Namibia na Zambia zatinga robo fainali CHAN | Michezo | DW | 19.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Namibia na Zambia zatinga robo fainali CHAN

Zambia na Namibia zimefikia  hatua ya robo  fainali  ya  mashindano  ya ubingwa wa mataifa barani  Afrika kwa wachezaji wa ligi za  ndani, CHAN baada ya kupata ushindi katika michezo yao mjini Marrakech.

Augustine Mulenga , ambaye  alifikisha  umri  wa  miaka 28  kabla  ya  mchezo huo, alifunga bao  katika  kila  kipindi wakati Zambia ikipata ushindi  wa  mabao 2-0 dhidi  ya  Cote d'Ivoire katika  uwanja  wa  Grand Stade de Marrakech wenye uwezo  wa  kuingia mashabiki 45,000.

Baadaye , Namibia  ilishinda  pambano  lake  la  pili  mfululizo  kwa  bao  1-0 wakati Halleluya Nekundi  alipofunga katika  dakika  za  majeruhi dhidi  ya Uganda  iliyokuwa  na wachezaji 10 uwanjani.

Namibia  na  Zambia  zinakutana  siku  ya  Jumatatu mjini  Casablanca  kuamua  nani anashika  nafasi  ya  kwanza  na  ya  pili  wakati  kutakuwa  na  pambano  la  kulinda  hadhi wakati Cote d'Ivoire  itakapokumbana  na  Uganda  mjini  Marrakech.

Ni mara  ya  tatu  katika  majaribio  matatu  ambapo Zambia  imefikia  awamu  ya  mtoano katika  mashindano  hayo  yanayofanyika  kila  baada  ya  miaka  miwili kwa  wachezaji wanaocheza  ligi  za  ndani  barani  Afrika.

Namibia inashiriki  mashindano  hayo  kwa  mara  ya  kwanza  baada  ya  kuishinda Zimbabwe kwa  mshangao  mkubwa  katika  michezo  ya  mchujo, na  matayarisho  yake yalizuiwa  na  kufutwa kwa  ligi ya  ndani  ya  mwaka  2016/17.

Uganda , ikicheza  mchezo  wake  wa  pili chini  ya  kocha  wao  mpya  Mfaransa  Sebastian Desabre , ilimiliki  kandanda  hadi  pale mlinzi  wake Timothy Awany alipotolewa  nje  kwa kadi  nyekundi katika  dakika  za  mwisho  za  mchezo  huo.

Namibia  ilitumia  fursa  hiyo dakika  mbili  katika  dakika  za  nyongeza  wakati Nekundi alipofanikiwa  kuutumbukiza  mpira  wavuni mpira  ukimpita  mlinda  mlango Isima Watega kwa  shuti  la  karibu.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe