Narendra Modi, waziri mkuu mpya India | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Narendra Modi, waziri mkuu mpya India

Kiongozi wa upinzani nchini India, Narendra Modi, atakuwa waziri mkuu mpya katika taifa hilo ambalo lina historia ndefu ya demokrasia, akishinda uchaguzi muhimu kuwahi kushuhudiwa katika nchi hiyo kwa miongo mitatu.

Indien Wahlen 2014 BJP Narendra Modi

Waziri mkuu mteule Narendra Modi

Modi na chama chake cha Hindu Nationalist amekiamngusha chama cha Congress ambacho kimekuwa kikidhibiti siasa za nchi hiyo kwa muda mrefu .

Modi, ambaye ni mwanasiasa mzoefu ambaye katika kampeni yake ameahidi kuufufua uchumi wa nchi hiyo, atakuwa na mamlaka makubwa kutawala katika wakati wa mabadiliko makubwa katika jamii ya India. Pia amesema kuwa anataka kuimarisha uhusiano wa kimkakati na Marekani.

Indien Wahlen Gewinner Narendra Modi 16.05.2014

Waziri mkuu mteule Modi

Lakini wakosoaji wanahofu kwamba kuingia madarakani kwa chama chake cha wazalendo cha Wahindu kunaweza kuhatarisha hali ya wasi wasi wa kimadhehebu na Waislamu wa India wapatao milioni 138 ambao ni wachache nchini humo.

Congress yaporomoka

Matokeo yalikuwa ni kipigo kikubwa kwa chama cha Congress, ambacho kinamafungamano makubwa na ukoo wa kisiasa wa Nehru-Gandhi ambacho kimekuwa katikati ya siasa za India kwa muda wa historia ya nchi hiyo ya baada ya uhuru.

Indien Wahlen Feier BJP Sieg 16.05.2014

Wapiga kura wa India wakisherehekea ushindi wa chama cha BJP

Serikali , ikiongozwa na waziri mkuu anayeondoka madarakani Manmohan Singh, imekabiliwa na kashafa za mara kwa mara za rushwa na uchumi mbovu.

Wakati ushindi wake wa kishindo ulipoanza kuonekana wazi kuanzia siku ya Ijumaa, Modi alijitokeza katika kundi la waungaji wake mkono waliokuwa wakishangiria na kujaribu kutoa matamshi ya maridhiano.

"Nimekuwa nikisema kila wakati kuwa kuongoza taifa ni wajibu wetu kuwajumuisha kila mtu pamoja nasi," Modi amesema baada ya uchaguzi mrefu na uliohitaji kazi ngumu. "Nahitaji ridhaa yenu ili tuweze kuiendesha serikali ambayo inabeba kila mtu pamoja."

Ni kiongozi anayeleta mtengano

Pamoja na hayo , Modi anabaki kuwa mtu anayeleta mtengano katika nchi hiyo yenye wakaazi bilioni 1.2, kwa kiasi kikubwa kwa sababu, yeye kama waziri kiongozi wa jimbo la Gujarat, alikuwa mamlakani mwaka 2002 wakati ghasia za kikabila katika jimbo hilo ziliposababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000, wengi wao Waislamu.

Indien Wahlen Feier BJP Sieg 16.05.2014

Waungaji mkono wa chama cha BJP wakisherehekea

Modi alishutumiwa kwa kutofanya vya kutosha kuzuwia ghasia hizo, licha ya kuwa anakana kosa lolote na hajafunguliwa mashtaka kwa uhalifu. Alikataliwa visa kuingia nchini Marekani mwaka 2005 kwa madai ya kuhusika katika ghasia hizo, licha ya kuwa kama waziri mkuu atakuwa na hakika ya kupata visa kuingia nchini Marekani.

Obama ampongeza Modi

Jana Ijumaa(16.05.2014) rais Barack Obama wa Mareakani amempigia simu Modi na kumpongeza kwa ushindi na kumwalika "kutembelea Washington katika muda ambao utakubalika na pande zote ili kuimarisha uhusiano wa mataifa yetu," Ikulu ya Marekani imesema katika taarifa.

Indien Wahlen Narendra Modi in Gandhinagar

Waziri mkuu mpya wa India Narendra Modi

Utawala wa Marekani ulikuwa unaangalia kunyanyuka kwa Modi kwa karibu, na mwezi Februari, kwa mara ya kwanza katika muda wa uongozi wa karne moja kama afisa wa ngazi ya juu wa jimbo la Gujarat, balozi wa Marekani alikutana nae.

Nchini India , suala sasa ni iwapo Modi anaweza kweli kuwa kiongozi anayetenganisha dini na serikali katika nchi hiyo ambayo ina waumini wa imani nyingi. Chama cha Congress kilijaribu kuibua hali ya ghasia za mwaka 2002, katika kampeni, lakini kasi ya Modi na kutoangalia sana udhaifu wa uchumi, umemfikisha katika ushindi.

Mwandishi: Sekione Kitojo /ape

Mhariri: Sudi Mnette

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com