1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSingapore

Mkutano wa Usalama wa Shangri-La wafunguliwa Singapore

2 Juni 2023

Mkutano wa kilele wa masuala ya usalama unaofahamika kama jukwaa la Shangri-La umefunguliwa leo Ijumaa nchini Singapore.

https://p.dw.com/p/4S8HR
Mkutano wa Shangri-La Singapore
Mkutano wa Shangri-La Singapore Picha: Vincent Thian/AP Photo/picture alliance

Inatazamiwa mjadala utatuama juu ya kutanuka kwa ushawishi wa China duniani na taathira ya vita vinavyoendelea nchini Ukraine. 

Mkutano huo wa siku tatu utakaoendelea hadi siku ya Jumapili unawaleta mbele ya jukwaa moja wawakilishi karibu 600 kutoka mataifa 40 duniani ikiwemo Marekani, China, Uingereza, Ujerumani na Australia kujadili kwa upana masuala ya ulinzi na usalama.

Mkutano huo utajumuisha mijadala miwili ya wazi ya ngazi ya mawaziri itakayojikita juu ya kuainisha changamoto za usalama kwenye kanda ya Asia na eneo zima la Pasifiki na kisha kupendekeza suluhisho linalotekelezeka.

Vita vya Ukraine vitakuwa sehemu ya majadiliano ya Shangri-La 

Deutschland Berlin | Ben Wallace, Verteidigungsminister Großbritannien | PK mit Boris Pistorius
Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Ben Wallace Picha: Nadja Wohlleben/REUTERS

Ijapokuwa  mkutano wa Shangri-La kwa kawaida ni jukwaa la kujadili masuala ya usalama barani Asia, kwa mwaka huu yumkini utagubikwa pia na vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

Katika siku ya kwanza hii leo, tayari mzozo wa Ukraine umejitokeza wazi wazi. Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace anayehudhuria mkutano huo amesema nchi yake inaunga mkono Ukraine kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na kwamba njia iko wazi kwa taifa hilo licha ya ukweli kwamba mchakato huo utakuwa mrefu.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters pembezoni mwa mkutano wa Shangri-La, Wallace amefahamisha lakini licha ya uungaji mkono wa Uingereza juu ya suala hilo, Ukraine itapaswa kwanza isubiri hadi vita vinavyoendelea vimalizike kabla ya kukaribishwa kuwa mwanachama wa NATO.

"Tuwe wakweli, kitu pekee tunachoweza kufanya sasa kuisadia Ukraine ni kuwawezesha kuishinda Urusi na baada ya hapo ni kuhakikisha wanakuwa tayari kwa uwezo kuhimili mahsambulizi yoyote ya Urusi siku zijazo na hilo ni kuipa nafasi ya kuwa na uhusiano wa siku za usoni na Jumuiya  ya NATO."

Ushawishi wa China litakuwa ajenda ya juu ya mkutano wa Singapore

Asia Defense
Picha: Vincent Thian/AP/picture alliance

Suala jingine kubwa kwenye mkutano wa Shangri-La itakuwa ni ushawishi unaoongezeka wa China duniani na hasa kwenye kanda ya bahari ya Hindi na Pasifiki.

Mataifa ya magharibi yana wasiwasi na kutanuka kwa nguvu za China lakini hayawezi tena kuipuuza dola hiyo ya mashariki ya mbali yenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Shangri-La Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese ametoa wito wa ushirikiano kati ya Marekani na China ambazo zimetumbukia kwenye uhasama na vitendo vya kutunishiana misuli.

Albanese amewaambia wajumbe kwamba iwapo njia za majadiliano kati ya madola hayo mawili zitasambaratika kutakuwa na athari kubwa kwa ulimwengu.

Mawaziri wa China na Marekani wapeana mkono wa salamu 

Mawaziri wa China na Urusi wakisalimiana mjini Singapore
Mawaziri wa China na Urusi wakisalimiana Picha: Vincent Thian/AP/picture alliancePRESS

Mapema hii leo mawaziri wa ulinzi wa Marekani na China wanaoshiriki mkutano huo walikutana ana kwa ana na kupeana mikono.

Katika mkanda wa video uliorushwa kwenye mitandao ya kijamii waziri Lloyd Austin wa Marekani alionekana akitabasamu wakati akipeana mkono na mwenzake wa China Li Shangfu. 

Hata hivyo imearifiwa kwamba mbali ya kusalimiana hakuna chochote walichozungumza juu ya mahusiano baina ya nchi zao.

Wote wawili wamepangiwa kuhutubia mkutano huo kesho Jumamosi ambapo waziri wa China atatumia jukwaa hilo kutangaza na kufafanua mpango mpya wa usalama wa Beijing kwenye kanda hiyo.

Ujerumani kwa upande wake imemtuma waziri wake wa ulinzi  Boris Pistorius kushiriki mkutano huo unaohudhuriwa pia na afisa wa ngazi ya juu wa Jumuiya ya NATO na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya.