Mwanawasa azikwa Lusaka | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 03.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mwanawasa azikwa Lusaka

Nchini Zambia mazishi ya marehemu Rais Levy Mwanawasa yanafanyika hii leo mjini Lusaka. Marehemu rais Mwanawasa alifariki majuma mawili yaliyopita mjini Paris nchini Ufaransa akiwa na umri wa miaka 59.

Marehemu Rais Levy Mwanawasa wa Zambia

Marehemu Rais Levy Mwanawasa wa Zambia


Nchini Zambia mazishi ya marehemu Rais Levy Mwanawasa yanafanyika hii leo mjini Lusaka.


Marehemu rais Mwanawasa alifariki majuma mawili yaliyopita mjini Paris nchini Ufaransa akiwa na umri wa miaka 59.


Kiongozi huyo aliugua kiharusi mwezi Juni alipokuwa akihudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyika Sharm el Sheikh nchini Misri.


Mazishi hayo yalianza asubuhi kwenye majengo ya bunge la nchi hiyo mjini Lusaka.


Maelfu ya waombolezaji walihudhuria shughuli hiyo ili kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi wao.Televisheni na radio ya kitaifa ilitangaza shughuli hiyo moja kwa moja iliyoanza kwa ibada maalum.


Takriban marais 14 wa mataifa ya Afrika wanahudhuria mazishi hayo.


Marehemu rais Mwanawasa alipata umaarufu mkubwa kwasababu ya vita dhidi ya ufisadi na rushwa vilevile msimamo wake mkali dhidi ya uongozi wa Rais Mugabe katika nchi jirani ya Zimbabwe.


Rais Mugabe ni miongoni wa viongozi waliokuwa wa kwanza kuwasili mjini Lusaka akijumuika na Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki aliye kiongozi wa sasa wa Jumuiya ya Maendeleo ya SADC pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania.


Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa za radio ya Zambia Rais Mugabe alimsifu marehemu Mwanawasa kwa ushupavu na uwazi katika utendaji wake wa kazi.


Itakumbukwa kuwa marehemu rais Mwanawasa aliukosoa vikali uongozi wa Rais Mugabe na kuifananisha hali nchini humo kama meli aina ya Titanic iliyokuwa ikienda mrama.


Wengine waliyoudhuria mazishi hayo ni pamoja na marais wa Botswana Ian Khama,Bingu wa Mutharika wa Malawi,Pakalitha Mosisili wa Lesotho, na Paul Kagame wa Rwanda.


Pia Mwakilishi wa malkia Elizabeth wa Uingereza,Mwanamfalme mtawala wa jimbo la Gloucester pamoja na Waziri wa Uingereza anayehusika na masuala ya Afrika,Asia na Umoja wa Mataifa Malloch Brown anaudhuria mazishi hayo.


Aidha wawakilishi wa nchi za Ujerumani na Uchina nao pia wanahudhuria.


Makamu wa rais wa Zambia anayekaimu wadhifa wa rais kwa sasa Rupiah Banda anatarajiwa kutoa wasifu wa marehemu Mwanawasa katika hotuba maalum.


Rais Mwanawasa alikuwa kiongozi wa tatu tangu Zambia kujipatia uhuru wake na ni wa kwanza kufariki.


Mazishi hayo yatafuatiwa na ibada maalum kanisani kama ilivyoeleza ratiba rasmi ya shughuli hiyo.


Marehemu Rais Mwanawasa alifariki tarehe 19 mwezi Agosti katika hospitali ya kijeshi ya Ufaransa ya Percy baada ya kuugua kiharusi.Akiwa na umri wa miaka 59 na hii leo kiongozi huyo angetimiza miaka 60.


Rais Mwanawasa aliyekuwa mwanasheria atazikwa katika bustani la Embassy iliyoko karibu na ofisi za rais.Ameacha mjane Maureen Mwanawasa na watoto sita.

Kwa upande mwingine Uingereza imetoa wito kwa uongozi wa Zambia kuhakikisha kuwa uchaguzi wa rais unafanyika katika mazingira ya huru na haki ili kuepuka utata ulitokea katika nchi jirani ya Zimbabwe.Uchaguzi mkuu huo wa rais umepangwa kufanyika mwezi Novemba.Kauli hizo zimetolewa na Waziri wa Uingereza anayehusika na masuala ya Afrika,Asia na Umoja wa Mataifa Malloch Brown punde baada ya kuwasili mjini Lusaka ili kuhudhuria maziko hayo.Bwana Brown alikutana na Waziri wa Fedha wa Zambia Ng'andu Magande na kuahidi msaada wa kufadhili uchaguzi huo wa Novemba.

Kulingana na katiba ya Zambia uchaguzi wa rais sharti ufanyike katika kipindi cha siku 90 baada ya kifo cha rais aliye madarakani.


Wakati huohuo kwenye nchi jirani ya Zimbabwe mkwamo wa kisiasa unaogubika uongozi bado haujatafutiwa ufumbuzi.Chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change,MDC kimetangaza kuwa mazungumzo hayo kati yao na chama cha ZANU-PF cha rais Robert Mugabe yamekwama.

Chama hicho kinatoa wito kwa rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki aliye msuluhishi mkuu kwenye mazungumzo hayo kuingilia kati.Hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa chama cha MDC Nelson Chamisa.Hii ni mara ya kwanza kwa chama hicho kukiri kuwa mazungumzo hayo yamegonga mwamba.Majadiliano hayo yalianza mwezi Julai na suala tete linalozua migongano ni ugavi wa madaraka katika hatua ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.DW inapendekeza

 • Tarehe 03.09.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FAhd
 • Tarehe 03.09.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FAhd
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com