1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo wiki hii

27 Novemba 2009

Bayern Munich inacheza na Hannover 96

https://p.dw.com/p/Kjer
Gomez wa B.MunichPicha: AP

KOMBE LA CECAFA:

Kinyan'ganyiro cha kuania Kombe la Afrika Mashariki na kati-Challenge Cup au Kombe la (CECAFA) kimeanza leo mjini Nairobi, Kenya-nani mwishoe, ataibuka bingwa ?

Kura itapigwa ijumaa ijayo mjini Cape Town,Afrika Kusini kuamua jinsi timu 32-6 kutoka Afrika zitakavyoumana kuania taji la 2010.Timu za Afrika zitaangukia kundi gani ?

Wakati katika Bundesliga, macho yanakodolewa mpambano kati ya Bayern Munich na Hannover 96 mjini Hannover ,katika Premier League, viongozi wa Ligi-Chelsea wana miadi leo na Arsenal.

Firimbi inalia leo huko Kenya, kuanzisha kinyan'ganyiro cha mwaka huu cha Kombe la Challenge Cup-kombe la Shirikisho la dimba -kanda ya Afrika Mashariki na Kati.Je, jogoo la shamba litawika mjini au Harambe Stars, watawika nyumbani ?

Ni timu gani safari hii kutoka kanda ya CECAFA na nje yake zinashiriki ? Mara hii ni ameripoti Eric Ponda ni zamu ya Zambia na Zimbabwe. Taifa Stars,Tanzania, haikutwaa Kombe hili tangu miaka 15 na inadai huu ni mwaka wake. Miongoni mwa timu za asili ni Uganda na Zanzibar,lakini kuna pia Ethiopia na Somalia.Kinyan'ganyiro hiki kitadumu wiki 2 kabla mshindi kujulikana mjini Nairobi.

Kabla kuanza Kombe hilo la Challenge, Rwanda, mojawapo ya timu za CECAFA zinazoania kombe hili, ilimtimua kocha wake Branco Tucak.Hii ilifuatia mlolongo wa kushindwa kwa timu ya taifa ya Ruanda na hasa kutofuzu kucheza Kombe lijalo la Afrika la Mataifa nchini Angola.

Mcroat huyo mwenye umri wa miaka 57 aliechukua uongozi wa Amavubi ,April, 2008 alipigwa kumbo na Shirikisho la dimba la Ruanda (FERWAFA ) baada ya Amavubi kuburura mkia wa kundi la 3 katika duru za mwisho za kuania tikiti za Kombe la Afrika na dunia.Mkataba wa Branco,ulikuwa umalizike mwishoni mwa April, 2010.Usukani wa Amavubi sasa umo mikononi mwa makamo wake Eric Nhsimiyimana ambae ndie alieiandaa Ruanda kwa Kombe hili la Challenge Cup nchini Kenya.Kwavile, yeye ni kocha wa muda tu, hatima yake itategemea vipi Amavubi watavyoweza kutimua vumbi huko Nairobi .

Kombe lijalo la dunia 2010 nchini Afrika Kusini :

Kabla ya firimbi kulia kuanzisha dimba Juni 11,2010 hadi finali Julai 11, kura itapigwa ijumaa hii ijayo katika hafla ya muda wa saa 1 na nusu mjini Cape Town,kuzigawa timu hizo 32 katika makundi 8 ya timu 4 kwa duru ya kwanza: Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya kombe hili ,ina timu 6 mara hii pamoja na wenyeji Bafana Bafana:

Zaidi ya miaka 3 tangu firimbi ya kwanza kulia kuanzisha kinyan'ganyiro cha kuania tiketi za kufuzu kwa Kombe la dunia 2010,la kwanza barani Afrika, ijumaa ijayo hatima ya kila timu kati ya zote 32 itajulikana-nani anacheza na nani na timu gani imeangukia kundi la kufa-kupona.

Sherehe hiyo mjini Cape Town itachukua muda wa dakika 90 na vyombo vya TV ulimwengu mzima vitakodoa macho huko,kwani Kombe la dunia mwishoe, limewasili Afrika. Na wale waliosema "haiwi,watajua siku hiyo,kwamba imekuwa".

Inadhihirika utaratibu uliotumika katika Kombe la dunia 2006 hapa Ujerumani ,utatumika tena ijumaa ijayo .Kwa muujibu wa mfumo huo nafasi ya timu katika orodha ya timu bora za dunia mnamo miaka 3 iliopita na ilivyocheza katika mashindano 2 yaliopita ya Kombe la dunia huwa kipimo cha kuamua kuwa kileleni mwa kila kuni kati ya yote 8 ya timu 4 kila moja.

Hii itakuwa na maana kuwa Brazil itakuwa kileleni kabisa ,ikifuatwa na Ujerumani,halafu mabingwa wa ulaya Spian,mabingwa wa dunia Itali na Uingereza.

Baada ya kura hiyo kupigwa, macho yatakodolewa ijumaa, Juni 11,2010 itakapolia firimbi ya kwanza huko Soccer City Stadium, uwanja mpya wa dimba mjini Johannesberg.Timu 2 zitakazofungua dimba ni timu ya kwanza kileleni dhidi ya timu ya pili kutoka kundi A.Mechi 63 zitakazofuatia , zitachezwa katika viwanja mbali mbali vya Afrika Kusini kutoka Polokwane huko kaskazini-mashariki hadi Cape Town,katika bahari ya Hindi.Jumla ya viwanja 10 vitachezewa dimba hilo.Kilele cha Kombe la kwanza la dunia barani Afrika, kitakuwa Julai 11,2010 katika Soccer City Stadium, Johannesberg, ambako mara hii, waafrika eti wameshapiga ramli na kujua moja kati ya timu 6 za Afrika itateremka uwanjani siku hiyo.

Safari ya Afrika Kusini 2010 ilikua ndefu,kwani, ilianza August 25,2007 huko Oceania pale mashabiki 60 tu walipofika uwanjani kukishuhudia kisiwa cha Samoa kikipambana na vanuatu. Tangu mwaka huo, mashabiki milioni 20 walisheheni viwanjani kujionea timu za mataifa 204 zikipigana vikumbo hadi 32 za mwisho. Uruguay, mabingwa wa kwanza kabisa wa dunia,kombe hilo lilipochezwa mara ya kwanza 1930 huko Montevideo, ndio timu ya mwisho kukata tiketi yake ya Afrika kusini.

Mpambano wa mwisho wa kufa-kupona uliochafua usuhuba wa kibalozi kati ya majirani 2 ulikuwa Khartoum,Sudan kati ya mabingwa wa Afrika,mafiraouni Misri na mahasimu wao wa jadi,Algeria. Baada ya kukwepa baadhi ya mawe yaliovurumishwa na mashabiki wa Misri mjini Cairo, kaburi waalgeria waliowachimbia (mafiraouni) huko Algiers,liliwazika Khartoum,Sudan. Wamisri,hawatausahau mpambano ule,kwani Kombe la dunia barani Afrika bila ya mabingwa wa Afrika lawezekanaje?

Iliobaki sasa ni juu ya rais Muamar Gadhafi wa Libya, jirani yao kupatanisha na kurejesha usuhuba mwema kati ya Cairo na Algiers.Jaribio kama hilo linafanywa wakati huu kati ya Ireland na Ufaransa, baada ya Thierry Henry,nahodha wa Ufaransa, kuunawa mpira na kuipiga kumbo Ireland nje ya Kombe la dunia 2010.

Bundesliga na Premier League:

Bayern Munich, mabingwa mara kadhaa, wana miadi leo na Hannover 96 wakati viongozi wa Bundesliga,Bayer Leverkusen, wanapambana na Stuttgart.Mabingwa Wolfsburg wanatoana jasho na Werder Bremen iliopo pointi 1 tu nyuma ya Leverkusen kileleni.

Ama katika Premier League-ligi ya Uingereza, Chelsea, viongozi wanakutana na Arsenal ,wakati mahasimu wao wakubwa Manchester United wanataraji kuinyemelea Chelsea hadi pointi 2 kwa kuitoa leo Portsmouth.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ AFPE/DPAE

Uhariri: Aboubakary Liongo