Champions League yarejea uwanjani | Michezo | DW | 12.02.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Champions League yarejea uwanjani

Champions League inarejea uwanjani katika michuano ya 16 bora kuanzia kesho Jumanne, na katika bara la Afrika, michuano ya Champions League na ile ya kombe la shirikisho yaanza katika awamu ya awali.

Ligi  ya   mabingwa  barani  Ulaya  inarejea  uwanjani  kesho Jumanne,  ambapo michezo  miwili  itarindima  uwanjani na  kisha keshokutwa  Jumatano  viwanja  viwili tena   vinatarajiwa  kuwaka moto.

Mabingwa mara  mbili  wa  taji  hilo  la  Champions League  barani Ulaya Juventus Turin wataoneshana  kazi kesho  Jumanne  na  timu inayoonesha  kung'ara katika  Premier League  ya  England Tottenham Hot Spurs  katika  pambano  lao la  kwanza  katika kinyang'anyiro  hicho. Washambuliaji  hatari Harry Kane  wa  Spurs na  Gonzalo Higuain  wa  Juve  watakuwa  kivutio  kikubwa  katika pambano  hilo la  timu  16  zilizobakia  katika  kinyang'anyiro  hicho.

Fußball Premier League - Harry Kane (picture-alliance/Actionplus)

Mshambuliaji wa Spurs Harry Kane

Manchester City  ambayo  ina paa  katika  Premier League ya England  nayo  inafunga  safari  kwenda  mjini  Basel  kutiana  kifuani na  kikosi  cha  Basel  ya  Uswisi. Siku  ya  Jumatano  itakuwa  zamu ya FC Porto  ya  Ureno  ikiikaribisha  Liverpool ya  Uingereza  pia , na  siku  hiyo  hiyo  itakuwa  lile  pambano  baina  ya misumeno mikali ya  kukata  minyororo  wa  ulinzi. Real Madrid  itaikaribisha Paris Saint Germain  ya  Ufaransa. Cristiano Ronald akiongoza kundi  la  washambuliaji Kareem Benzema  na  Gareth Bale , wakati Neymar  ataliongoza  kundi  la  kina Kylian  Mbappe  na  Edinson Cavanni.

Jumanne  ijayo shughuli itahamia  mjini  London  ambapo Chelsea itaikaribisha FC Barcelona na  Bayern  ya  Ujerumani inaikaribisha Besiktas  ya  Uturuki  na  siku  inayofuata  Jumatano FC Sevilla itapimana  nguvu  na  Manchester United , na Schaktar  Donezk   ya Ukraine itaikaribisha  AS Roma  ya  Italia.

Fußball UEFA Champions League RSC Anderlecht - Paris Saint-Germain (picture-alliance/Zumapress/M. Ciambelli)

Washambuliaji watatu wa PSG , Cavani, Mbappe na Neymar

Barani Afrika

Na  katika  bara  la  Afrika  michuano  ya  awali  ya  kombe  la Champions League  ilifanyika  mwishoni  mwa  juma, ambapo nchini Nigeria  timu  ngeni  katika  kinyang'anyiro  hicho  Plateau United iliishinda  bila  taabu  na Mountain of Fire , Mlima  wa  Moto MFM ikitoka  sare ugenini. Plateau  ikiishinda  Eding Sport  wa  Cameroon kwa  mabao 3-0  na MFM ilitoka  sare  ya  bao 1-1  na  Real Bamako ya  Mali.

Kiungo  mchezeshaji  wa  Manchester City Kevin De Bruyne anaweza  kuwa  mmoja  kati  ya  wachezaji  watakaowania kwa karibu tuzo  ya  mpira  wa  dhahabu Ballon d'Or iwapo  timu  hiyo itashinda  mataji  makubwa, kwa  mujibu  wa  kocha  wake Pep Guardiola. De Bruyne  amekuwa  muhimu  katika  msimu  huu ambapo City imekuwa  ikitawala ambapo mchezaji  huyo  mwenye umri  wa  miaka 26 akitoa usaidizi  wa  kufunga  mabao  mara  14 ikiwa  ni  kiwango  cha  juu  katika  ligi  hiyo ikiwa  ni  pamoja  kutoa usaidizi  wa  mabao 3 katika  kipingo  walichoiangushia  Leicester City  cha  mabao 5-1 mwishoni  mwa  juma.

Fußball Champions League Manchester City v Paris St Germain Kevin De Bruyne (Reuters/A. Yates)

Mchezaji wa kati wa Manchester City akifurahia bao

Nae kocha  wa  Liverpool Juergen Klopp amemmwagia  sifa mlinzi Virgil van Dijk kwa  utulivu aliokuwa  nao  katika  pambano  la  jana Jumapili  ambapo Liverpool  iliishinda  Southampton  kwa  mabao 2-0 wakati  mdachi  huyo  aliporejea kwa  mara  ya  kwanza  kwa mwajiri wake  wa  zamani  kabla  ya  kuhamia  Liverpool.

Kocha  wa  Leicester City Claude Puel anaamini  mgomo  wa  siku 10  wa winga machachari Riyad Mahrez  ilikuwa  ni  kosa na ana matumaini  kwamba  kila  mmoja  atajitoa  kutoka  katika tukio  hilo na  kusonga  mbele. Mahrez  alirejea  kufanya  tena  mazowezi  na timu  hiyo  siku  ya  Ijumaa kwa  mara  ya  kwanza tangu  pale alipotoa  ombi  la  kutaka  kuihama  timu  hiyo mwezi  uliopita huku vyombo  vya  habari  vikisema mchezaji  huyo amefadhaika  sana baada ya  kushindwa  kuhamia  Manchester City.

 

Mwandishi:   Sekione  Kitojo / dpae / afpe / rtre

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com