.dw.com/p/3fvCW
Grossbritannien | Manchester United | Marcus Rashford
Marcus Rashford, kinda anayetegemewa sana kwenye kikosi cha United.Picha: picture-alliance/dpa/M. Rickett

Msimu mrefu kabisa wa ligi kuu ya England, Premier League, PL unamalizika hii leo na mechi zenye msisimko wakati Chelsea, Manchester United na Leicester City wakichuana vikali kusaka nafasi ya kushiriki michuano ya klabu bingwa Ulaya, wakati Aston Villa, Watford na Bournemouth zikipambana kuepuka kushuka daraja.

Msimu wa 2019-2020 hatimaye utafikia tamati baada ya kusimama kwa miezi mitatu kufuatia janga la virusi vya corona, katika wakati ambapo klabu za PL kawaida huwa kwenye ziara za kujiweka sawa msimu mpya.

Klabu ya Liverpool tayari imekwishakabidhiwa kombe la ubingwa wa ligi, na Manchester City iliyoshika nafasi ya pili inapigiwa chapuo la kunyakua ubingwa wa michuano ya klabu bingwa Ulaya. Norwich wao wameiaga ligi kuu baada ya kushuka daraja. Lakini kuna masuala muhimu ambayo bado hayajapatiwa suluhu.

Großbritannien Fußball | Manchester City | Logo Etihad Airways
Kikosi cha Manchester City chapigiwa chapuo la kuchukua ubingwa wa Champions.Picha: picture-alliance/dpa/Offside Sports Photography/S. Stacpoole

Katika raundi ya mwisho na yenye mvuto, vilabu viinavyoshika nafasi nne za juu, vitakavyoshiriki ligi ya Europa, vile vinavyoshuka daraja na kiatu cha dhahabu, vyote vinatakiwa kuhitimishwa katika raundi hiyo ya mwisho.

Ni Man United au Chelsea?

Lakini macho yote yataelekezwa kwenye uwanja wa King Power, ambako Manchester United inayoshika nafasi ya tatu itakapokuwa ikimenyana na Leicester ambao ni wenyeji na wanaokamata nafasi ya tano.

Kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer kitarejea kwenye michuano ya klabu bingwa Ulaya baada ya kushindwa kushiriki kwa mwaka mmoja, iwapo watashinda mechi hii. Lakini iwapo Leicester itashinda, Manchester United watashiriki michuano ya Europa kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2016-17.

Kikosi cha United kilionekana kuwa na uchovu wiki iliyopita, lakini Solskjaer aliwaomba wachezaji wake kumaliza kazi waliyoianza baada ya kupanda hadi nafasi ya nne kwa mara ya kwanza tangu mwezi September iliyopita.

"Tunausubiri kwa hamu mchezo huu, tumejipa nafasi nzuri kabisa ya kushiriki ligi ya Champions mwakani" alisema Solskjaer. Tunataka kwenda pale na kuudhibiti mchezo, hatuendi kubadilisha mkakati wetu".

Chelsea inayoshika nafasi ya nne inahitaji pointi inapocheza nyumbani dhidi ya Wolves ili kujithibitishia kusalia kwenye nafasi hiyo, lakini iwapo kikosi hicho cha Frank Lampard kikishindwa, basi ni dhahiri kwamba hata droo kati ya Leicester na United itavipa fursa vikosi hivyo viwili kufuzu kushiriki michuano ya Champions.

UEFA Champions League | FC Chelsea - Bayern München | Frank Lampard, Trainer
Kocha wa Chelsea, Frank Lampard na kikosi chake wanahitaji pointi kujihakikishia "Champions"Picha: Reuters/M. Childs

Itakuwa ni siku ngumu kwa Lampard, lakini atatakiwa kuwa na matumaini. "Tunajua mambo yalivyo, lakini tutajaribu kushinda". Sidhani kama kuna namna nyingine ya kucheza mchezo huu", alisema Lampard.

Kwa yoyote atakayeikosa michuano ya Champions kati ya United, Chelsea na Leicester atasalia nafasi ya tano na atafuzu kushiriki msumu ujao wa ligi ya Europa. Wolves inayoshika nafasi ya sita, itakuwa na uhakika wa kushiriki ligi hiyo iwapo itaifunga Chelsea.

Na mambo yakoje kwenye timu zinazoshika mkia?

Hata hivyo, kushindwa kwao kutawafungulia njia Totenham Hotspur kuwa juu yao iwapo wataibuka na ushindi dhidi ya Crystal Palace, ambao wamepoteza katika mechi saba zilizopita.

Huko mkiani, klabu ya nne kutoka mwisho Aston Villa, watakabiliana na West Ham huku wakijua fika kwamba watakuwa salama iwapo matokeo yao yatafanana na ya Watford ambayo ni ya tatu kutoka mwisho na inayokutana na Arsenal. Hata hivyo, Villa ina idadi kubwa ya magoli.

Lakini hata kama timu zote zitashinda, Watford ambayo haina meneja wa kudumu baada ya Nigel Pearson kutimuliwa huenda wakaepuka kushuka daraja iwapo ushindi wao utakuwa mzuri kuliko wa Villa.

Iwapo Villa na Watford watashindwa, basi Bournemouth ambayo ni ya pili kutoka mwisho ambayo ina upungufu wa pointi tatu inaweza kuepuka kushuka daraja kwa tofauti ya magoli iwapo watafanikiwa kuifunga Everton. Meneja wa Bournemouth Eddie Howe alinukuliwa akisema "Mchezo ujao ni muhimu sana kwao".

Jamie Vardy wa Leicester anaongoza kwa wingi wa magoli katika msimu huu akiwa amefunga magoli 23, mawili mbele ya Danny Ings wa Southampton.

Mashirika: AFPE