Michezo Mwishoni mwa Wiki | Michezo | DW | 30.08.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Michezo Mwishoni mwa Wiki

Bundesliga ya yaanza kwa kishindo

Kaiserslauten yaichapa B.Munich2:0

Kaiserslauten yaichapa B.Munich2:0

-Bundesliga, imeanza kwa kishindo ,kwani, tangu mabingwa Bayern Munich, hata makamo-bingwa Schalke na Bayer Leverkusen,zimekiona kilichomtoa kanga manyoya.

-Daniel Rudisha wa Kenya,avunja tena rekodi ya dunia ya masafa ya mita 800 -wiki tu baada ya kuiweka mjini Berlin.

-Na wakati Taifa Stars,timu ya taifa ya Tanzania, yafunga safari kesho kuelekea Algeria kwa kampeni ya Kombe la Afrika,ujumbe wa ZFA,ukiongozwa na waziri wa michezo Ali Juma Shamhuna, uko Uswisi,Makao Makuu ya FIFA kuomba uwanachama wa Zanzibar katika FIFA. Je, mara hii hodi hodi za ZFA zitaitikiwa ?

Kaiserslauten, timu iliopanda daraja ya kwanza msimu huu, iliwachezesha mabingwa Bayern Munich, kindumbwe-ndumbwe na kuwazaba mabao 2:0.

Baadae ikawa zamu ya Bayer Leverkusen,moja ya timu za kileleni kukandikwa mabao 6-3 na B.Moenchengladbach,licha ya kucheza na nahodha wao mpya Michael Ballack.

Ushindi wa Kaiserslauten, ijumaa iliopita dhidi ya mabingwa Bayern Munich,unakumbusha ushindi sawa na huo pale timu hii ilipotoka daraja ya pili na kutawazwa moja kwa moja mabingwa wa Bundesliga.Je, safari hii,Kaiserslauten ina azma kama hiyo ? Ushindi wa juzi wa mabao 2:0 dhidi ya Bayern Munich, unafuatia ule wa mabao 3:1 dhidi ya FC Cologne, Jumamosi iliotangulia.

Lango la Bayern Munich, lilifumaniwa tayari mnamo dakika ya 36 ya michezo kwa mkwaju maridadi wa Ivo Ilicevic na hazikupita sekunde 60 ,Kaiserslauten, ikapiga msumari wa pili katika jeneza la kocha van Gaal wa Bayern Munich.

Munich, ilidhibiti mchezo kipindi kikubwa, lakini Thomas Mueller,jogoo la Ujerumani katika kombe lililopita la dunia,lilikosa nafasi nzuri kabisa kutia bao.Hata wenzake akina Ivica Olic,Miroslav klose na Toni Kroos,hawakufua dafu katika lango la Kaiserslauten.Baadae, kocha wa Bayern Munich, mdachi,Luis van Gaal, alisema,

"Siwezi kuungama kwamba, tumeanza msimu wa ligi vibaya,kwani,tumecheza uzuri,isipokuwa hatua za mwisho langoni ,yaani pasi ya mwisho, haikuwa nzuri."

Schalke ,makamo bingwa, nao walikiona cha mtemakuni walipozabwa na timu nyengine chipukizi Hannover 96 mabao 2:1.Kocha wa Schalke,Felix Magath, ambae baada ya kuitawaza Wolfsburg,mabingwa mwaka juzi,ameajiriwa kuivalisha taji Schalke,alililieleza ,

"Pigo tuliopata Hamburg, linavumilika,kwani tukiwa timu inayoania mojawapo ya nafasi 5 bora,tunaweza kuvumilia kushindwa mara 1 ugenini, lakini , mbaya kushindwa na Hannover na kupoteza pointi 3 ambazo tungezihitaji mno siku zijazo."

Timu ya 3 ya kileleni mwa Bundesliga kuchezeshwa kindumbwe-ndumbwe, ilikuwa Bayer Leverkusen ikiongozwa na nahodha wake mpya Michael Ballack. Leverkusen ilichapwa mabao 6-3 na Borussia Moenchengladbach wakati Stuttgart, ilizikwa kwa mabao 3-1 na Borussia Dortmund.

Leverkusen, iliomaliza nafasi ya 4 msimu uliopita,ilimuajiri Ballack kutoka Chelsea, ili kuimarisha kikosi chake.Lakini, kikosi cha kocha Jupp Hynckes,hakikufua dafu na mwishoe, kikafedheheshwa kwa mabao 6-3.Hata nahodha Ballack alibidi kubadilishwa akapumzike.

Kocha Jupp Hynckes akasema,

"Leo hatukuwa na nidha katika ulinzi na hatujajiandaa vyema.Nahasa ukielewa jinsi Borussia ilivyo hatari kurejesha ghafula mashambulio leo, tumejionea hayo."

FC Cologne, ni miongoni mwa timu zilizoanza vibaya msimu huu,kwani baada ya pigo la kwanza nyumbani la mabao 3:1 ,mwishoni mwa wiki hii ilizabwa mabao 4:2 na Bremen.Ili kujiimarisha kwa changamoto zijazo kuzima vishindo vya kuteremshwa daraja ya pili,FC Cologne, imememuita kwa majaribio Jean-Batiste Mugiraneza,chipukizi kutoka Rwanda kumuangalia uchezaji wake.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 19,ataondoka kuichezea Rwanda mwishoni mwa wiki hii itakapo pambana na Ivory Coast katika kinyan'ganyiro cha Kombe la Afrika.Hatahivyo, kocha wa FC Cologne,Soldo, anadai licha ya kijana huyo ana usatdi wa dimba, bado Mugiraneza hajakomaa kuweza kuliokoa jahazi la FC Cologne lisizame.

Taifa Stars, inaondoka Dar-es-salaam, kesho kwa safari ya Algiers, kuanza kampeni ya kuania tiketi yake ya Kombe la Afrika la mataifa ijumaa hii itakapoumana na wenyeji Algeria.

Wakati lakini Taifa Stars,inaelekea Algiers, viongozi wa Shirikisho la dimba la Zanzibar ( ZFA) pamoja na waziri wa michezo Ali Juma Shamhuna,wako Geneva ,Uswisi,makao makuu ya FIFA kupiga tena hodi - hodi ili Zanzibar iwe mwanachama wa FIFA.

Mabingwa wa Ethiopia, Saint George wamemuajiri Guiseppe Dossena,stadi wa Itali ilipotwaa Kombe la dunia Ujerumani 2006 kuwa kocha wake mpya. Dossena amefunga mkataba wa miaka 2.

Tumalizie riadha na rekodi mpya ya dunia ya masafa ya mita 800 kutoka mkenya Daniel Rudisha hapo jana huko Rieti,Itali:Rudisha amevunja rekodi ya dunia mara ya pili kwa muda wa wiki moja pale alipotimka mbio na kuweka muda mpya wa dakika 1,41.01 sek. huko Rieti,Itali.

Ni Jumapili tu iliotangulia chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 21 alipoifuta rekodi ya mkenya mwenzake aliechukua uraia wa Denmark, Wilson Kipketer iliodumu miaka 13 mjini Berlin. Rudisha, aliekuwa bingwa wa dunia wa wanariadha chipukizi-junior,alipachika rekodi ya Afrika,alipoanza kutoa salamu zake kwa mahasimu .

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed