1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mogadishu bado si shuwari kamili

Miraji Othman8 Agosti 2011

Wakaazi wa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, uliovurugwa kutokana na vita, leo waliyakimbia tena mapigano katika mji huo.

https://p.dw.com/p/12D7H
Jumuiya za kimataifa za misaada zikipakua shehena zao katika uwanja wa ndege wa MogadishuPicha: dapd

Wakaazi wa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, uliovurugwa kutokana na vita, leo waliyakimbia tena mapigano katika mji huo: Hayo yametokea wakati waasi waliobakia mjini wa kundi la Al-Shabaab baada ya wenzao kuondoka  wiki iliopita, yalipopigana na majeshi ya serikali jana usiku.Milio ya  bunduki ilikuwa ikisikika katika mitaa ya karibu na wilaya ya Suqaholaha na kusababisha wasi wasi mkubwa.

Wapiganaji wa al-Shabaab, wenye maingiliano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida, na ambao walikuwa wanaidhibiti karibu ya nusu ya mji wa Mogadishu, kwa mshangao waliondoka kutoka sehemu hizo siku ya jumamosi. Mapigano ya jana yalitokea katika maeneo kadhaa ya kusini na kaskazini, huku majeshi ya serikali yanayoungwa mkono na Umoja wa Afrika, AU, yakiweka vituo katika ngome za zamani za al-Shabaab. Maafisa wa serikali walisherehekea kuondoka kwa waasi hao, lakini wenyewe wanamgambo wa al-Shabaab walisema hatua yao hiyo ilikuwa tu mabadiliko ya mbinu zao za kijeshi. Msemaji wa al-Shabaab, Abdulaziz Abu Musab, aliwaambia waandishi wa habari kwamba wamewatia adui hasara kubwa, pale majeshi ya kikristo ya uvamizi yalipojaribu kujitanua.

Somalia islamistischer Miliz in Mogadischu Kämpfe Kindersoldaten
Mtoto mdogo ambaye ni mwanamgambo wa al-Shabaab akiwa katika mji wa Mogadishu, Somalia, akiwaongoza wapiganaji wenzakePicha: AP

Majeshi ya serikali yameyatupilia mbali madai hayo ya waasi, yakiripoti tu kufyetuliwa risasi hapa na pale, huku wao, kwa tahadhari, wakiingia katika maeneo ambayo zamani yalishikiliwa na al-Shabaab. Walisema walikuwa hawakabiliani na upinzani hadi sasa, na kwamba waasi wachache waliobakia wanakimbia.

Leo asubuhi  mji wa Mogadishu ulikuwa kimya baada ya mapigano ya jana usiku, lakini wakaazi waliendelea kuuhama wakihofia kutatokea mzozo mwingine. Karibu ya watu laki moja waliokumbwa na ukame wamewasili Mogadishu mnamo miezi miwili iliopita, wakitafuta vyakula, maji na hifadhi, na juhudi za watoaji misaada kuwafikia zikiendelea leo. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia wakimbizi, UNHCR, lilituma kwa ndege shehena za dharura hadi katika mji huo, ikiwa ni operesheni ya mwanzo ya shirika hilo kufanywa tangu kupita miaka mitano. Kwa kawaida, shehena za misaada ya shirika hilo hutumwa kwa meli, lakini kuengezeka kukubwa kwa idadi ya wakimbizi wanaoikimbia njaa kumelilazimisha shirika hilo kutuma misaada hiyo kwa ndege ili kutopoteza wakati.

Sehemu kubwa ya Kusini mwa Somalia, ikiwemo mikoa kadhaa, imetangazwa kuwa na njaa, na inadhibitiwa na waasi wa al-Shabaab ambao wamezipiga marufuku wakala kadhaa za misaada kutofanya kazi katika maeneo hayo.

Nayo Uturuki leo ilipeleka ndege mbili za mizigo ya misaada ya kiutu kwa ajili watu waliokumbwa na njaa Somalia.Tani hamsini za misaada hiyo zitazisaidia familia 1,500 kwa mwezi mmoja, kukiwemo pia tano kumi za madawa na vifaa vya matibabu.

Na katika nchi jirani ya Kenya ambako ukame pia umeingia katika sehemu za kaskazini, serikali ya nchi hiyo na wanasaiasa wamelaumiwa kwa namna wanavolishughulikia suala la ukame na njaa ambapo raia wamechanga shilingi nusu bilioni kuwasaidia walio na njaa. Wakenya milioni 3.5 wako katika njaa iliosababishwa na ukame ulionea katika Pembe ya Afrika, hivyo kuzifanya kampuni za simu za mkono na benki za nchi hiyo kuanzisha kampeni za michango wiki mbili zilizopita. Wakati jamii ikijizatiti kukabiliana na janga hilo, msemaji wa serekali, Alfred Mutua, mwezi uliopita alisema kwamba serikali haina ripoti yeyote ilio rasmi kwamba kuna Wakenya waliokufa kutokana na njaa. Pia seri kali ya Kenya imelaumiwa kwa kushindwa kusambaza mavuno mengi kutoka mikoa ya magharibi na katikati ya nchi hiyo, huku mamilioni ya watu wakikabiliwana na njaa katika mikoa ya kaskazini na mashariki.

Mwandishi : Othman, Miraji/AFP

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed