Mtiririko wa matukio ndani ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika | Matukio ya Afrika | DW | 23.05.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mtiririko wa matukio ndani ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika

ADDIS ABABA, Jan. 30, 2010 (Xinhua) -- Flags of African Union (AU) members flutter in front of the United Nations Conference Center, the venue of the 14th Ordinary Session of the Assembly of the AU, in Addis Ababa, capital of Ethiopia, Jan. 30, 2010. Preparations were geared up here Saturday, a day ahead of the summit. Xinhua /Landov Keine Weitergabe an Drittverwerter.

Flaggen African Union AU

Umoja wa Afrika, zamani ukiitwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), unaadhimisha miaka 50 tangu kuundwa kwake, ukiwa na hadithi ya mafanikio na mapungufu, lakini ukisalia na dhamira ya kusonga mbele.

Tarehe 25 Mei 1963: Mataifa 30 huru ya Afrika yakutana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kuanzisha Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU). Lengo: umoja wa bara hilo na pia uhuru na mamlaka ya wanachama wake. Mwaka huo huo, OAU inaunda Kamati ya Ukombozi yenye makao makuu yake nchini Tanzania, ambayo inaunga mkono mapambano dhidi ya utawala wa wachache Namibia na Afrika ya Kusini.

1976: Mtawala wa kijeshi wa Uganda, Idi Amin, atangazwa kuwa rais wa maisha. Ukatili wake dhidi ya kiasi cha wahanga 400,000 wapelekea kuvunjwa kwa sera ya OAU ya kutokuingilia mambo ya ndani ya nchi.

Nembo ya Umoja wa Afrika.

Nembo ya Umoja wa Afrika.

1980: OAU yazindua kile kilichoitwa “Lagos Plan of Action” yaani Mpango Kazi wa Lagos” nchini Nigeria. Mpango huo wadhamiria kuongeza ushirikiano wa kikanda na kutandika msingi wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika. Mafanikio yake hayakuweza kuonekana mara moja.

1985: Morocco yajitoa rasmi kwenye OAU ikilalamikia kuruhusiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi (Sahara ya Magharibi) kujiunga na Umoja huo mwaka 1982. Kundi la waasi wa Polisario lilikuwa limejitangazia uhuru wake kutoka Morocco na kuunda jamhuri na kuanzisha serikali wakiwa uhamishoni.

1989: Kamisheni ya Haki za Binaadamu na Watu ya OAU yaundwa rasmi.

Mkutano wa 18 wa Umoja wa katika ukumbi wa jengo jipya la Umoja huo mwaka 2012.

Mkutano wa 18 wa Umoja wa katika ukumbi wa jengo jipya la Umoja huo mwaka 2012.

1991: Mataifa wanachama wa OAU yaanzisha “Jumuiya ya Uchumi ya Afrika” kwa lengo la kuwa na uchumi mmoja wa Afrika kufikia mwaka 2025 kwa kuigiza mfano wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya ambayo ilikuwa muasisi wa Umoja wa Ulaya.

1994: Baada ya kumalizika kwa utawala wa kibaguzi, Afrika ya Kusini yajiunga na Umoja.

1999: Katika mkutano maalum wa kilele mjini Sirte (Libya, OAU inajadili uundwaji wa Umoja wa Afrika wenye malengo mamoja ya kisiasa kama vile Umoja wa Ulaya. Wazo hilo lilitokana na Muammar Gaddafi aliyekuwa kiongozi wa Libya kwa wakati huo.


Jengo la Makao Makuu Mapya la Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Jengo la Makao Makuu Mapya la Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia.

2000: Kuelekea enzi mpya: Katika mkutano mjini Lome, Togo, viongozi wakuu wa mataifa ya OAU wanasaini makubaliano ya kuasisi Umoja wa Afrika (AU). Kwa mujibu wa Kifungo Namba 30 cha mkataba huo, serikali zilizoingia madarakani kwa njia isiyo ya kidemokrasia zitengwe na Umoja huo.

2001: Sasa OAU inaitwa rasmi Umoja wa Afrika na ina wanachama 53. Morocco haijiungi na AU kwa sababu ya mgogoro unaoendelea kwenye Sahara ya Magharibi. OAU na AU zinaendelea kuwapo kwa pamoja katika kipindi cha mpito cha miaka miwili. Vyombo vikuu vya Umoja wa Afrika ni mkutano mkuu wa kilele wa viongozi wa mataifa wanachama na uwenyekiti unaozunguka kila mwaka. “Jumuiya ya Uchumi ya Afrika” inakuwa sehemu ya AU.

2002: Baraza lililoasisi AU linakutana Durban (Afrika ya Kusini). Makao makuu ya umoja huo yabakia Addis Ababa (Ethiopia).

Viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika katika mkutano wa kilele wa mwaka 2011.

Viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika katika mkutano wa kilele wa mwaka 2011.

2003: AU yaanzisha Baraza la Usalama kama lile la Umoja wa Mataifa. Linaundwa na wawakilishi 15 wa kuchaguliwa kutoka mataifa wanachama na linaweza kufanya operesheni za kuingilia kati kijeshi na za kulinda amani barani Afrika dhidi ya matakwa ya taifa mwanachama.

2004: AU yafungua “Bunge la Afrika” mjini Midrand (Afrika ya Kusini). Sasa lina wajumbe 265 waliochaguliwa kutoka mataifa wanachama. Lengo la bunge hilo ni kutekeleza siasa na malengo ya AU na kukuza demokrasia na maendeleo ya uchumi. Bunge hilo ni chombo cha ushauri tu na halina nguvu ya kutunga sheria. Mwaka huo huo, Umoja wa Afrika watuma wanajeshi katika mkoa wenye migogoro wa Darfur kupitia kikosi chake cha AMIS (Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Sudan) na UNAMID (Kikosi cha Umoja wa Mataifa jimboni Darfur).

2005: Somaliland ambayo ni sehemu ya kaskazini mwa Somalia, yawasilisha ombi la uwanachama kwa AU. Mkoa huo hautambuliwi kimataifa kama dola na hakuna dalili kwamba kwa siku za karibuni Somaliland itaweza kujiunga na AU.

Taifa la Kaskazini Magharibi ya Afrika, Mali, linavuliwa uwanachama wake kwa muda kutokana na mapinduzi ya kijeshi. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 larudishwa tena lakini laondolewa tena kwa muda baada ya mapinduzi mengine ya kijeshi ya mwaka 2008.

Viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika katika mkutano wa kilele wa mwaka 2011.

Viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika katika mkutano wa kilele wa mwaka 2011.

2006: Kutokana na Azimio 1725, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaruhusu kupelekwa kwa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM). Kufikia mwishoni mwaka 2012, idadi ya wanajesji wanaoilinda serikali ya Somalia yaongezeka hadi 17,000.

2009: Kutokana na kanuni yake ya uwenyekiti unaozunguka, kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi anakuwa rais wa AU. Wakati wa uwenyekiti wake, anapigania kwa nguvu dira yake ya “United States of Africa”. Afrika ya Kusini ni miongoni mwa mataifa yanayopingana vikali na wazo hilo.

2012: Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika ya Kusini, Nkosazana Dlamini-Zuma, awa mwanamke wa kwanza kwenye historia ya umoja huo kuchaguliwa kuwa mkuu wa Kamisheni ya AU. Ni nafasi ya juu kabisa kwenye umoja huo.

2013: AU ina wanachama 54, yaani nchi zote za Kiafrika isipokuwa Morocco. Sahara ya Magharibi ni mwanachama kamili wa AU lakini si mwanachama wa Umoja wa Mataifa wala haitambuliwi rasmi kuwa dola. Hata mengi ya mataifa ya AU hayaitambui Sahara ya Magharibi kama dola. Uwanachama wa Jamhuri ya Afrika ya Kati umesitishwa tangu kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi mwezi Machi 2013. Guinea Bissau na Madagascar pia zimesitishwa uwanachama.

Mwandishi: Ludger Schadomsky
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yusuf

1963