Michezo wiki hii | Michezo | DW | 25.07.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Michezo wiki hii

China yajiandaa kuanza kwa Olimpik na kutamba.Finali ya kombe la klabu bingwa kanda ya Afrika mashariki na kati mjini Dar-es-salaam.

Michezo ya olimpik ya Beijing ikinyemelea,wenyeji China,wametangaza wiki hii kikosi chao cha wanariadha 639,kikosi kikubwa zaidi kuliko ilivyotarajiwa-

Je,Nigeria itarudi tena na medali ya dhahabu kutoka dimba la olimpik kama ilivyofanya Atlanta,1996 ?

Na jumapili hii ni finali ya kombe la klabu bingwa kanda ya Afrika mashariki-nani watatawazwa mabingwa ?

►◄

Bunduki italia August 8, kuanzisha michezo ya olimpik ya Beijing 2008 na wakati wanariadha wa Afrika wanaendelea kujinoa kuonesha ubingwa wao, wenyeji wao China, nao wamedhamiria makubwa mara hii.

China, inataka kuibuka kileleni mwa orodha ya medali pale michezo hii itakapofungwa August 24 na wanariadha wake kwa waume, wakifunga virago kurudi nyumbani kujiandaa kwa michezo ya 2012 mjini London,Uingereza.

China imetangaza kikosi cha wanariadha 639-kikubwa zaidi kuliko ilivyotazamiwa.Na China haitaki huo kuwa wingi wa garasa bali uwe wa turufu.Wanariadha wa China watagombea medali za dhahabu,fedha na shaba katika michezo 28 na umri wa wanariadha wake ni wa wastani wa miaka 24.4.

Katika kikosi hicho wanariadha 469 wanashiriki kwa mara ya kwanza katika olimpik wakipepea bendera ya china.Wengine 165 walishiriki katika michezo iliopita mjini Athens,Ugiriki 2004. kikosi jumla cha china pamoja na viongozi wake na walimu ni 1,099.

Wanariadha 37 ni kutoka mashindano ya 2000 mjini Sydney, Australia n a ni watatutu walioshiriki katika michezo ya Atlanta,georgia,Marekani, 1996.

China kwahivyo, inataka kutamba nyumbani kwa ari mpya na nguvu mpya.

China utakumbuka ilipeleka kikosi cha wanariadha 407 katika michezo iliopita ya Athens,Ugiriki na 311 katika michezo ya Sydney, 2000. Mabingwa wengi wakitazamia China ingeshiriki katika michezo hii na kikosi cha wanariadha 570,lakini kimepindukia kima hicho.

Mahasimu wao Marekani imetangaza kikosi cha wanariadha 596 wakati dola jengine kubwa la riadha Russia, inapanga kutuma Beijing jumla ya wanariadha 470.

Katika michezo iliopita ya Olimpik mjini Athens, ugiriki 2004, china ilinyakua jumla ya medali za dhahabu 32-medali 4 kasoro zile za marekani na 5 zaidi kuliko Russia.

Mara hii inakisiwa kuwa China yaweza ikatwaa kati ya medali 41 hadi 46 za dhahabu na hivyo kuipita Marekani.

Mapema wiki hii, rais Hu Jintao wa china, aliwataka wanariadha wa China kushinda ili kulitukuza jina la China pale alipotembelea vituo vya michezo vya Tennis,Gymnastics na kuogolea.

Kwa ufupi, China imejiwinda sio tu kuibuka dola kuu jipya la kiuchumi bali pia la kispoti.

Jina maarufu katika medani ya riadha ulimwenguni kutoka china, ni bingwa wake wa olimpik katika mbio za mita 110 Liu Xiang,stadi wa mpira wa kikapu wa NBA Yao ming na stadi wa kike wa kupigambizi katika hodhi la kuogolea Guo Jingjiang na wote hawa watakuwa uwanjani mjini Beijing.

China ina nafuu moja -kama mwenyeji wa olimpik- haikubidi kufuzu kushiriki katika dimba la olimpik.kwahivyo, mlango ni wazi kushiriki moja kwa moja.

Mbali na Corte d'iviore-tembo wa Ivory Coast, Nigeria ni mojawapo ya timu 4 za dimba za Afrika zinazotaka kurudi Afrika na medali ya dhahabu kama ilivyofanya Nigeria na Kamerun hapo kabla.

Kocha wa Nigeria Samson Siasia, ni mtu anaependa nidhamu kabisa na havumilii utovu wa adhabu.Siasia amewaonya wachezaji wake wa timu ya olimpik kukata nywele zao fupi na kuvaa mavazi yanayostahiki kwa michezo ya BSiasia alidai wachezaji wa Nigeria wanapitisha muda mwingi kwa staili za nyewele zao -muda ambao aanahisi ungetumika bora zaidi kujiandaa kwa dimba la olimpik.

Nigeria, iliibuka mabingwa wa olimpik 1996 huko Atlanta ilipocheza na mastadi kama Nwanko Kanu.katika dimba la olimpik ambamo Brazil pia inashiriki, Nigeria safari hii iko kundi moja na Holland,Japan na Marekani kwa changamoto za duru ya kwanza.

Nigeria inatazamiwa kuwa na ngome imara kama vile beki wake mshahara Taye Taiwo , mwenye mikwaju mikali ya freekick.Kwavile, John Obi Mikel, amekorofishana na kocha Siasia, Taiwo anaefananaishwa kwa mikwaju yake mikali na Roberto Carlos wa Brazil anajaza pengo lake.

Akiwa miezi 3 tu chini ya umri unaotakiwa -miaka 23 kwa olimpik- Taiwo aliichezea Nigeria katika ile timu iliomaliza wapili nyuma ya Argentina katika kombe la dunia löa vijana 2005.alitia mara mbili mabao wakati wa kombe lile la dunia na alichaguliwa mchezaji 3 bora kabisa.

Ugandan Revenue Authority, ilikua timu ya kwanza katika kinyan'ganyiro cha kombe la Kagame, kanda ya Afrika mashariki na kati kukata tiketi yake kwa finali ya jumapili ya Kombe hilo kabla ya Young African kutimuana na wakenya Tusker hapo alhamisi.

Mashabiki wa klabu 2 za Tanzania-simba na younga walitamani kuona kesho timu zao 2 zikicheza finali hii baada ya Tanzania kuwakilishwa na jumla ya timu 3-moja ikiwa Miembeni ya Zanzibar.

Miembeni ilizusha msangao pale ilipowazaba mabingwa APR wa Ruanda mabao 3-2,lakini baadae ikadhihirika kama wenzao simba ni vishindo vya darini vilivyoishia sakafuni.

Simba hasa iliwekewa matumaini lakini baada ya kumudu sare hadi dakika ya 90 ya mchezo, Waganda waliitia kitanzi simba mara tu uliporefushwa mchezo na kuwafunga bao 1:0.vishindo vya simba kunguruma na kufuta bao hilo la Revenue Authority, hazikufua dafu na simba akalala mzizima.

Wapi basi kombe kesho litaelekea ,tusiandike mate na wino upo.

Msichana wa Brazil-stadi wa dimba anaevaa namba 10- MARTA, ni mchezaji pekee wa kike aliepewa heshima Brazil ya kuacha nyayo zake katika safu ya mastadi mashuhuri mbele ya uwanja mkuu wa Rio de Jeneiro wa Maracana Stadium.

Marata alialikwa kujiunga na mastadi wakubwa akina pele,Garrincha,Jairzhino,Romario,Zico,Rivelino na franz Beckenbauer.Hii yaonesha jinsi anavyoheshimiwa msichana huyu mwenye umri wa miaka 22-shujaa wa dimba nchini Brazil.

Marta alitia mabao 7 kuisaidia Brazil kuwasili finali ya kwanza kwa Brazil ya kombe la dunia la wanawake mwaka jana kabla kulazwa na Ujerumani na kunyimwa kombe.

Pia marta alichangia mno kuisukuma mbele Brazil katika dimba la Pan-American Games mjini Rio de Janeiro.

Miaka 4 iliopita, Marta alikua katika ile timu ya Brazil ilioshinda medali ya fedha katika michezo ya olimpik ya Athens.Mara hii,Marta anatumai kutamba tena na kupiga hata hatua moja zaidi kwa kutwaa medali ya dhahabu ya dimba la olimpik kwa wasichana wa Brazil huko Beijing.

Akiwa amekulia katika mji mdogo wa Dois Riachos h,kaskazini-mashariki mwa mkoa wa Sertao,kaskazini-mashariki mwa Brazil, Marta alianzia kupiga teke mpira na kaka zake alipokua mtoto.

Akiwa na umri wa miaka 16 alijiunga na klabu ya Vasco Dagama na baada ya kupita miaka 2 alianza kucheza katika daraja ya kimataifa kwa timu za chipukizi.

Mashabiki wengi wanasema sasa Marta amechangia zaidi kukuza dimba la akina dada kuliko shirikisho zima la kabumbu la Brazil ambalo halikuandaa mashindano ya dimba ya kitaifa nchini Brazil tangu 2001.Marta akicheza dimba Sweden tangu alipotimiza umri wa miaka 18.