1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wa kisiasa wapamba moto Armenia

25 Februari 2021

Waziri mkuu Pashnyan ameingia mitaani kujiunga na maandamano ya wafuasi wake mjini Yerevan wakati Jeshi likimtia kishindo ajiuzulu kufuatia maandamano ya miezi kadhaa tangu nchi iliposhindwa katika vita na Azerbaijan

https://p.dw.com/p/3pvOs
Armenien Jerevan | Premierminister Nikol Pashinyan
Picha: Stepan Poghosyan/AP/picture alliance

Hali ya wasiwasi inaripotiwa huko Armenia ambapo maandamano yameshuhudiwa kwa siku kadhaa. Waziri mkuu Nikol Pashinyan leo aliingia mitaani na wafuasi wake katika mji mkuu Yerevan wakati mkuu wa majeshi akimtaka ajiuzulu na serikali yake.

Kinachoshuhudiwa nchini Armenia kwa sasa ni hali kuzidi kuwa tete kufuatia maandamano ya kila upande. Upinzani na wafuasi wake wanaandamana wakimtaka waziri mkuu Nikol Pashinyan ajiuzulu na waziri mkuu huyo nae na wafuasi wake wameingia mitaani kuonesha mamlaka yake.

Chama kikubwa kabisa cha upinzani nchini humo kwa miezi sasa kilianzisha miito ya kumtaka waziri mkuu huyo ajiuzulu na kilimpa muda wa hadi leo alhamisi awe ameshaondoka madarakani ili aepushe kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Taarifa ya chama hicho  imeeleza kwamba wanamtaka waziri mkuu asiipeleke nchi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe bali aiepushe na umwagaji damu.Chama hicho kinachojiita cha kupigania maendeleo ya Armenia-PA kimesema Pashinyan ana fursa ya mwisho ya kuepusha mkwamo katika nchi hiyo. Lakini leo waziri mkuu huyo nae ameamua kuingia mitaani kuandamana na wafuasi wake baada ya kulituhumu jeshi kwamba linapanga kumpindua madarakani. Amewaambia wafuasi wake, hali ni tete lakini wanapaswa kukubaliana kwamba hawatoingia kwenye machafuko.

Armenien Jerevan | Premierminister Nikol Pashinyan und Unterstützer
Picha: Stepan Poghosyan/Photolure/REUTERS

Urusi imeitaka Armenia kuyatatua matatizo yake mwenyewe wakati Uturuki ikisema inapinga jaribio la mapinduzi nchini Armenia.

Imetajwa kwamba leo Alhamisi mapambano yamezuka kati ya wafuasi wa waziri mkuu huyo na wale wa upinzani katika mji mkuu Yerevan. Waziri mkuu Pashinyan amesema mvutano huu wa kisiasa uliofuatia miezi kadhaa ya maandamano dhidi ya serikali yake unaweza kudhibitiwa. Anawatuhumu maafisa wa juu jeshini kwamba wanajaribu kufanya mapinduzi kuiondowa serikali yake baada ya kumtaka ajiuzulu. Cha kufahamu ni kwamba maandamano ya miezi chungunzima ya kumpinga Pashinyan na serikali yake yalifuatia kitendo cha kushindwa nchi hiyo katika vita yake na Azerbaijan ya kuliwania jimbo la Nagorno Karabakh.

Armenien I Demo für den Rücktritt von Premierminister Pashinyan in Eriwan
Picha: Vahram Baghdasaryan/Photolure/TASS/dpa/picture alliance

Kilichotokea ni kwamba,punde baada ya waziri mkuu Pashinyan kusaini makubaliano ya amani na Azerbaijan,yaliyosimamiwa na Urusi na Uturuki, Novemba 10 mwaka jana na Azerbaijan, ikakabidhiwa sehemu kubwa ya ardhi ya jimbo hilo la Nagorno Karabakh na maeneo mengine yaliyokuwa yakidhibitiwa na wanajeshi wa Armenia kwa zaidi ya robo karne,maandamano hayo yakazuka. Sasa maandamano hayo yameongezeka kasi wiki hii na hali hii iliyojitokeza ya mvutano na makamanda wake wa juu wa jeshi kunaonesha kuidhoofisha kabisa nafasi ya Pashinyan.

Na kilichoibua mvutano huu na jeshi ni hatua ya waziri mkuu huyo kumtimua naibu mkuu wa majeshi Tiran Khachatryan baada ya kumkosoa na kundi la majenerali kadhaa waandamazi wa jeshi la ulinzi.Hatua hii ndiyo iliyomfanya mkuu wa majeshi  kumtaka Pashinyan ajiuzulu, lakini waziri mkuu huyo akamtimua pia mkuu huyo wa majeshi Onik Gasparyan. Pashinyan amelitaja tamko hilo la mkuu wa majeshi kuwa jaribio la mapinduzi. Na pia kwa upande mwingine waziri mkuu  amekanusha tetesi zinazoenea zinazodai  anajiandaa kuikimbia nchi.

Chanzo: Mashirika

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW