Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Gambia aipa kisogo nchi yake | Matukio ya Afrika | DW | 03.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Gambia aipa kisogo nchi yake

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Gambia, Alieu Momar Njai amekimbia ili kuyanusuru maisha yake katika wakati ambapo hali inatisha katika nchi hiyo ndogo ya Afrika Magharibi. Vituo viwili vyengine vya radio vimefungwa.

Alieu Momar Njai ndie aliyemtangaza Adama Barrow kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa decemba mosi iliyopita, lakini rais Yahya Jammeh amekataa kung'atuka na badala yake kutuma madai mahakamani kwa hoja za udanganyifu. Mpwa wa Alieu Momar Njai, Modou Njai ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba mjombaake amekimbia kwasababu ya vitisho dhidi ya usalama wake.

"Hakutaka kuondoka....lakini amelazimishwa na familia" amesema Modou Njai.

Kabla ya hapo vikosi vya usalama viliizingira ofisi ya tume ya uchaguzi na kuwakatalia ruhusa ya kuingia ofisi watumishi wa ofisi hiyo kwa wiki kadhaa. Hata hivyo wanajeshi hao wameshalihama eneo hilo hivi sasa.

 

Wagambia washerehekea ushindi wa upande wa upinzani

Wagambia washerehekea ushindi wa upande wa upinzani

Kufungwa Radio za kibinafsi ndio mwanzo wa kuandamwa vyombo vya habari

Shirika linalopigania uhuru wa vyombo vya habari nchini Gambia limesema kwamba idara ya upelelezi imekifunga kituo cha matangazo ya Radio Afri Radio, kituo cha tatu cha kibinafsi kufungwa bila ya sababu yoyote katika kipindi cha siku tatu zilizopita. Shirika hilo linalopigania uhuru wa vyombo vya habari nchini Gambia limeelezea wasi wasi wake uamuzi huo wa kufungwa vituo vya matangazo ya kibinafsi isije ikawa mwanzo wa kuandamwa vyombo huru vya habari katika wakati ambapo mzozo wa kisiasa unaonyesha kuikaba nchi hiyo.

Mshindi wa muungano wa upande wa upinzani Adama Barrow amesema atatwaa madaraka january 19 inayokuja kama ilivyotajwa na katiba, licha ya malalamiko Jammeh aliyoyatuma mahakamani. Upande wa upinzani umemuonya pia rais huyo aliyeitawala Gambia kwa zaidi ya miongo miwili, ataangaliwa kuwa ni sawa na kiongozi aliyeasi pindi akitwaa silaha na kukataa kung'atuka baadae mwezi huu.

Rais mteule wa Gambia Adama Barrow

Rais mteule wa Gambia Adama Barrow

Jumuia ya ECOWAS inasema itatuma wanajeshi Gambia

Msemaji wa muungano wa upande wa upinzani Halifa Sallah amesema Jammeh ataangaliwa kuwa  ni raia wa kawaida kuanzia Januari 19 na hatokuwa na jukumu lolote la kikatiba kuliongoza jeshi la nchi hiyo.

"Rais yeyote ambae mhula wake unamalizika na ambae anaamua kubeba silaha dhidi ya rais mteule ambae mhula wake ndio kwanza unaanza kwa mujibu wa sheria, anabidi aangaliwe na jumuia ya kimataifa kuwa ni kiongozi  aliyeasi.

Mwenyekiti wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi wa nchi za Afrika Magharibi ECOWAS amesema viongozi wa jumuia hiyo watatuma wanajeshi nchini Gambia pindi Jammeh akikataa kutoka madarakani.

Halifa Sallah ameongeza kusema,Barrow,ECOWAS,Umoja wa Afrika na Umoja wa mataifa wametathmini kikamilifu hatua zao na kuongeza Jammeh anapaswa kuiga mfano huo ili kutoitia hatarini amani na usalama wa nchi hiyo.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/dpa/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga