Mkataba wa Amani Sudan Kusini watiwa saini | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkataba wa Amani Sudan Kusini watiwa saini

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi dhidi ya serikali yake, Riak Machar wamesaini makubaliano ya kuacha mapigano. Ulimwengu umeyakaribisha makubaliano hayo, kama hatua nzuri kwa mustakabali wa nchi hiyo.

Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi, Riek Machar baada ya kusaini makubaliano mjini Addis Ababa

Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi, Riek Machar baada ya kusaini makubaliano mjini Addis Ababa

Jumuiya ya Maendeleo katika Pembe ya Afrika, IGAD ambayo iliyosimamia mazungumzo baina ya viongozi hao Ijumaa mjini Addis Ababa, imesema uhasama unapaswa kusitishwa katika muda wa saa 24 tangu kusainiwa makubaliano hayo.

Makubaliano mengine yaliyosainiwa na viongozi hao mwezi Januari yalivunjika baada ya muda mfupi. Tangazo la IGAD limesema kuwa Kiir na Machar wamekubaliana kuunda serikali ya umoja wa taifa ambayo itaiongoza nchi hadi uchaguzi mpya utakapofanyika. Viongozi hao wameafikiana pia kukutana tena baada ya mwezi mmoja, huku shirika la IGAD likiufanyia kazi muundo wa serikali ya mpito.

Mustakabali wa matumaini

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye amesaidia katika juhudi za usuluhishi kwenye mgogoro wa Sudan Kusini, amesema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, kuwa ''Tunatarajia kwa matumaini mkutano mwingine ambao utaimarisha muafaka uliopatikana leo''.

Mapigano yaliyodumu kwa miezi 5 yameuwa maelfu na kuwalazimisha zaidi ya milioni 1 kuyahama makazi yao

Mapigano yaliyodumu kwa miezi 5 yameuwa maelfu na kuwalazimisha zaidi ya milioni 1 kuyahama makazi yao

Makubaliano hayo ya amani kwa Sudan Kusini yamefikiwa kufuatia wasiwasi ambao umekuwa ukizidi kuongezeka katika jumuiya ya kimataifa mnamo wiki za hivi karibuni. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye aliizuru Sudan Kusini mapema wiki hii alisema ameshuhudia ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa vile vile imeelezea uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu na ukiukaji wa sheria ya kimataifa katika taifa hilo changa zaidi duniani.

Mgogoro ulioibuka nchini Sudan Kusini Desemba iliyopita na ambao ulichukua sura ya ukabila umeuwa maelfu ya watu na kuwalazimisha wengine takribani milioni 1.3 kuyahama makazi yao. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa tahadhari kuhusu kile lilichokiita ''mauaji ya kutisha dhidi ya raia.

Ahueni kwa jumuiya ya kimataifa

Mkataba wa amani uliofikiwa umekaribishwa na jumuiya ya kimataifa. Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ambaye ndie kiongozi wa IGAD kwa wakati huu, amewaambia viongozi wa Sudan Kusini kwamba ''Tunawaangalia kwa makini, na hatutawaruhusu kuingia vitani tena.''

Maelfu ya raia wamejikuta wakitaabika katika kambi za wakimbizi

Maelfu ya raia wamejikuta wakitaabika katika kambi za wakimbizi

Mshauri wa Rais wa Marekani kuhusu masuala ya usalama, Susan Rice ametoa tamko mjini Washington, akisema hatua hiyo inaleta matumaini ya kuumaliza mgogoro wa Sudan Kusini. Mshauri huyo wa rais Barack Obama amewataka rais Salva Kiir na mpinzani wake Riak Machar kuendelea na nia njema ya mazungumzo na kufikia makubaliano ya kisiasa.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ambaye pia aliitembelea Sudan Kusini hivi karibuni, amesema makubaliano yaliyofikiwa yanaweza kusafisha njia kwa mustakabali mwema wa Sudan Kusini, akiyaita hatua ya kwanza kuelekea safari ndefu.

Viongozi wanaohasimiana nchini Sudan Kusini wamekuwa wakikabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa, kuwataka wasitishe mapigano angalau kwa muda ili wananchi waweze kupanda mazao yao katika msimu huu wa kilimo.

Mashirika ya msaada yalikuwa yakionya kuwa ikiwa wakulima hawataweza kupanda mbegu katika msimu huo, Sudan Kusini ingekabiliwa na janga kubwa la ukosefu wa chakula.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com