Michezo wiki hii | Michezo | DW | 21.11.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Michezo wiki hii

Hoffenhein yaumana na FC Cologne katika Bundesliga. Kura ya Conf.Cup mjini Johannesberg.

Luca Toni-jogoo la B.Munich.

Luca Toni-jogoo la B.Munich.

Kura inapigwa jumamosi hii mjini Johannesberg kuamua jinsi timu 8 zitakavyoania Kombe la mashirikisho-Confederations Cup- linalofungua Juni ijayo 2009 mlango kwa kombe la Dunia la FIFA -la kwanza barani Afrika 2010.

Baada ya Al Ahly ya Misri, kutawazwa mabingwa wa kombe la klabu bingwa wiki iliopita,ni zamu ya timu 2 za Tunisia CS Sfaxien na Etoile du Sahel kuamua wapi jumamosi hii kombe la Shirikisho (CAF) linaelekea.

Katika changamoto za Bundeliga -Hoffenheim iliopo kileleni inaumana na FC Cologne wakati Leverkusen i iko uwanjani na Bielefeld.

Tuanze na kura ya jioni hii ya Kombe litakalofungua pazia kwa kombe lijalo la dunia inayopigwa Johannesberg: Erica Ponda anasimulia:

Kombe la mashirikisho au Confederations Cup litachezwa miezi 7 hivi kutoka sasa kuanzia Juni 14-28, 2009.

Katika kura ya leo, Bafana Bafana au Afrika kusini imewekwa kandika kundi A lakini kama mojawapo ya timu 4 zinazoongoza makundi hayo:Hivyo ama itakumbana na mabingwa wa dunia Itali au mabingwa wa Ulaya Spian lakini Bafana Bafana haiwezi kuangukia kundi moja na Brazil. Wapinzani wake 2 wengine watatokana na Iraq,New Zealand na Marekani.

Kundi jengine litaingiza Misri,mabingwa wa afrika,Brazil-mabingwa wa Amerika kusini na ama Itali au Spain na moja kati ya Irak,New Zealand au Marekani.

Kwa mashabiki wa Bafana Bafana ambao mapema mwaka huu walibidi kuvumilia kuona timu yao imepigwa kumbo ya kombe la Afrika la mataifa litakaloaniwa Angola ,kura ya leo itawapa matumaini kidogo kwavile Bafana Bafana watakua na nafasi alao ya kufikia nusu-finali.Mjumbe wa FIFA Nicolas Maingot amekanusha uvumi wote kwamba kura ya leo imeandaliwa hivyo kuipa nafuu Afrika kusini.

Timu inayoongoza juu kila kundi huamuliwa kwa muujibu wa ngazi ya FIFA.

Kinyanganyiro cha Confederations Cup daima huangaliwa ni kufungua pazia kwa kombe la Dunia ambalo mara hii hapo 2010 litakuwa la kwanza barani Afrika.

Kamati ya maandalio inadai kila kitu kitakuwa tayari wakati ukiwadia. Anatumai viwanja 4 vitakavyochezewa Kombe la mashirikisho na kombe la dunia vitakuwa pia tayari kwa wakati.

Kura ya leo inafanyika katika Ukumbi wa Sandton Convention Centre mjini Johannesberg ikiongozwa na Katibu mkuu wa FIFA Jarome Valcke.

Valcke atasaidiwa na warembo 8 wanaoania mwezi ujao taji la dunia la Miss world huko Afrika kusini, mashindano ambayo yatafanyika pia katika ukumbi wa Convention Centre hapo desemba 13.

"Kuandaa mashindano makubwa kama haya warembo wa dunia-Miss world- tena kwa mara ya pili kunabainisha uwezo wa Afrika Kusini kuandaa matokeo makubwa ya kimataifa."

Warembo hao wanaomsaidia leo katibu mkuu wa FIFA ni Miss Brazil-Tamara Almeida Silva, Misri Egypt-Sanaa Hamed,Miss Itali-Claudia Russo,Miss New Zealand Kahhurangi Taylor,Miss Afrika Kusini Tansey Coetzee,Miss Spian -Patricia Rodriguez Alonjo,Miss America Mercia Lindell pamoja na miss world wakati huu Zilin Zhang atakemuakilisha bingwa wa Asia-Iraq.

Ni kwa urembo kama huo ,kura ya leo inapigwa na mashabiki wa dimba wataonja utamu wa Kombe la shirikisho Juni, 14-28 ,2009-miezi 7 kutoka sasa.

Macho ya mashabiki wa Afrika yanakodolewa pia kombe jengine la Shirikisho ambalo bila ya shaka yoyote litabaki Afrika:Kombe la CAF ambalo finali yake inachezwa leo kati ya timu 2 za Tunisia kama vile Sitaji Kalyango anavyosimulia:

Ama Etoile du sahel au CS Sfaxien inaandika historia jioni hii kwa kuibuka klabu ya kwanza kulinyakua kombe hili la CAF mara 2 ikilia firimbi ya mwisho ya finali ya timu 2 za Tunisia.

Etoile du sahel kidogo ina nafuu baada ya kutoka sare SC Sfaxien nyumbani ya 0:0 wiki mbili zilizopita.Hii ilikomesha kushinda mara 13 mfululizo nyumbani kwa Sfaxien .

Kocha wa Sfaxien Ghazi Ghrairi anabakia na matumaini makubwa ya kutamba na kutoroka na kombe hili jioni hii.

Etoile inabidi kucheza bila ya stadi wake wa kiungo Mohammed Ali Nafkha ambae bao lake la mkwaju wa penalty katika lango la Asante Kotoko nchini Ghana liliamua hatua hii iliofika timu hii.

Mbali na mastadi kadhaa wa timu ya taifa ya Tunisia,kuna wachezaji wengi maarufu wa timu nyengine za kiafrika katika finali ya leo kama vile Ivory Coast,Nigeria na Ghana. Mnigeria Emeka Opara ni mtiaji mashuhuri wa magoli wa wetoile katika kombe hili.Mwaka huu pekee alipachika mabao 3.Mghana Sadat Bukari,Mguinea Mohammed Sacko na mzambia Fwayo tembo ndio majogoo wanaotazamiwa kuwika kwa etoile du Sahedl,klabu pekee ya Afrika jkutwaa kila kombe la CAF.

Sfaxien wanajivunia waghana akina Opoku,mguinea-Naby Soumah na muivory Coast Balise Kouassi na Basisila Lusadisu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya kongo.

Kwa ufupi finali ya kombe la CAF jioni hii si ngoma ya kuchezwa na watuinisia pekee.

BUNDESLIGA:

Viongozi wa Bundesliga jioni hii Hoffenheim na Leverkusen wote wameingia uwanjani:

Hoffenheim inapambana wakati huu na FC Cologne ,mjini Cologne kulipiza kisasi kwa kulazwa mara mbili na Cologne,msimu uliopita pale timu hizo 2 zilipokuwa daraja ya pili.Wenyeji waliacha pointi 3 jumapili iliopita huko Bremen na hawamudu kuacha nyengine 3 ziondoke kwenda Hoffenheim. Hoffenheim lakini nayo haitaki kupoteza usukani wa Bundesliga ilionao pamoja na bayer Leverkusen inayocheza na Armenia Bielfeld.

Kwahivyo, vishindo wakati huu mjini Cologne ni vikubwa mno,kwani Hoffenheim imemsangaza kila mmoja msimu huu.

Viongozi wa Bundesliga Bayer Leverkusen kama Hoffemnheim hawana mteremko .Kwani Bielefeld imekuwa ikiitoa sana jasho Leverkusen na katika changamoto zao 7 zilizopita, Leverkusen imeshinda mara moja tu.

Mara ya mwisho Leverkuen kutamba nyunbani mwa Armenia Bielefeld, ilikua 1999 na hicho ni kitambo kirefu.

Mabingwa Bayern Munich walioteleza mwishoni mwa wiki ilopita walipoongoza kwa mabao 2 na halafu kutoka sare 2:2 na Borussia Dortmund wanacheza na Energie Cottbus.

B.Munich lazima itambe leo kwani mechi 2 zinazofuata inakumbana na timu 2 za kileleni-Bayer Leverkusen na halafu Hoffenheim.

katika mapambano mengine jioni hii,Hamburg wanaikaribisha nyumbani Bremen katika zahama ya timu mbili za kaskazini. Bremen ilianza vibaya sana msimu huu lakini walishindw amara 1 tu na hamburg katika mapambano yao 10. Schalke inacheza na B.Moenchengladbach wakati Wolfsburg inakumbana na Stuttgart.Eintracht Frankfurt inachuana na Hannover wakati Bochum inakamilisha kalenda ya mashindano ya mwishoni mwa wiki hii kwa kuikaribisha nyumbani Hertha Berlin.

Tumalizie Premier League-Ligi ya Uingereza na kinyanganyiro cha kubakia kileleni kati ya Chelsea na Liverpool: Chelsea ipo pointi 8 usoni kabisa mwa mahasimu wao wakubwa mabingwa Manchester united walioangukia nafasi ya 3.Maaduni zao leo ni Newcastle inayopepesuka wakati Liverpool wana miadi nyumbani Anfield na Fulhalm. Chelsea wameshinda mechi 7 kati ya 7 walizocheza ugenini,lakini nyumbani walipepesuka kidogo. Chelsea itabidi kucheza bila jogolo lao Corte dIViore, Didier Drogba ,lakini simba wao mpya mfaransa Nicolas Anelika yutayari kunguruma tena.

Liverpool iliopoteza pointi 2 tu nyumbani msimu huu,inapambana na Fulhalm na ikiwa na miadi siku zijazo na West Ham United,Blackburn Rovers na Hull City,mashabiki wa Liverpool wanahisi wameshatia kikapuni pointi 12., Manchester pengine wanabidi leo kucheza bila ya Mbulgaria Berbatov alieumia kidogo kati ya wiki pale alipoichezea timu ya Taifa ya Bulgaria .Hata Rio Ferdinand bado si fit.Maadui zao Manchester United ni Aston villa.