Mkutano wa wanawake wafanyika Copenhagen | Masuala ya Jamii | DW | 16.05.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Mkutano wa wanawake wafanyika Copenhagen

Zaidi ya wajumbe 5000 wanakutana mjini Copenhagen katika mkutano wa kujadili masuala ya wanawake ikiwemo afya, pamoja na haki mbalimbali zinazomgusa mwanake na mtoto wa kike duniani

Zaidi ya wajumbe 5000 wanakutana mjini Copenhagen katika mkutano wa kujadili masuala ya wanawake ikiwemo afya, pamoja na haki mbalimbali zinazomgusa mwanake na mtoto wa kike duniani. Umoja wa Mataifa umelenga katika kipindi cha miaka 15 ijayo kuwe na usawa pasipo unyanyasaji na ukatili dhidi ya mwanamke.

Kila dakika mbili inayopita , mwanamke mmoja hupoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi, suala ambalo ni chanzo kikubwa cha vifo kwa mabinti katika nchi zinazoendelea. Asilimia 99 ya vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi vinatokea katika nchi zinazoendelea.

Karibu watoto wachanga milioni tatu hufariki kila mwaka. Wale wanaoachwa na mama zao kutokana na kifo nao hupoteza maisha katika kipindi cha miaka miwili.

Tatizo lingine linalowakumba watoto wa kike ni ndoa za utotoni ambapo kila mwaka mabinti milioni 15 wanaolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18 na hawa wamejikuta katika matatizo makubwa ya uzazi ambayo hupelekea uhai wao kukatika.

Wanawake wengi katika nchi zinazoendelea karibu wanawake milioni 225 hawachukui njia za uzazi wa mpango. Hali hiyo husababisha mimba zisizo tarajiwa , kwa mwaka inakadiriwa mimba zinazotolewa hufikia milioni 26.

Mkuu wa shirika la Afya duniani WHO, Margaret Chan ambaye ni mmojawapo ya washiriki anasema ili maisha ya mwanamke yaweze kustawi dunia inapaswa kufanya haya, namnukuu "Ninapenda kuona wanawake, wanawake wote wakifikia katika ngazi ya kupigania maendeleo endelevu. Ili hilo liweze kutokea, dunia isiwaache wanawake na watoto wa kike nyuma. Inamaanisha wawe mbele. Ni kuhakikisha unyanyasaji na ukatili haupo dhidi yao. Wafike sehemu ambayo watapata fursa ya elimu na kazi wanayostahili" mwisho wa kunukuu.

Ngariba akiwa na vifaa vya ukeketaji

Ngariba akiwa na vifaa vya ukeketaji

Ukeketaji ni tatizo lingine ambalo linawakabili wanawake hasa watoto wa kike. Mabinti milioni 200 katika nchi zipatazo 30 katika mabara matatu wamepitia ukeketaji ambao unatajwa kuwa na athari kubwa za kiafya ikiwemo matatizo wakati wa kujifungua.

Watoto wa kike pia bado wanakabiliwa na hatari ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI, asilimia 72 ya mabinti wanaoishi na VVU wanapatikana katika eneo la kusini mwa janga la sahara.

Mshiriki mwingine Helle Thorning-Schmidt , Mkurugenzi wa shirika la Save the children, anasema "Licha ya hatua kubwa zilizopigwa, watoto wa kike bado hawapati fursa sawa na wale wa kiume, katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. Sheria na sera zitungwe ili kuwasaidia wanawake na watoto wa kike. Hii inamanisha kupiga vita tamaduni zote mbaya, ikiwemo ndoa za utotoni, ukeketaji na kila aina ya ukatili. Ni lazima wapate elimu na huduma za afya."

Wanawake wengi karibu milioni 2 wamepata ugonjwa wa Fistula, ambao ni matokeo ya majeraha wakati wa kujifungua.

Suala la unyanyasaji kwa wanawake nalo ni tatizo ambalo bado linapaswa kupigiwa kelele , inaonyesha mwanamke 1 kati ya 4 anapatwa na ukatili wakati wa ujauzito.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com