Mkataba wa amani Sudan Kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkataba wa amani Sudan Kusini

Wajumbe wa serikali na waasi wameutia saini mjini Addis Ababa, mkataba wa kuleta amani katika Sudan Kusini. Lakini katika maoni yake mwandishi wetu Daniel Pelz anasema, licha ya mkataba huo, amani haitarejea haraka

Umwagikaji damu katika Sudan Kusini bado haujakomeshwa licha ya wawakilishi wa pande zote mbili kuutia saini mkataba wa kusimamisha mapigano .

Redaktionsleiter Daniel Pelz

Mkuu wa Idhaa ya Kiingereza DW Daniel Pelz

Ikiwa serikali ya Sudan na waasi wanadhamiria kuleta amani katika nchi yao pande hizo zitapaswa kuchukua hatua zaidi, baada ya kusimamishwa mapigano na kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa. Sudan inapaswa kujengwa kutokea kwenye mizizi.

Udikteta chini ya pama

Hata hivyo inapasa kusema kwamba mpaka sasa Rais Salva Kiir bado hajaonyesha kuwa kiongozi anaeona mbali. Chini ya uongozi wa Salva Kiir Sudan inafanana na nchi ya udikteta wa kijeshi.

Si Bunge wala Mahakama yenye usemi katika Sudan Kusini, bali ni kikundi kidogo cha viongozi na washirika wao wa chama cha ukombozi wa Sudan,SPLM .Chama hicho kiliendesha harakati za ukombozi kwa muda wa miaka, zaidi ya 20, kama jeshi la waasi, kupigania uhuru wa Sudan Kusini. Wakati huo Sudan Kusini bado ilikuwa sehemu ya Sudan.

Kikundi cha watu hao kimekuwa kinaichukulia Sudan Kusini kama mali yao binafsi, tokea kupatikana kwa uhuru mnamo mwaka wa 2011. Mawaziri wanaiba mabilioni ya fedha,wanajeshi na polisi wanawatesa na kuwaua waandishi habari na watu wanaodiriki kuikosoa serikali

Mapigano kati ya makabila na ufisadi

Kabla ya kuzuka mapigano baina ya watu wa Rais Salva Kirr na mpinzani wake RieK Machar, Sudan Kusini takriban yote ilikumbwa na migogoro ya kikabila.Serikali ilituma wanajeshi kwenda kuizima migogoro hiyo. Watu hawajayaona mageuzi katika jeshi yaliyoahidiwa siku nyingi na wala mawaziri fisadi bado hawajafukuzwa. Sheria ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari inaingia vumbi.

Nyadhifa za juu zinatolewa kwa watu waliokuwa wapiganaji wa kundi la SPLM , bila ya kujali iwapo wanao uwezo wa kufanya kazi. Riek Machar pia alishiriki katika udhalimu huo,hadi alipofukuzwa na Rais Salva Kiir mwaka uliopita.Machar alikuwa makamu wa Rais.

Lazima Salva Kiir abadilike

Sasa ni vigumu kuamini iwapo Rais Salva Kirr atabadilika na kuanza kuzijenga taasisi zinazofanya kazi na au atabadilika na kuwa tayari kuyasikiliza yanayosemwa na asasi za kiraia na vyombo vya habari. Lakini ikiwa hatabadilika,na ikiwa mamailioni ya watu wake watakuwa na hisia kwamba serikali yao haiwajali, itakuwa rahisi kwa hasimu wake Riek Machar kuwaandikisha wanamgambo na kupigana na serikali.

Amani ya kudumu itapatikana katika Sudan kusini ikiwa serikali itaitekeleza miradi ya ujenzi wa nchi. Sudani Kusini bado imo miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani licha ya kuwa na raslimali kubwa ya mafuta.

Mikataba ni mingi lakini usalama ni mdogo.Na Riek Machar ni kigeugeu. Salva Kiir na Riek Machar wameshatia saini mikataba mingi baina yao,kwa manufaa yao uliotiwa saini jana ni mmojawapo. Ikiwa mmoja wao anaona kuwa atapata manufaa zaidi kwenye uwanja wa mapambano kuliko kwenye meza ya mazungumzo,basi moto unaweza kuwa tena haraka. Lakini wanaoungua ni raia.

Mwandishi:Pelz Daniel.

Tafsiri;Mtullya Abdu.

Mhariri:Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com