1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mo Ibrahim: Afrika yapiga hatua katika utawala bora

John Juma
16 Novemba 2020

Faharasa ya utawala bora barani Afrika mwaka 2019 ya wakfu wa Mo Ibrahim, imezitaja Mauritius, Cape Verde, Ushelisheli Tunisia na Botswana kama nchi zilizoongoza. Angola na Somalia zimeshika mkia lakini zinaimarika.

https://p.dw.com/p/3lMqP
Äthiopien Addis Abeba Gipfeltreffen der Staatschefs der Afrikanischen Union
Picha: picture-alliance/AA/Palestinian Prime Ministry Office

Faharasa hiyo kuhusu mwaka 2019 ambayo imezinduliwa Jumatatu jijini London, imesema kwa mwaka wa 10 mtawalia, Mauritius imeendelea kushika nambari ya kwanza katika utawala bora, huku Somalia ikisalia katika nafasi ya mwisho kwa sababu ya changamoto za kiusalama katika baadhi ya maeneo ya nchi kufuatia mashambulizi kutoka kwa wanamgambo wa Al-shabaab.

Kulingana na ripoti hiyo, licha ya changamoto hizo, Somalia imeimarika katika viwango vyake vya uongozi tangu mwaka 2010, hasa kufuatia kuimarishwa kwa miundo mbinu, kuimarishwa kwa usawa wa kijinsia uongozini miongoni mwa masuala mengine.
Kwa mujibu wa Nathalie Delapalme ambaye ni Mkurugenzi Mkuu katika Wakfu wa Mo Ibrahim (MIF), hali imeimarika japo changamoto zipo. Akizungumza na Idhaa ya DW Kiingereza Nathalie Delapalme amesema: "Tangu mwaka 2010, utawala umekuwa ukiimarika barani Afrika, asilimia 60 ya Waafrika waliishi katika nchi ambazo utawala ulikuwa bora kuliko ulivyokuwa mwaka wa 2010. Hata hivyo kasi ya ustawi huo imepungua tangu mwaka 2015, jambo linalotia wasiwasi. Janga la sasa la COVID-19 linaendelea kuwa mbaya na kuathiri nchi zilizopiga hatua hasa katika sekta ya uchumi."

Mambo gani hupimwa?

Kap Verde Ministerpräsident Ulisses Correia e Silva
Waziri mkuu wa Cape Verde Ulisses Correia e Silva moja ya nchi inayotajwa kufanya vema katika utawala boraPicha: Press Office of Prime Minister

Faharasa ya Mo Ibrahim kuhusu utawala katika Afrika hutumiwa kufuatilia na kutathmini viwango vya utawala katika nchi 54 za Afrika kila mwaka. Faharasa hiyo huainisha masuala katika vigezo vinne;


Katika mwaka 2019, ustawi wa kibinadamu ndio uliimarika zaidi miongoni mwa vigezo hivyo vinne vya utawala. Ripoti hiyo inaeleza kuwa ndani ya muongo mmoja uliopita, japo kumekuwa na nafasi za ufanisi kiuchumi na ustawi wa kibinadamu, kumekuwa na upungufu katika masuala ya uzingatiaji wa utawala wa sheria pamoja na usalama.

Japo nchi kama Mauritius, Botswana na Afrika Kusini zinashika nambari ya kwanza, tano na sita kwa msururu huo, viwango vyao vimeendelea kudorora tangu mwaka 2015. Lakini nchi kama Gambia iliyoorodheshwa nambari 16, Ivory Coast nambari 18 na Zimbabwe katika nambari 33, zimeorodheshwa miongni mwa mataifa yaliyopiga hatua kubwa za kuimarika katika muongo mmoja uliopita. Somalia iliyoorodheshwa nambari 54 kwenye faharasi hiyo, ikitajwa kuwa iliyoimarika zaidi. Soma Tuzo ya Mo Ibrahim 2016 yakosa mshindi

Uhuru wa wananchi kujieleza waminywa

Faharasa hiyo imebaini kuwa raia katika zaidi ya nusu ya nchi zilizoshirikishwa, hawajaridhishwa na utawala wa serikali ndani ya miaka kumi iliyopita, wakitaja hatua za kuvurugwa kwa haki za kidijitali na intaneti kuzimwa hivyo kukwamisha mawasiliano.

Elfenbeinküste 2019 Ibrahim Governance Weekend in Abidjan
Mwanzilishi wa wakfu wa Mo IbrahimPicha: DW/F. Quenum

Changamoto za COVID-19

Wakfu wa Mo Ibrahim umekiri kuwa serikali za Afrika zimekumbwa na changamoto zisizo za kawaida kutokana na janga la COVID-19, ambazo zinaweza kuathiri viwango vyao vya utawala. Hata hivyo ripoti inaeleza kuwa bara hilo lilikuwa likididimia katika masuala ya usalama hata kabla ya mripuko wa virusi vya corona, na janga hilo lilifanya tu hali kuwa mbaya zaidi kwa kuzingatia vurugu za chaguzi, kuminya uhuru wa wanaharakati, kuongezeka kwa dhuluma na uwezekano wa machafuko zaidi.

Ukosoaji dhidi ya faharasa ya Mo Ibrahim
Katika miaka ya hivi karibuni, serikali za Afrika zimeushutumu wakfu wa Mo Ibrahim kwa kuchapisha tu ripoti mbaya kuhusu Afrika. Lakini wakfu huo umejitetea kwa kusema ripoti yao huwa ni mkusanyiko wa taarifa ambazo zimekusanywa na makundi kadhaa ya watafiti na si za wakfu huo pekee. Kwamba wanapata taarifa kutoka katika vyanzo 38 tofauti.

Licha ya machafuko kuhusiana na uchaguzi nchini Ivory Coast katika miaka ya hivi karibuni pamoja na tofauti za kisiasa miongoni mwa viongozi wake wa kisiasa, ripoti hiyo imeiweka nchi hiyo miongoni mwa mataifa yaliyoimarika vyema katika muongo uliopita.