1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Mwanamuziki mwengine afariki kizuizini Rwanda

Daniel Gakuba
2 Septemba 2021

Mwanamuziki maarufu wa miondoko ya kufokafoka nchini Rwanda, Joshua Tuyishime maarufu kama Jay Polly, amekufa akiwa korokoroni alfajiri ya Alhamis (Septemba 2).

https://p.dw.com/p/3zpUN
Ruanda Opposition Musiker  Kizito Mihigo
Picha: STEPHANIE AGLIETTI/AFP/Getty Images

Jay Polly ni mwanamuziki wa pili kupoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha nchini Rwanda katika muda usiotimia miaka miwili, baada ya Kizito Mihigo ambaye polisi ilisema alijinyonga akiwa rumande.

Mkuu wa hospitali ya Muhima mjini Kigali, Pascal Nkubito, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Jay Polly, aliyekuwa na umri wa miaka 33, alifikishwa katika hospitali hiyo majira ya saa tisa usiku akiwa katika hali mahtuti, na kukata roho muda mfupi baadaye.

Mwanamuziki huyo alikamatwa mwezi Aprili mwaka huu kwa tuhuma za kuandaa sherehe nyumbani kwake, akikiuka masharti ya kujikinga na virusi vya corona, na baadaye alishutumiwa kukutwa na bangi na vyeti vya kughushi vya vipimo vya ugonjwa wa Covid-19, shutuma ambazo alizikanusha.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Rwanda wameomboleza kifo cha Jay Polly kwa hisia mseto.