Mjadala wa kitaifa Tunisia waambulia patupu | Matukio ya Afrika | DW | 05.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mjadala wa kitaifa Tunisia waambulia patupu

Mazungumzo ya kumtafuta waziri mkuu mpya wa Tunisia yameahirishwa kwa muda usiojulikana, baada ya viongozi wa kisiasa kushindwa kuelewana juu ya mtu ambaye ataiongoza nchi kutoka katika mkwamo.

Mjadala wa kitaifa ulioanza tarehe 25 Oktoba umeahirishwa kwa muda usiojulikana

Mjadala wa kitaifa ulioanza tarehe 25 Oktoba umeahirishwa kwa muda usiojulikana

Tangazo la kiongozi wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi UGTT ambalo ni msuluhishi katika mgogoro wa Tunisia, ambalo lilitolewa baada ya mkutano wa jana jioni halikuashiria matumaini yoyote.

Kiongozi huyo Houcine Abbas alisema ''Tumeamua kusimamisha mjadala wa kitaifa hadi pale yatakapokuwepo mazingira mazuri ya kupata makubaliano. Tumejaribu kusuluhisha tofauti zilizopo lakini hatukupata muafaka juu ya mtu ambaye ataiongoza serikali''.

Mkwamo wa kisiasa ulizidishwa na kuuawa kwa wanasiasa wa upinzani

Mkwamo wa kisiasa ulizidishwa na kuuawa kwa wanasiasa wa upinzani

Mkutano wa mwisho katika juhudi za kumaliza mkwamo katika nchi hiyo ulianza jana saa saba mchana, saa mbili baada ya muda wa mwisho uliokuwa umewekwa kutangazwa jina la waziri mkuu mpya. Mazungumzo hayo yaliyoanza tarehe 25 Oktoba yalitazamiwa kuunda serikali ya wataalam ambayo ingeandika katiba mpya na kuandaa uchaguzi huru.

Vuta nikuvute katika majina ya wagombea

Watu waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuchaguliwa ni pamoja na Mohammed Ennaceur anayeungwa mkono na upinzani, na Ahmed Mestiri aliyependekezwa na chama cha Ennahda na washirika wake. Hata hivyo, kila upande ulikataa kumkubali mgombea wa upande mwingine.

Tunisia ilikumbwa na mvutano mkubwa baada ya kuangushwa kwa utawala wa muda mrefu wa Zine El Benadine Ben Ali katika vuguvugu la mwaka 2011, na mvutano huo uliongezeka zaidi mwaka huu kufuatia kuuawa kwa wanasiasa wawili wa upinzani, Chokri Belaid aliepigwa risasi mwezi Februari, na Mohammed Brahmi aliyeuawa kwa njia hiyo hiyo mwezi Julai.

Kwa muda mrefu Tunisia imekuwa chini ya utawala wa sheria ya hali ya hatari

Kwa muda mrefu Tunisia imekuwa chini ya utawala wa sheria ya hali ya hatari

Serikali na upinzani wanakubaliana kwamba wakereketwa wenye mrengo mkali wa kiislamu, ambao walikandamizwa wakati wa utawala wa Ben Ali ndio chanzo cha vurugu zilizoikumba nchi, ikiwa na pamoja na mauaji dhidi ya wanasiasa hao.

Mchakato warudi ulikoanzia

Upinzani ulikuwa umeitaka serikali inayoongozwa na chama cha kiislamu cha Ennahda ijiuzulu, na nafasi yake ichukuliwe na serikali isioegemea upande wowote, wakiishutumu kushindwa kukabiliana na wimbi la wapiganaji wa kiislamu.

Waziri mkuu wa sasa Ali Larayedh alikuwa ameridhia kuachia ngazi, kuheshimu mpango wa mpito ambao ungetokana na mjadala wa kitaifa.

Sasa chama chake cha Ennahda kitalazimika kuendelea kuzungumza na upinzani kuhusu tarehe ya uchaguzi na muundo wa tume ya uchaguzi, na kukamilisha kazi ya kuandika katiba mpya kabla ya muda wa chama hicho madarakani kufikia kikomo mwishoni mwa mwezi huu.

Jumapili iliyopita, Ikulu ya Tunisia ilitangaza kurefushwa kwa sheria ya hali ya hatari kwa miezi minane zaidi. Muda wa sheria hiyo umekuwa ukirefushwa mara kwa mara.

Habari njema kwa nchi hiyo licha ya mkwamo wa kisiasa, ni tangazo la waziri wa fedha wa nchi hiyo kuwa uchumi wake utakuwa kwa asilimia 4 mwaka 2014.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza