1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nawaf al-Ahmed Al Sabah aapishwa kuwa mfalme mpya wa Kuwait

Amina Mjahid
30 Septemba 2020

Mrithi wa Kiti cha ufalme wa Kuwait Nawaf al-Ahmad Al-Sabah ameapishwa Jumatano kama mtawala mpya wa taifa hilo la Ghuba, kufuatia kifo cha kaka yake Amir Sabah al-Ahmad Al-Sabah siku ya Jumanne.

https://p.dw.com/p/3jDfL
Kuweit Kronprinz Nawaf Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah
Picha: Jaber Abdulkhaleg/Anadolu Agency/picture alliance

Baraza la mawaziri la Kuwait lilimteua Nawafa mwenye umri wa miaka 83 kama mfalme mpya muda mfupi baada ya Sabah kufariki siku ya Jumanne nchini Marekani, ambako alikuwa amelazwa, akiwa na umri wa miaka 91.

Mwili wa marehemu Emir umepangiwa kuwasili nchini Kuwait siku ya Jumatano, na msiba utahudhuriwa na ndugu tu kwa sababu ya hatua za usalama wa kiafya, kwa mujibu wa familia ya kifalme.

"Naapa kwa jina la Allah, kuheshimu katiba na sheria za nchi, kulinda uhuru wote, maslahi na mali ya umma na kulinda uhuru na mamlaka ya mipaka ya nchi," alisema mfalme huyo mpya wakati akipishwa na bunge.

Katika hotuba baada ya kula kiapo, Nawaf aliomboleza kifo cha mtangulizi wake, akimuelezea kama ishara ya milele, alieifanyia mengi nchi yake na watu wake.

"Ameacha urithi uliojaa mafanikio kwa ngazi ya kitaifa, ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, alisema. "Taifa letu linakabiliwa na mazingira magumu katika kanda yenye machafuko, na njia pekee ya kuyamaliza haya na kuyavuka ni umoja na juhudi za pamoja," aliongeza.

Kuwait | Neuer Emir | Sheikh Nawaf Al Ahmad Al Sabah
Mfalme mpya wa Kuwait Sheikh Nawaf Al Ahmad Al Sabah, katikati, akisoma kiapo cha kikatiba katika Bunge la Kitaifa la Kuwait, Jumatano, Septemba 30, 2020.Picha: Jaber Abdulkhaleg/AP Photo/picture alliance

Changamoto zinazoikabili Kuwait

Changamoto zinazoikabili Kuwait zinajumlisha kuwa katika kanda tete iliyogubikwa na uhasama kati ya Saudi Arabia na Iran, mzozo wa kidiplomasia wa miaka kadhaa kati ya kundi la mataifa linaloongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Qatar, pamoja na kushuka kwa bei za mafuta duniani, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya Kuwait.

Nawaf aliteuliwa mrithi wa ufalme mwaka 2006, muda mfupi baada ya Sabah kuteuliwa kuongoza. Nawaf, ambaye alizaliwa Juni 25, 1937 katika mji mkuu wa Kuwait, alianza kazi ya siasa akiwa kwenye umri wa miaka 20, alipoteuliwa kuwa gavana wa mkoa wa Hawalli.

Nawaf baadae alishika nyadhifa kadhaa za uwaziri, ukiwemo wa mambo ya ndani, ulinzi na masuala ya kijamii, kabla ya kuteuliwa kuwa mrithi wa kiti cha ufalme. Ana watoto watano kwa mujibu wa tovuti yake.

Chanzo: Mashirika