1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani nchini Kongo bado wavutana juu ya msemaji wake

Jean Noël Ba-Mweze
27 Machi 2024

Miezi miwili baada ya kuapishwa Rais Félix Tshisekedi kwa muhula wa pili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wapinzani bado wamegawika kuhusu wadhifa wa msemaji wa upinzani.

https://p.dw.com/p/4eBDv
Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo | Rais Felix Tshisekedi
Rais Felix Tshisekedi aliyeshinda awamu nyingine ya urais aliuagiza upinzani Picha: AFP

Wakati akiapishwa mwezi Januari, Rais Felix Tshisekedi aliitaka kambi ya upinzani kuteua msemaji. Baadhi ya wapinzani wameeleza kuwa wadhifa huo siyo zawadi kutoka kwa rais bali ni haki, huku wengine wakiendelea kudai uchaguzi wa wazi kufanyika wakisema hawawezi kukubali wadhifa huo katika hali ya sasa.

Ensemble pour la République, chama cha Moïse Katumbi ambacho kilishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa Disemba iliyopita kimekumbusha kuwa nafasi ya msemaji wa upinzani ni haki ya kikatiba.

Soma pia: Serikali ya DR Kongo yaondoa uwezekano wa kurudiwa kwa uchaguzi

"Unajua kwamba hadi sasa bado hatujawa na Seneti na ajenda ya bunge bado haijapanga maswali kama na hayo. Kwa hiyo hatuwezi kulaumu wapinzani. Tunakusudia kutumia haki zetu zote za kikatiba ili kutetea demokrasia yetu iliyo hatarini,” amesema msemaji wa Ensemble pour la République, Hervé Diakese.

Aliyekuwa mgombea kiti cha urais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Moise Katumbi
Aliyekuwa mgombea wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Moise Katumbi katika mkutano wa kutambulisha muungano wa upinzani wa Lamuka, Machi 23, 2019Picha: Nicolas Maeterlinck/picture alliance

Nafasi ya msemaji wa upinzani inatambulika kikatiba

Lakini huo sio msimamo wa muungano wa Lamuka unaohofia mkakati wa Rais Tshisekedi kuendelea kuwanunua baadhi ya wapinzani ili kuhalalisha uchaguzi ambao haujawahi kukubaliwa. Wadhifa wa msemaji wa upinzani utakuwa na maana tu baada ya uchaguzi kutokana na mazungumzo ya wazi. Ndivyo alivyosisitiza Prince Epenge, mmoja wa wasemaji wa Lamuka.

Christian Moleka akiwa mratibu wa muungano wataalam wa maswala ya  kisiasa hapa Kongo Dypol, anaamini kuwa mgawanyiko wa upinzani ndio unasababisha mchakato huo wa uteuzi kuwa mgumu. 

"FCC ambayo haikushiriki uchaguzi na haina nia ya kuchukuwa nafasi hiyo, pia Lamuka iliyosusia uchaguzi wa bunge na haina uwakilishi bungeni haitakubali kuona wadhifa huo unachukuliwa na Moise Katumbi. Yaani upinzani unao vichwa vitatu."

Nafasi ya msemaji wa upinzani imetolewa na katiba ya mwaka 2006. Lakini hata serikali zilizopita, wapinzani hawakuwahi kukubaliana kuhusu hilo.

Soma pia: Upinzani DRC wadai Tshisekedi anaandaa ushindi wa uchaguzi