Mkutano wa kilele wa G 20 nchini Mexico | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.06.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa kilele wa G 20 nchini Mexico

Mnamo siku ambayo wapiga kura wa Ugiriki wanateremka vituoni kulichagua bunge jipya,viongozi wa taifa na serikali wa mataifa 20 makubwa kiviwanda na yale yanayoinukia,wanakutana katika mji wa pwani wa Los Cabos .

default

Nembo ya mkutano wa kilele wa G20 nchini MNexico

Kimsingi kuna mada tofauti muhimu zilizopangwa kwaajili ya mkutano huo wa G-20 nchini Mexico:juhudi za kutuliza uchumi wa dunia,kuepukana na ukosefu wa usawa,kuimarisha mfumo wa fedha na mageuzi katika mfumo wa fedha wa dunia.Lakini macho ya walimwengu yatakodolewa katika nchi ndogo ya Ulaya ambayo hatima ya sarafu ya Ulaya-Euro itategemea hali ya mambo katika nchi hiyo:Ugiriki.Ikiwa ushirika wa mrengo wa shoto utajikingia wingi wa viti na kugeuka kuwa nguvu muhimu katika bunge,hapo mpango wa umoja wa ulaya wa kuhimiza hatua za kufunga mkaja,utaingia hatarini.Mpango wa kufunga mkaja ukiachiliwa mbali,hakutakuwa tena na uwezekano wa kupatiwa misaada kutoka Umoja wa Ulaya kwa hivyo matokeo yake ni kuiona Ugiriki katika kipindi cha muda mfupi utakaofuatia,ikishindwa kutekeleza majukumu yake na kwa hivyo kuwa muflis.

Hispania na Italy zinaweza kufuata anaonya Jörge Hinze wa taasisi ya mjini Hamburg inayoshughulikia masuala ya uchumi wa dunia na kusema:

" Mgogoro wa fedha ukizuka katika kanda ya Euro,uchumi wa dunia utaathirika.Hata nchi zinazoinukia na zile zinazoendelea zitaathirika.Ndio maana ni kwa masilahi ya nchi hizi pia kama balaa la kiuchumi kama lile la mwaka 2009/2010 halitatokea tena."

G-20 Gipfel Los Cabos Mexiko Proteste masken

Masanamu ya viongozi wanaoshiriki katika mkutano wa G 20

Ili kuepukana na balaa kama hilo,viongozi wa G-20 wanataka kuimarisha nguvu za shirika la fedha la kimataifa IMF.Kwa kupatiwa mikopo ziada mataifa wanachama,dola bilioni moja zitaweza kupatikana ili kujikinga dhidi ya migogoro ya kimataifa.Zaidi ya hayo mapendekezo yatakayojadiliwa Mexico si mepya.Kansela wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Angela Merkel anataka kupigania hatua kali zaidi katika kuchunguzwa shughuli za benki.

Mtaalam wa taasisi ya kiuchumi ya mjini Hambourg Jörg Hinze anasema madai hayo yametolewa tangu benki ya Lehman ilipofilisika-lakini hadi wakati huu hayakutekelezwa kikamilifu.

September mwaka 2008,benki ya uwekezaji ya Marekani-Lehman Brothers ilifilisika na miaka miwili baadae Umoja wa Ulaya ukaamua kuanzisha mfumo wa kusimamia shughuli za kiuchumi kwa ufupi ESFS.Mpango huo ulilengwa kumulika shughuli za benki,mashirika ya bima sawa na mitindo ya hatari ya kubahatisha katika masoko ya hisa.Yote hayo hayakuleta tija anahisi Peter Wahl wa shirika lisilomilikiwa na serikali la Uchumi wa Dunia,Ekolojia na Maendeleo-WEED.

Peter Wahl aliyataja madai yaliyotolewa na kansela Angela Merkel kuhusu kufanyiwa marekebisho kwa kila hali mfumo wa benki,kuwa ni ya maana lakini usiotekelezeka.

Rio 20 +

Rio de Janeiro

Sababu moja kubwa ya kutoweza kutekelezeka mpango huo,anasema Peter Wahl ni zile hofu za wanasiasa linapohusika asuala la mashindano ya kibiashara.

Hata katika mada ya pili kuu katika mkutano huo wa G-20 nchini Mexico yaani kodi ya shughuli za fedha ambayo Ujerumani inaitetea inakabiliana na ubishi mkubwa tokana na hofu za mashindano ya kibiashara.

Hata kabla mkutano huo wa kilele wa G-20 kuanza,dalili zilianza kuchomoza kwamba viongozi watataka kuyashawishi madola mawili makubwa kiuchumi,Ujerumani na Canada yachangie zaidi katika kuinua uchumi wa dunia.Kansela Angela Merkel ameshasema nguvu za kiuchumi za Ujerumani si za milele.Kansela Angela Merkel ametahadharisha dhidi ya kuitwika mzigo mkubwa kupita kiasi Ujerumani,akaikumbusha kuna mataifa mengine pia yenye nguvu za kiuchumi:Marekani na China.

Mwandishi: Gehrke,Mirjam/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Yusuf Saumu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com