Ndoto ya King haikukamilika | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.08.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ndoto ya King haikukamilika

Maelfu kwa maelfu ya watu wameandamana kwenye kituo cha Kumbukumbu cha Martin Luther King Jr. mjini Washington hapo Jumamosi (25.08.2013) kuadhimisha miaka 50 ya hotuba yake "Nina Ndoto" na kuahidi kutekeleza dira yake.

Maadamano ya miaka 50 ya hotuba ya King.

Maadamano ya miaka 50 ya hotuba ya King.

Pia kumetolewa wito wa kuchukuliwa hatua za kuleta ajira,kuheshimiwa kwa haki za kupiga kura na kutokomeza matumizi ya nguvu ya silaha.

Tukio hilo ni la kutowa heshima kwa kizazi cha wanaharakati ambacho kimevumilia madhila ya polisi na kudunishwa kwa utu wao ili kupigania usawa kwa Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.Lakini kuna mada nzito kwamba kazi hiyo haikukamilika ambapo waliotowa hotuba zao wamelalamika kwamba wanaona kuwepo kwa mashambulizi mapya dhidi ya haki za kiraia.

Ndoto ya King haikukamilika

Maadamano ya miaka 50 ya sehemu ya maadhimisho ya hotuba ya Martin Luther King Jr. mjini Washington-24.08.2013

Maadamano ya miaka 50 ya sehemu ya maadhimisho ya hotuba ya Martin Luther King Jr. mjini Washington-24.08.2013

Martin Luther King wa Tatu ambaye ni mtoto wa kwanza wa mtetezi huyo wa haki za kiraia aliyeuwawa amesema "Huu sio wakati wa maadhimisho ya hamu" na "Sio wakati wa sherehe za kujipongeza.Kazi bado haikufanyika.Safari haikukamilika.Tunaweza na tunapaswa kuchukuwa hatua zaidi."

Mkusanyiko huo wa Jumamosi ulikuwa ni kitangulizi cha maadhimisho ya kila mwaka ya tarehe 28 mwezi wa Agosti mwaka 1963 ya Washington wakati muhimu katika historia ya Marekani ambao ulianzisha wazo la kuwa na maandamano makubwa kabisa bila ya matumizi ya nguvu na ambayo yalisaidia kuanzishwa kwa Sheria ya Haki za Kiraia hapo mwaka 1964.

Hapo Jumamosi Eric Holder mwanasheria mkuu wa kwanza Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika aliwashukuru wale walioandamana nusu karne iliopita.Amesema asingelikuwepo katika kazi hiyo na wala Obama asingelikuwa rais bila ya watu hao.Holder amesema watu hao "waliandamana kwa sababu waliamini juu ya uadhimu utakaokuwa nao taifa hili na wamevunjika moyo kwa kutotimizwa kwa ahadi za waasisi hao."

Haki za kupiga kura zatiwa walakin

Martin Luther King wakati wa uhai wake.

Martin Luther King wakati wa uhai wake.

Mbunge John Lewis ambaye ni mtoa hotuba pekee wa maandamano ya mwaka 1963 aliyesalia hai ameandamana Jumamosi kupinga uamuzi wa hivi karibuni wa Mahakama Kuu uliofuta kifungu muhimu cha kupinga ubaguzi cha Sheria ya Haki ya Kupiga Kura ambapo kupitishwa kwake hapo mwaka 1965 kulileta mabadiliko makubwa sana katika mapambano ya Wamarekani weusi ya kuwania usawa.Lewis wa jimbo la Georgia alikuwa kiongozi wa maandamano ya mwaka 1965 ambapo polisi iliwapiga na kuwafyatuliwa gesi waandamanaji waliokuwa wakidai kupatiwa haki ya kupiga kura.

Amesema "Sitokaa kando na kuiachia Mahakama Kuu kutuondolea haki yetu ya kupiga kura.Amesema "Huwezi kukaa pembeni. Huwezi kuketi chini.Inabidi usimame.Useme,ukemee na uiingie barabarani."

Hoja ya Mahakama Kuu ni kwamba kifungu hicho ambacho kilikuwa kikitaka majimbo yenye historia ya ubaguzi katika upigaji kura kupata idhini ya serikali kuu kabla ya kufanya mabadiliko ya utaratibu wa kupiga kura kilitegemea data za miaka 40 ambazo hazionyeshi kupigwa hatua kwa masuala ya kupinga ubaguzi.

Uamuzi huo ulisababisha kupitishwa kwa sheria na kanuni kadhaa zenye vikwazo vya kupiga kura katika majimbo mbali mbali.

Marekani mpya

"Tunaamini kuwepo kwa Marekani mpya.Wakati umefika wa kundamandana kwa ajili ya Marekani mpya." hiyo ilikuwa ni kauli ya kiongozi wa kupigania haki za kiraia Al Sharpton wakati akizungumza na umati uliojitokeza Jumamosi.

Rais Barack Obama wa Marekani.

Rais Barack Obama wa Marekani.

Amesema King alikiona kile atakachoweza kufanya Obama miaka 50 iliopita na kwamba dunia ina watu wenye ndoto ambao hubadili uhalisia kutokana na ndoto zao hizo. Kwa hiyo ametaka ndoto hizo wapewe tena vijana wao.

Wanaharakati wengine waligusia juu kuendelea kuwepo kwa ukosefu wa ajira miongoni mwa Wamarekani weusi ambapo kiwango hicho ni maradufu ya kile cha wazungu na kupigwa risasi na kuuwawa kwa kijana mweusi Trayvon Martin huko Florida ambapo mmuaji wake mlinzi wa kujitolea mitaani George Zimmerman aliachiwa huru na baraza la mahakama kwa hoja kwamba alichukuwa hatua hiyo kwa ajili ya kujihami.

Itakumbukwa Martin Luther King Jr alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel hapo mwaka 1964 na aliuwawa hapo tarehe 4 akiwa na umri wa miaka 39.

Katika siku yenyewe hasa ya maadhimisho hayo hapo Jumatano (28.08.2013) Rais Barack Obama rais wa kwanza mweusi wa Marekani atazungumza kwenye ngazi za Kituo cha Kumbukumbu cha Lincoln mahala ambapo King alisimama wakati akitoa hotoba yake ya kusisimuwa miaka 50 iliopita.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP

Mhariri : Caro Robi

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com