Michezo mwishoni mwa wiki: | Michezo | DW | 07.12.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Michezo mwishoni mwa wiki:

Baada ya kura ya timu 32 za Kombe la dunia 2010 ?

fifa 2010 logo

fifa 2010 logo

BAADA YA KURA YA KOMBE LA DUNIA 2010:

Baada ya kura ya Kombe lijalo la dunia Ijumaa usiku ,nani atatamba katika kundi la kufa-kupona la mabingwa mara kadhaa Brazil,Ivory Coast,Ureno na Korea ya kaskazini ?

Je, wenyeji Bafana Bafana au Afrika Kusini, wataaga na mapema Kombe lao la dunia waliloandaa wenyewe ?

Ujerumani, mabingwa mara 3 wa dunia, wameikaribisha vipi kura ya Ijumaa katika kundi D ?

Wakati Bayer Leverkusen, yateleza kidogo katika Bundesliga,Bayern Munich,yaonesha huenda ikatimiza ahadi yake ya kuparamia kileleni mwa Bubndsliga kabla ya x-masi.

Hali baada ya kura ya Ijumaa mjini Cape Town , ya timu 32 zitakazoania

Kombe lijalo la dunia,kuanzia ( Juni, 11-Julai,11, 2010 ): Wenyeji Afrika kusini, wameitikiaje kura ya Ijumaa iliowatumbukiza katika kundi jengine la kufa -kupona mbali nalile la Brazil,Ureno,Ivory Coast na Korea ya kaskazini ?

Afrika kusini, ilishangiria sherehe za kwanza kubwa kabla firimbi kulia kuanzisha dimba hapo Juni ,mwakani.Lakini, kitumbua chao kilitiwa mchanga kwa kuangukia Bafana Bafana-timu yao ya Taifa, kundi A pamoja na mabingwa 2 wa dunia-kwanza na Uruguay,mabingwa 1930 lilipoanzishwa Montevideo, na tena 1950 walipowapiku Brazil,mjini Rio de Jeneiro.

Tena Bafana Bafana wanapambana na Ufaransa,mabingwa wa dunia 1998 na makamo-bingwa hivi sasa.

Afrika kusini, itafungua Kombe la Dunia na Mexico kabla kukutana na Cristiano Ronaldo wa Ureno na Thierry Henry wa Ufaransa.Mpambano na Mexico, utaamua hatima yao katika mapambano yajayo ama sihivyo, itakua timu ya kwanza ilioandaa Kombe la dunia kuaga na mapema duru ya kwanza.Hatahivyo, Bafana Bafana inadai kuwa, halitawaachia majogoo hao wa shamba kuwika mjini Johannesberg.

Kocha wao Mbrazil, Carlos Alberto Parreira, alisema baada ya kura hiyo, " Hili ni kundi pekee lenye mabingwa 2 wa zamani wa Kombe la dunia .Halitutishi,isipikuwa ni changamoto kwetu."

Timu kali kabisa kati ya 6 za Afrika-Tembo wa Ivory Coast, kwa mara nyengine tena, wameangukia kundi la kufa-kupona pamoja na

mabingwa mara 5 wa dunia -Brazil,Ureno na Korea ya kaskazini.

Katika kombe lililopita la dunia 2006 hapa Ujerumani, Ivory Coast iliangukia kundi gumu kama hilo.lilijumuisha Argentina,Holland na Serbia. Je, hatima ya 2006 ya kutolewa Ivory Coast duru ya kwanza,itawafika tena mara hii licha ya jogoo lao Didier Drogba ? Mpambano kati ya Brazil na Ivory Coast utakua wa kukata na shoka .

KUNDI LA 4:

Ujerumani huenda ikapatwa na shida kuzima vishindo vya Australia na hasa kwavile, Ujerumani, ina desturi ya kuanza pole pole Kombe la dunia na kutia kasi duru ya pili:

Mbali na Australia, Ujerumani ina miadi na Serbia na mwishoe, na Black Stars-Ghana, timu pekee ya Afrika iliocheza duru ya pili ya Kombe lililopita la dunia nchini Ujerumani na mwishoe, ikatolewa nje na Brazil.Kocha wa Ujerumani Joachim Loew, alisema baada ya kura ya ijumaa: "Nina heshima kubwa mbele ya Serbia.Waliishinda Ufaransa na walishinda bila taabau kundi lao la kufuzu kwa Kombe la dunia."

Kabla ya kura ya majuzi, Ujerumani, nusra ikione kilichomtoa kanga manyoya ilipomudu dakika za kufidia kutoka sare na Ivory Coast 2:2 mjini Gelsenkirchen.Waivory kwahivyo, wametoa tayari salamu zao kwa wajerumani.

Bundesliga na Premier League:

Viongozi wa Bundesliga-Bayer Leverkusen, waliteleza jumamosi walipomudu sare tu ya 0:0 na Hannover 96 lakini wamebakisha rekodi yao ya kutofungwa tangu mechi 15 kupita.Wakiwa na pointi 31,Leverkusen wanakabiliwa lakini na hatari ya kupoteza usukani kwa mabingwa mara kadhaa Bayern Munich ambao waliishinda Borussia Mönchengladbach kwa mabao 2:1 na sasa wako karibu sana kileleni wakiwa nafasi ya 3 nyuma ya Schalke. Kocha wa Leverkusen,Jupp Hynckes alisema hivi baada ya kutoka suluhu na Hannover:

"Ulikua mchezo wa viroja vingi,nafasi nyingi za kutia magoli na ingawa matokeo ni 0:0 ilistahiki hivyo.Yabidi hatahivyo, kuungama Hannover, walikuwa kidogo bora kushinda sisi."

Werder Bremen, iliopo nafasi ya pili ya ngazi ya Ligi,ilishindwa kutamba mbele ya FC Cologne na kuondoka pia suluhu 0:0.Bremen sasa iko pointi 28 sawa na Schalke .Schalke iliitandika berlin 2:0 na kuizamisha zaidi mkiani mwa Ligi. Stuttgart imemtimua mwishoe kocha wake Markus Barbbel baada ya kumudu sare tu bao1:1 na Freiburg.

Ama, katika Premier League,Ligi ya Uingereza, Chelsea, imeambiwa "kila kitu kina mwisho wake " na huwezi kushinda kila siku.

Chelsea, imezabwa mabao 2-1 na Manchester Ciity.Mtogo Emmanuel Adebayor,alifuta madhambi ya kutia bao mwenyewe katika lango lake na kusawazisha langoni mwa Chelsea. Hii imerudisha mwanya wa pointi 2 kati ya Chelsea na Manchester United ilioizaba West Ham mabao 4:0.Arsenal imeparamia kileleni hadi nafasi ya 3 nyuma ya Manu.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ RTRE/AFPE

Mhariri:Abdul-Rahman