Mitandao ya Kijamii yalaumiwa kusambaa kwa Habari za Uongo | Masuala ya Jamii | DW | 27.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Mitandao ya Kijamii yalaumiwa kusambaa kwa Habari za Uongo

Kongomano la Kimataifa la Vyombo vya Habari linaendelea mjini Bonn na siku ya kwanza mjadala mkubwa umetuama juu ya nafasi ya mitandao ya kijamii ambayo katika miaka ya karibuni imekuwa kitovu cha upatikanaji habari.

Hata hivyo mitandao ya kijamii imegeuka kuwa chanzo cha wasiwasi wa kusambaa kwa habari za uzushi na upotoshaji. 

Katika majadiliano ya wazi yaliyowajumuisha wawakilishi wa vyombo vya habari na afisa kutoka kampuni ya Facebook suala la kuongezeka  kitisho cha kusambaa habari za uzushi na upotoshaji  limeibuka kuwa changamoto kubwa kabisa zama za mapinduzi ya teknolojia.

Mkurugenzi wa kampuni ya habari kupitia mtandao  ya Axel Springer, Mathias Döpfner, ameyalaumu makapuni makubwa ya mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook na Google kwa kutochukua hatua madhubuti kukabiliana na kitisho cha habari bandia.

Kampuni hizo zimelaumiwa kwa kushindwa kuweka mifumo kamili ya usalama ikiwa ni pamoja na kuzuia kusambaa kwa taarifa za uuzushi na kuchukua hatua za kupunguza uwepo wa akaunti bandia zinazoendesha shughuli za kusambaza chuki na taarifa za uongo.

Mhariri mkuu wa jarida la India Today Aroon Purie amesema changamoto kubwa ni kuwa makampuni yanayomiliki mitandao ya kijamii yamegeuka kuwa biashara badala ya kufanya kazi ya kutoa huduma na kusaidia jamii.

Facebook inafanya nini?

Plenary Session: Who’s got the power in the media landscape? Part 1

Jesper Doub, Mwakilishi wa Facebook

Mwakilishi wa kampuni ya Facebook anayehudhuria kongamano hilo  Jesper Doub amesema licha ya lawama zinazoelekezwa kwa Facebook kampuni hiyo imekuwa ikichukua hatua kupambana na habari za uzushi na akaunti bandia.

"Tunaondoa zaidi ya akaunti bandia milioni moja kila siku na nyingi tunaziondoa hata kabla hazijafunguliwa kwa sababu tunaona zinavyoanzishwa. Hilo linakwenda sambamba na uondoaji taarifa za uzushi. Tumewekeza sana kwa ajili ya usalama na kudhibiti habari bandia na wavamizi mtandaoni." amesema Doub

Rais Steinmeier asifu nafasi ya Vyombo vya Habari

Mapema leo Asubuhi Rais wa Shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alitumia hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano hilo kuusifu mchango wa mkubwa wa vvombo vya habari na mitandao ya kijamii katika kukuza demokrasia na uwajibikaji lakini akaonya juu ya matumizi mabaya mitandao ya kijamii yanayotishia ustawi na mahusiano  kwenye jamii.

Kwa upande wao washiriki kutoka eneo la Afrika Mashariki wanaodhuria kongamano hilo wameelezea matumaini yao ya kujifunza na kubadilishana mawazo kuhusu kile kinachoweza kufanywa ili kuboresha nafasi ya uandishi habari katika maendeleo duniani.

Kongamano hilo la siku mbili ambalo huandaliwa kila mwaka na Shirika la Utangazaji la DW linawakutanisha zaidi ya wajumbe 2000 ikiwemo waandishi habari, wanaharakati, wanasayansi na wawakilishi wa mashrikia yasiyo ya kiserikali kujadili nafasi ya vyombo vvya habari katika maendeleo ya ulimwengu.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com