1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Muswada wa maridhiano waridhiwa Senegal

Amina Mjahid
29 Februari 2024

Serikali ya rais wa Senegal Macky Sall, imeuridhia muswada wa sheria ambao utatoa msamaha kwa waandamanaji wa kisiasa waliokamatwa kati ya mwaka 2021 na 2024. Muswada huo unalenga kuleta maridhiano ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/4d0wk
Senegal I  Macky Sall
Rais wa Senegal Macky SallPicha: Amr Alfiky/File Photo/REUTERS

Muswada huo ambao kwanza ni lazima upitishwe bungeni, unaweza kutoa nafasi ya kuachiwa kwa mamia ya watu akiwemo kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo Ousmane Sonko, waliozuiliwa wakati wa maandamano ya kuipinga serikali yalioanza mwaka 2021.

Kulingana na ripoti ya Baraza la mawaziri, iliyotolewa baada ya mkutano uliofanyika jana Jumatano ulioongozwa na rais Sall, muswada huo ulipendekezwa na rais mwenyewe kwa lengo la kuleta maridhiano ya kisiasa, maelewano na kusonga mbele.

Senegal: Rais Sall asema ataachia madaraka muda wake ukifika

Muswada huo ulikuwa sehemu ya majibu ya Sall ya mgogoro mkubwa wa kisiasa aliyouanzisha, baada ya kuahirisha uchaguzi uliokuwa ufanyike tarehe 25 mwezi Februari. Kuahirishwa huko kulifanyika saa chache kabla ya kampeni za uchaguzi kuanza rasmi.

Sall,  aliyeingia madarakani mwaka 2012 alisema alichukua uamuzi huo kufuatia mivutano iliyokuwepo, iliyotokana na kupigwa marufuku baadhi ya wagombea katika uchaguzi huo na hofu ya kurejea vurugu zilizoonekana mwaka 2021 na 2023.

Hata hivyo matumaini ya Sall kutangaza hivi karibuni tarehe mpya ya uchaguzi katika mkutano wake wa siku mbili yalififia. Ofisi ya rais ilitoa taarifa ikisema Sall, ataliomba Baraza la Katiba kutoa maoni juu ya mapendekezo yaliyofikiwa katika mkutano huo, ikiwa ni pamoja na kumuacha rais Sall aendelee kubakia madarakani hata baada ya muhula wake kukamililka Aprili 2.

Upinzani wasema mkutano wa Sall umemsaidia kutekeleza alichokitaka.

Senegal
Upinzani Senegal haukubaliani na pendekezo la Sall kuendelea kubakia madarakani baada ya muhula wake kukamilika Aprili 2 Picha: John Wessels/AFP

Mmoja ya wagombea wa upinzani Bassirou Diomaye Faye, alipinga vikali pendekezo hilo, hii ikiwa ni kwa mujibu wa msemaji wake Amadou Ba.

Mkutano huo uliofanyika katika mji wa Diamniadio kilomita 30 kutoka mji mkuu wa Dakar ulihudhuriwa na viongozi wa kisiasa, wawakilishi wa mashirika ya kiraia pamoja na viongozi wa kidini na miongoni mwa yaliyopendekezwa ni hilo la Sall kuendelea kubakia madarani hata baada ya muhula wake kukamilika, uchaguzi kufanyika mwezi Juni ama julai na orodha ya wagombea wa urais inayopaswa kuangaliwa upya.

Rais Macky Sall apendekeza mswada wa msamaha Senegal

Orodha iliyokuwepo zamani ya wagombea 19,  haikuwa na baadhi ya wagombea wa upinzani waliopigwa marufuku ya kugombea. Wagombea 17 kati ya hao 19 walioidhinishwa kugombea katika uchaguzi ulioahirishwa waliususia mkutano wa Maridhiano wa Sall. makundi mengine ya mashirika ya kiraia pia hawakuhudhuria.

Thierno Alassane Sall, mmoja ya wagombea alisema waliohudhuria wamemsaidia Sall kutekeleza kile alichokitaka.

Senegal,  taifa lililo Magharibi mwa Afrika, lililokuwa na sifa ya dola lililo na uthabiti na lililoimarisha demkokrasia, linapitia kipindi kigumu cha kisiasa baada ya Sall kuuahirisha uchaguzi mkuu.

Tangazo la kuahirishwa uchaguzi Senegal lazusha kizaazaa

afp/reuters