Musharraf aruhusiwa kua rais | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Musharraf aruhusiwa kua rais

Korti kuu ya Pakistan yapinga madai ya upinzani

Pervez Musharraf ahutubia taifa

Pervez Musharraf ahutubia taifa

Mahakama kuu nchini Pakistan imelikataa dai la mwisho dhidi ya kuchaguliwa upya Musharraf kama rais October sita iliyopita. Uamuzi huo unamfungulia njia ya kusalia kwa mara ya pili madarakani na kuachana kama alivyoahidi na wadhifa wake kama mkuu wa vikosi vya wanajeshi wa Pakistan .

“Dai la mwisho limekataliwa” amesema msemaji wa korti kuu ya Pakistan -Arshad Munir .

Jenerali Pervez Musharaf,aliyeingia madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi miaka minane iliyopita,alichaguliwa upya na kwa wingi mkubwa,kwa kura ya mabaraza ya taifa na ya kimkoa October sita iliyopita.

Lakini upande wa upinzani ulibisha uasmuzi huo,wakihoji katiba inamlazimisha aache kwanza wadhifa wake kama mkuu wa vikosi vya wanajeshi kabla ya kuchaguliwa kua rais.Wapinzani wake walishuku pia kama kuchaguliwa kwake ni halali,wakihoji rais mpya angebidi ateuliwe na bunge jipya baada ya uchaguzi mkuu uliopangwa kuitishwa January nane ijayo.

Mahakama kuu ikaamua kwa hivyo matokeo ya uchaguzi wa rais yasitishwe hadi madai ya upande wa upinzani yatakapochunguzwa.

Wakati huo huo lakini Musharaf akatangaza sheria ya hali ya hatari,November tatu iliyopita .Aliwafukuza kazi majaji wanaompinga na kuwateuwa wengine wanaoelemea zaidi upande wake.

Korti kuu iliyakataa madai matano ya mwanzo jumatatu iliyopita ikiacha hili la mwisho ambalo tokea mwanzo watu walikua wakijua kwamba lisingeweza kubatilisha chochote .

Rais Musharaf aliahidi tangu muda sasa,kutokana na shinikizo la Marekani, atajiuzulu wadhifa wake kama mkuu wa vikosi vya wanajeshi mara tuu atakapotangazwa kua rais.Wadadisi wanaamini Jenerali rais Pervez Musharaf atavua uniform zake za kijeshi na kuvaa suti mwishoni mwa wiki hii.Ameamua pia kuwaachia huru wapinzani elfu tano, waliowekwa katika kifungo cha nyumbani tangu sheria ya hali ya hatari ilipotangazwa November tatu iliyopita.

Hata hivyo rais Musharraf hakubatilisha sheria ya hali ya hatari na Washington inaonyesha kuifumbia macho hali hiyo.

Upande wa upinzani nchini Pakistan umegawanyika linapohusika suala la kususiwa au la,uchaguzi mkuu January nane ijayo.Mcheza Cricket mashuhuri wa Pakistan Imran Khan ametoa mwito uchaguzi huo ususiwe ili kuepukana na kile alichokiita “balaa la kuhalalisha sheria ya hali ya hatari.”

Macho ya walimwengu yanamlenga hivi sasa Benazir Bhutto ambae chama chake cha PPP kinatazamiwa kutamka hii leo kama watasusia au la uchaguzi huo,sawa na muungano wa vyama sita vya kiislam vinavyowakilishwa bungeni.

Wakati huo huo maduka yasiyopungua manane ya video na CD za muzik yameteketezwa akufuatia shambulio la bomu katika mji wa kaskazini magharibi wa Mardan,umbali wa kilomita 60 toka mji mkuu wa jimbo la Punjab-Peshawar.

Nalo jeshi la Pakistan limesema hii leo limewaauwa wanamgambo 35 wa itikadi kali ya dini ya kiislam wanaoungwa mkono na Al Qaida,katika juhudi za kuliteka bonde la Swat,kaskazini magharibi ya Pakistan .

 • Tarehe 22.11.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CQNU
 • Tarehe 22.11.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CQNU

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com