Michezo wiki hii | Michezo | DW | 24.04.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Michezo wiki hii

Wolfsburg yatamba bado katika Bundesliga-Manu katika Premier League.

default

Lukas Podolski -Munich itaipiku leo Wolfsburg

Wakati katika Bundesliga,Wolfsburg inaongoza bado kwa pointi 3,Manchester United ilidhibiti Premier League-Ligi ya Uingereza juzi kwa kuizaba Portsmouth mabao 2-0.

Finali ya Kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB) itakua kati ya Bayer Leverkusen na Werder Bremen katika uwanja wa olimpik wa Berlin mwezi ujao .Martin Lel wa Kenya atazamiwa kutamba kesho katika London marathon upande wa wanaume.Ule wa wanawake, bingwa mara 2 wa dunia Catherine Ndereba pia wsa Kenya, atumai kutoroka na taji la wanawake.

Katika Bundesliga,Wolfburg,viongozi wa Ligi wanarudi uwanjani wakiwa na uongozi wa pointi 3 mbele ya mabingwa Bayern Munich na Hamburg.Wakitamba tena kesho Jumapili mbele ya Energie Cottbus, sio tu watatanua mwanya wao kileleni bali watawka rekodi ya kutoshindwa mapambano 11 msimu mmoja-rekodi iliowekwa na Borussia Moenchengladbach, 1987.Wakisonga mbele na kushinda mapambano 5 yajayo, wataipiku Bayern Munich ilioshinda mapambano 15 msimu wa 2005.Munich ina miadi leo na Schalke wakati Hamburg inacheza na Borussia Dortmund.Stuttgart inapambana na Frankfurt wakati FC Cologne iko Hannover.

Premier League-ligi ya uingereza inarudi uwanjani huku mabingwa Manchester united ikiwa na miadi leo na Tottenham Hotspur.Chelsea wanapambana na West ham United huku Liverpool ikitazamia kutamba mbele ya Hull City.

Kombe la Shirikisho la dimba la Ujerumani: DFB Pokale:Kati ya wiki hii, timu 4 zilipambana katika nusu-finali ya Kombe hilo:Kwanza walicheza Bayer Leverkusen na Mainz na siku ya pili yake ikawa zamu ya majirani 2 wa kaskazini:Hamburg na Bremen, timu 2 zitakazokutana pia katika nusu-finali ya Kombe la ulaya la UEFA:

Baada ya Liverkusen kuzima vishindo vya Mainz katika kipindi cha kurefushwa mchezo na kuitoa kwa mabao 4:1, Hamburg na Bremen ziliamua uhasama wao kufuatia changamoto za mikwaju ya penalty. Kipa wa bremen Tim Wiese alikua shujaa wao siku hiyo.kwani alizuwia mikwaju 3 ya penalty ya Hamburg.Kwa ushindi wa mabao 3:1,Bremen imeekewana miadi na Leverkusen hapo Mei 30 kwa finali ya Kombe hilo .

Hamburgh ina nafasi nyengine ya kuilipizia kisasi Bremen kwa kuitoa nje ya fina,li ya mei 30 katika uwanja wa olimpik wa Berlin.Timu 2 za Ujerumani na 2 za Ukraine zinacheza nusu-finali ya Kombe la ulaya la UEFA.Bremen imepata moyo kwani, baada ya kuanza vibaya msimu huu wa Bundesliga, ushindi dhidi ya Hamburg umeitia moyo kushinda mpambano wao ujao.

Awali,Hamburg ililenga kutwaa mataji 3 msimu huu ,lakini baada ya kupokonywa nafasi ya finali ya DFB Pokale,ina nafasi 2 kufuta madhambi ya juzi.Kutamba leo katika Bundesliga na kuitoa Bremen nje ya Kombe la UEFA.Yote mawili si kazi rahisi.

Kesho ni zamu tena ya London marathon na majogoo wa Kenya wamekuwa wakiwika mara kwa mara.Martin Lel alitoroka na usindi mwaka jana na licha ya maumivu ya paja aliopata hivi majuzi, anatumai kama mwenzake upande wa wanawake Catherine Ndereba wataondoka na ushindi:

Mkenya Martin Lel ,ametamba katika m,bio nyingi za marathon ulimwenguni na ndie anaetetea taji la London marathon hapo kesho.Shaka shaka za mwisho iwapo angeingia mitaani London kesho ziliondoshwa na waandazi wa mashindano hayo.Kwani, bingwa huyo alikuwa na maumivu pajani na sasa inafahamika ni fit tena .Lel akiwa na umri wa miaka 30,alikaguliwa afya yake na amekutikana fit .Wakenya wengine watampa pia changamoto ,kwani kila mmoja anataka kurejea Nairobi na zawadi ya ushindi wa London Marathon.

Hali ni sawa na hiyo upande wa wanawake:

Bingwa wa olimpik upande huo ni Constantina Data na licha ya umri wake wa miaka 39 anajaraibu kwa mara ya 9 kutamba katika London marathon.Mara 8 zilizopita alitoka mikono mitupu.lakini ni yeye aliempiku mkemnya Catherine Ndereba huko Beijing mwaka jana ili kutawazwa bingwa wa Olimpik.

Hasimu yake mkubwa kesho atakuwa mkenya Catherine Ndereba, bingwa mara mbili wa dunia na makamo-bingwa wa olimpik. Sio tu Ndereba atataka kułipiza kisasi cha kushindwa Beijing, bali angependa binafsi kurudi Nairobi na taji la London marathon.Akiwa na umri wa miaka 36, ana kasi zaidi kuliko Constantina Dita.

Washindi upande wa wanaume na wanawake, watanyakua kitita cha dala 55.000 kila upande .Kuna kitita cha dala 125.000 kwa kuweka tu rekodi ya dunia ambayo imewekwa mjini Berlin na mkongwe wa Ethiopia,Haile-Gebreselassie.

Bingwa wa rekodi ya dunia, Irina Mikitenko, alinyakua kitita kama hicho alipoweka rekodi ya dunia huko Berlin kwa muda wake wa masaa 2 na dakika 19 na sek.19.

Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 36, aliekosa kushiriki mbio za Olimpik za Beijing mwaka jana, anadai pesa hazikubadili mtindo wa maisha yake.Mikitenko amekuwa akijiandaa kwa mbio za kesho na kwa ushindi wake katika mbio za km 10 huko Paderborn,Ujerumani jumapili ya Pasaka, ametoa salamu tangu kwa Constantina Dita hata kwa Catherine Ndereba,wachunge kesho katika London marathon.

Mwandishi: Ramadhan Ali

Mhariri: Othman, Miraji

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com