Nchi za SADC zaazimia kuwa na Satelaiti ya pamoja | Matukio ya Afrika | DW | 16.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Nchi za SADC zaazimia kuwa na Satelaiti ya pamoja

Nchi zinazounda jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, zinaazimia kuwa na Satelaiti ya pamoja ya mawasiliano, ambayo itasaidia kuendeleza sekta ya tehama miongoni mwa nchi hizo.

Hatua hiyo ni mojawapo ya masuala yanayoangaziwa na makatibu wakuu wa wizara za tehama kutoka nchi hizo, ambao wanakutana mjini Dar es Salaam, Tanzania.

Majadiliano na makubaliano hayo ni utaratibu wa kawaida kwa SADC katika kuelekea kilele cha mkutano wa mawaziri wanaoshughulikia sekta hizo ambazo ni mhimili mkubwa katika kufikia azma ya maendeleo katika jumuia hiyo iliodumu kwa zaidi ya miongo miwili na nusu.

Sehemu ya dhamira ya jumuia hiyo ni kuhakikisha kuwa na soko la pamoja ifikapo mwaka elfu mbili na hamsini, hivyo kwa kauli moja wanajadili na kukubaliana kuwa wanaulazima wa kuhakikisha wanajiimarisha katika miundombinu ya uchukuzi na mawasiliano ikiwa ni zana muhimu wa kuifikisha jumuia katika lengo hilo la soko la pamoja.

Mapolao Mokoena, mkurugenzi wa miundombinu na huduma katika sekretarieti ya SADC, ameuambia mkutano kuwa kuna ulazima wa kutoa kipaumbele katika kuimarisha miundombinu ya uchukuzi ili kutoa fursa za kibiashara kwa wakaazi ndani ya jumuia hiyo.

Katika upande wa kuimarisha mawasiliano, tayari hoja ya kuwa na satelaiti ya pamoja inapigiwa chapuo na mataifa yote wanachama kwa azma ya kuimarisha mawasiliano kadhalika kupunguza gharama za mawasiliano, pamoja na kujitegemea wenyewe kwa asilimia mia moja, ispokuwa sisitizo likisalia kuwa hawana lengo la kujitenga na dunia kimawasiliano ila ni katika mikakati yake ya kuimarisha mawasiliano.

Waziri mwenye dhamana ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano nchini Tanzania Aisack Kamwelwe, anasema, hilo litaleta ushirikiano usio na shaka, kadhalika kupeana taarifa na kujiweka tayari katika kukabiliana na majanga mbalimbali ya kiasili yanapotokea ndani ya nchi mwananchama.

Mkutano wa ngazi ya mawaziri wa SADC katika sekta ya Tehama, Habari, Uchukuzi na hali ya hewa utafikia tamati Septemba ishirini, ambapo mawaziri wa sekta hizo watapitisha maamuzi yaliokubaliwa na makatibu wakuu pamoja na maafisa mbalimbali wa serikali.

 

DW inapendekeza