Michezo wiki hii | Michezo | DW | 13.06.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Michezo wiki hii

Kombe la Ulaya la mataifa linaendelea .

Kombe la Ulaya la mataifa linaendelea leo kwa mabingwa watetezi-Ugiriki wakipambana na Russia na changamoto ya pili ni kati ya Sweden na Spian.

Kesho jumapili,wenyeji Uswisi waliokwishapigwa kumbo nje ya kombe hili wana miadi na Ronaldo wa Ureno.

Pia nje ya kom,be la Ulaya,kinyan'ganyiro cha kuania tiketi za kombe lijalo la dunia kanda ya Afrika,Amerika ya kusini na ya kati kinaendelea.

Baadae tutawafungulia pazia la michezo 28 ya Olimpik ya Beijing,August 8 huku wanariadha wake kwa waume wakijinoa kuteremka Beijing.

Kufuatia changamoto za jana jioni za kuamua hatima ya mabingwawa dunia-Itali kati yake na rumania na ya pili ya kuamua hati ya makamo-bingwa wa dunia Ufaransa kati yake na Holland, mabingwa watetezi wa kombe hili-Ugiriki wanateremka uwanjani jioni hii wakipania wasivuliwe taji na mapema na kurudi Ugiriki.Mahasimu wao ni Russia -iliolazwa na spian mabao 4-1 katika duru ya kwanza.

Jumapili mjini Basel,wenyeji Uswisi ambao wameshayaaga mashindano haya wanaagwa kabisa na Ureno inayotamba na Christiano Ronalndo.

Uturuki iliowasangaza dakika ya mwisho waswisi na kuwatoa kwa mabao 2:1 hapo majuzi wanatoana jasho na Jamhuri ya Czech.

Jumatatu keshokutwa itaamuliwa hatima ya Ujerumani-mabingwa mara 3 wa ulaya.Wajerumani walichezeshwa tena juzi alhamisi kindumbwe-ndumbwe na Croatia kama ilivyokua katika kombe la dunia 1998 nchini Ufaransa.

Walizabwa mabao 2:1.

Kocha wa Ujerumani Joachim Löew alieleza hivi kwanini timu yake ilioshindwa kufua dafu mbele ya Croatia:

Kushindwa Ujerumani mabao 2:1 na Croatia kuliwahuzunisha mno mashabiki wao baada ya Ujerumani kuanza kwa vishindo jumapili iliopita walipoizaba Poland mabao 2:0.Kocha Löew anaamini hatahivyo, kwamba Ujerumani itarudi kutamba.Alisema,

"Mnamo miaka 2 au 3 iliopita ,timu ya Ujerumani daima ikifufuka kutoka kaburini."

Ujerumani inatazamiwa kwahivyo jumatatu kufufuka na kuizika Austria ili kuchukua nafasi ya pili kutoka kundi B kwa duru ijayo ya robo-finali.

Ujerumani itamtegemea tena Lukas Podolski alietia juzi bao lake la 3 katika mashindano haya.

Ujerumani itahitaji alao kutoka sare na Austria mjini Vienna, nyumbani mwa Austria na wachezaji wake akina Ballack,Miroslav Klose na Podolski wanaelewa watapaswa kucheza kwa kasi na ari zaidi kuliko juzi dhidi ya Croatia.

Podolski -mchezaji pekee wa usoni wa Ujerumani alienguruma hadi sasa kwa mabao yake 3,alisema itakua ni jukumu la kila mchezaji kuonesha anamudi zahama na vishindo mjini Vienna, zizi la waustria jumatatu.Akaongeza,

"ikiwa hatutamudu ,basi tufunge virago kurudi nyumbani."

Mashabiki wao hawatawakaribisha na wanajua hayo.Kwahivyo, itazamie timu nyengine ya Ujerumani jumatatu hii:

►◄

Tumalizie michezo ijayo ya olimpik ya Beijing itakayofunguliwa rasmi hapo August 8:

Jumla ya michezo 28 iko katika kalenda ya michezo ijayo ya Olimpik ya beijing itakayoanza August 8 na kumalizika August 24.Kiasi cha wanariadha 10,500 kutoka nchi 201 miongoni mwao wale wa Afrika mashariki na hasa Kenya na Ethiopia-wanatazamiwa kutia fora.

Ikiwa ni mwenyeji wa michezo hii, China imehakikishiwa kushiriki katika kila mchezo kati ya hiyo 28.

Wakati kinyan'ganyiro cha kuania tiketi za Olimpik kimemalizika,bado nchi zinazoshiriki hazikukamilisha kuteua waakilishi wao katika michezo hiyo.

Kikawaida, baadhi ya michezo inafungua milango kwa wanariadha waliofikia vipimo maalumu wakati mengine kama vile kabumbu ni kwa timu za nchi .

Afrika inatazamiwa kutia fora katika medani ya riadha-Athletics:

Hapa kutakua na mashindano 24 kwa wanaume na 23 kwa wanawake na hii ndio idadi kubwa kabisa kuliko ilivyo katika michezo mengine ya Olimpik.Kiasi cha wanariadha 2000 kati yao wanaume 1,1000 watashiriki beijing.Kabla lakini wanatakiwa kufikia vipimo vilivyowekwa-qalifying standards.Ni vipimo vilivyowekwa na shirikisho la riadha ulimwenguni-IAAF.

Kwa mashindano mbali na mbio za marathon, vipimo vya kuweza kushiriki vilipaswa kufikiwa kati ya januari mosi,mwaka jana na Julai 23 mwaka huu.Kila nchi mlango wazi kuingiza mashindanoni hadi wanariadha 3 katika kila mchezo ikiwa tu wamefikia vipimo vilivyowekwa.

Baadhi ya dola kuu za riadha kama marekani ,huchagua waakilishi wao kupitia mashindano maalumu ya kitaifa-national Trials.Kikawaida 3 wa kwanza huchaguliwa kuwakilisha Marekani.Nchi nyengine hucchaguwa wale walioweka muda bora mnamo msimu wa mwaka huu wa riadha 2008.

Kuna mashindano ya timu kama vile kabumbu na mpira wa kikapu-basketball.Katika Basketball, timu 12 zashiriki upande wa wanaume na wanawake:

Angola inawakilisha afrika tangu upande wa wanaume na hata ule wa akina mama.

Michezo mengine katika ajenda ya michezo 28 ya olimpik ni pamoja na Baseball,Badminton na kuogolea:

Afrika imewahi kutoroka na medali za dhahabu katika hodhi la kuogolea lakini pia hoki.Wasichana wa Afrika kusini na Zimbabwe wamewahi kutamba.

Afrika pia imewahi kutawazwa mabingwa wa olimpik katika dimba-Nigeria imewahi kuwika.

Riadha lakini,inasalia moyo wa michezo hii na ndipo ulipo msisimko.Ni hapa ambapo wanariadha wa Afrika wake kwa waume wanatazamiwa kupepea bendera za bara la afrika wakifuata nyayo za akina Abebe Bikila wa Ethiopia, ambae akikimbia miguu chini alinyakua medali ya kwanza ya dhahabu kwa afrika katika mbio za marathon,mjini Roma, 1960.

Mabingwa wengine mashuhuri wa Olimpik waliemfuata ni pamoja na mkenya kip keino,waliemuita "mfalme wa mbio barani Afrika".

1972 Uganda iliandika jina lake katika ramani ya washindi wa olimpik pale marehemu John Akii-bua alipowika katika mbio za mita 400 kuruka viunzi wakati wa michezo wa olimpik ya Munich.

Miaka ya 1980 alitamba Miruz Yiftre wa Ethiopia,mshindi wa medali 2 za dhahabu katika michezo ya Moscow,1980.

Msichana wa kwanza kunyakua medali ya dhahabu ya Olimpik kwa afrika na kwa ulimwengu wa kiarabu alikua mmorocco-Hassiba Boulmerika.Alishinda mbio za mita 400 kuruka viunzi wanawake huko Los Angeles, 1984.

Leo wasichana wa Kenya na Ethiopia wako usoni kabisa na ndio wanaotazamiwa kutamba huko Beijing kuanzia mita 800 hadi marathon.

Afrika kwa kweli, inasubiri kwa hamu kuu bunduki kulia hapo August 8 ili kutamba zaidi kuliko ilivyofanya miaka 4 iliopita wakati wa michezo ya Athens, Ugiriki 2004.