Mpango wa kuleta amani Mali, waibua matumaini | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mpango wa kuleta amani Mali, waibua matumaini

Waasi wa kabila la Tuareg wanaotaka kujitenga nchini Mali, hatimaye wamekubali kusaini mkataba wa amani wa Mei. Wananchi wanaikaribisha hatua hii, lakini pia wengi hawana tena imani na ujumbe wa Umoja wa Mataifa MINUSMA.

Tuareg Rebellen unterzeichnen Friedensabkommen in Bamako

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita(Kushoto) na Mahamadou Djery Maiga, makamu wa rais na msemaji mkuu wa muungano wa makundi yenye silaha ya Azwad, CMA.

Hatimaye siku ya Jumamosi (20.06.2015) wawakilishi wa muungano wa makundi yenye silaha ya Azwad CMA, unaoongozwa na wanamgambo wa kabila la Tuareg nao wamekubali kusaini mkataba wa kuleta amani nchini Mali. Mkataba ambao tayari ulishasainiwa baina ya pande tatu ambazo ni serkali ya Mali, wapatanishi wa kimataifa na makundi ya kiasi ya kabila la Tuareg tangu tarehe 15 Mei, mwaka huu katika mji mkuu wa Bamako. Tofauti na siku za nyuma ambapo mazungumza ya amani yalikuwa yakishindikana.

Mkataba huo wa makubaliano unatoa wito wa kutambulika kwa serikali ya nchi hio katika mji mkuu wa Bamako, na kwa upande mwengine unaipa wanamgambo wa kundi la kikabila la Tuareg wanaodhibiti maeneo ya kaskazini mwa nchi hio haki zaidi. Akiwa katika mazungumzo hayo ya makubaliano ya amani Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita alizungumzia juu ya matumaini yake ya maendeleo kwa taifa hilo, kufuatia kufikiwa kwa makubaliano baina ya pande zinazozozana.

"Utekelezaji wa mpango huu utafungua hatua mpya wa maendeleo, si tu katika mikoa ya kaskazini, bali mikoa yote ya Mali. Mfumo mpya wa kitaasisi wa utawala ulio huru utaimarisha, bila shaka, uwazi katika usimamizi wa umma na utatupa nafasi kusimamia vyema maswali ya usalama, na kutoa nafasi kwa jamii kushiriki zaidi katika kuliendeleza taifa letu, " amesema rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita.

Makubalaino hayo baina ya muungano yaliyosainiwa na waasi wa Tuareg pamoja na serikali ya Mali, yatasitisha mapigano yaliyoanza mwaka 2012 na kuruhusu mamlaka zinazohusika kukabiliana na wanamgambo wa itikadi kali wa Kiislamu waliyo katika eneo la kaskazini mwa jangwa.

Makundi ya waasi wanaotaka kujitenga kaskazini mwa Mali, walianza mashambuli mnamo mwaka 2012. Licha ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwezi wa Mei, kwa msaada wa wapatanishi wa kimataifa machafuko nchini humo yaliendelea.

Wananchi wa Mali wapoteza imani kwa MINUSMA

MINUSMA Soldaten UN Mission Mali

Ujumbe wa kuleta amani Mali, wa Umoja wa Mataifa.

Kwa sasa kuna takriban wanajeshi 11,500 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MINUSMA nchini Mali, ujumbe ambao ulitumwa kuanzia mwaka 2013. Hata hivyo kamanda wa ujumbe huo wa jeshi Michael Lollesgaard ameuambia Umoja wa Mataifa, hata wanajeshi hao wanahofia maisha yao kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo. Lakini kwa upande wa wananchi, wengi wao wanasema hawana tena imani na ujumbe huo wa jeshi la Umoja wa Mataifa kutokana na kushindwa kwao kuudhibiti uasi kwa muda mrefu sasa.

Makubaliano hayo yanajumuisha pia kuondoka kwa wanamgambo wanaoelemea upande wa serikali, katika mji wa kaskazini wa Menaka. Siku ya Alhamisi viongozi wa makundi ya wanamgambo hao walikubali kuondoka katika mji huo, jambo ambalo lilikuwa ndio kikwazo cha mwisho cha kuleta makubaliano kamili ya amani baina ya pande zinazozozana.

Mwandishi :Yusra Buwayhid/dw

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com