1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mukwege awahimiza Wakongomani kuzuia wizi wa kura

23 Januari 2023

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Dokta Denis Mukwege amewatolea wito wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kujipanga ili kuzuia udanganyifu wowote katika uchaguzi uliopangwa kufanyika baadae mwaka huu nchini humo.

https://p.dw.com/p/4MZpp
DRC | Friedensnobelpreisträger Denis Mukwege in Bukavu
Picha: Ernest Muhero/DW

Mukwege aliyeshinda tuzo hiyo mnamo mwaka 2018, aliyatoa matamshi hayo siku ya Jumapili wakati wa mkutano na vijana zaidi ya 5,000 uliofanyika kwenye mji wa Bukavu katika jimbo la Kivu Kusini.

Aidha, aliwataka vijana hao na Wakongo kwa ujumla kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika mwezi Desemba, 2023 na amewaonya pia kuepuka makosa ya uchaguzi uliopita.

Alipoulizwa iwapo atakuwa mgombea urais mwezi Desemba, Denis Mukwege hakukataa na wala hajakubali rasmi, ila aliwataka raia wa Kongo wenyewe wawe chanzo cha mabadiliko wanayoyataka katika nchi yao.

Dokta Mukwege pia alitumia fursa hiyo kukikosoa kikosi cha kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichoko mashariki ya Kongo akisema kamwe hakuna nchi inayoweza kulinda usalama wa nchi nyingine jirani, na amependekeza mageuzi katika vyombo vya usalama vya Kongo.