Michezo mwishoni mwa wiki | Michezo | DW | 30.11.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Michezo mwishoni mwa wiki

Bayer Leverkusen kileleni mwa Bundesliga.

Stefan Kiessling-atia mabao 3 pekee

Stefan Kiessling-atia mabao 3 pekee

MICHEZO MWISHONI MWA WIKI:

Kinyan'ganyiro cha Kombe la CECAFA-Challenge Cup-Kombe la Afrika Mashariki na Kati kinaendelea mjini Nairobi na Mumiyas huku timu 2 za Tanzania zikianza kwa matokeo tofauti:Tanzania-bara imeteleza kwa mabao 2:0 mbele ya Waganda wakati Zanzibar imetamba kwa mabao 4:0 mbele ya Ruanda.Wenyeji "Harambee Stars " wameteleza mbele ya Zambia.Miji 5 ya Afrika kusini, imechaguliwa kuchezewa duru za kwanza za Kombe lijalo la dunia 2010.

Wakati katika Bundesliga, Bayer Leverkusen, inaendelea kutamba kileleni ,katika Premier League,Chelsea baada ya mabao 2 ya Didier Drogba katika lango la Arsenal, yaendelea kuongoza Premier League, ikifuatwa nyuma na Manchester Katika La Liga-Ligi ya Spain,bao la Mswede, Zlatan Ibrahimovic ,laipa ushindi FC Barcelona dhidi ya mahasimu wao Real Madrid.

CHALLENGE CUP:

Harambee Stars ,wenyeji wa Challenge Cup-Kombe la CECAFA-kanda ya Afrika Mashariki na Kati walikandikwa mabao 2:0 na Chipolopolo Zambia,lakini wanadai kutangulia si kufika.Watarudi kutamba.

Timu 2 za Tanzania,zimeanza tofauti kinyan'ganyiro hicho cha Kombe la Challenge.Wakati Zanzibar Heroes,ilitamba mbele ya Amavubi-Ruanda kwa mabao 4:0 ,Taifa Stars iliteleza mbele ya Ugandan Cranes kwa mabao 2:0.Tanzania-bara sasa imefikiria mkakati mpya wa kuimarisha kikosi cha taifa kupitia timu za vijana.Viongozi wa dimba sasa wameanza kutambua kwamba, ukitaka kujua nguvu za timu ya Taifa,angalia zile nguvu za chipukizi wake- aripoti George Njongopa, kutoka Dar-es-salaam .Kwahivyo, Ligi ya chipukizi imeanzishwa Tanzania.Tanzania sasa ina miadi na Ruanda katika mpambano wake wapili wa Challenge Cup.

DURU ZA KWANZA KOMBE LA DUNIA 2010:

Ijumaa hii ijayo, kura itapigwa huko Cape Town, Afrika Kusini, kuamua jinsi timu 32 zilizofuzu kwa Kombe lijalo la dunia, zitakavyo pambana katika makundi 8 ya timu 4.Mara hii, Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya kombe la dunia,itawakilishwa na timu 6: wenyeji Bafana Bafana,Ghana-Black Stars,Kamerun -Simba wa nyika, Nigeria-Super Eagles,Algeria na bila shaka Tembo wa Ivory Coast.

Sasa miji 5 imechaguliwa kwa duru za kwanza za Kombe hilo-nayo ni pamoja na Pretoria,Bloemfontein,Polokwane na Rustenburg.Jiji la Pretoria nyakati za usiku huweza likawa na baridi kali wakati wa kombe hilo la dunia linaloanza Juni 11-hadi finali Julai 11,2010.Rustenburg,hali ya hewa ni ya wastani,jua pia hutoka.Nelspruit ina hali ya joto.Viongozi wengi wa timu zilizofuzu kwa Kombe hilo la dunia ,wanafikiriwa kupanga kambi za mazowezi ya timu zao kandoni mwa jiji la Pretoria,Rustenburg,Bloemfontein na Johannesburg.

BUNDESLIGA NA PREMIER LEAGUE:

Mtiaji mabao mengi katika Bundesliga,Stefan Kiessling, alikomea mabao 3 pekee katika ushindi wa Bayer Leverkusen, wa mabao 4-0 dhidi ya Stuttgart.

Werder Bremen, ilioparamia kileleni mwishoni mwa wiki kabla kuzimwa na Bayer Leverkusen jana nusura ikione kilichomtoa kanga manyoya.Bremen, ilitoka nyuma na kwa bao la dakika ya mwisho la mlinzi wake Per Mertesacker, ikamudu kusawazisha 2-2 katika mpambano wao na mabingwa Wolfsburg.

Bremen inajikuta sasa nafasi ya pili ya ngazi ya Ligi nyuma ya Bayer Leverkusen.Schalke iko nafasi ya 3 baada ya kuzabwa bao 1:0 na Borussia Moenchengladbach.Bayern Munich,mabingwa mara kadhaa ambao sasa wamejipatia rais mpya nae ni yule meneja wao wa zamani Uli Hoenes, aliechukua kiti cha Franz Beckenbauer, walitamba huko Hannover walipowazaba wenyeji mabao 3-0. Sasa Munich imechupa hadi nafasi ya 4 ya ngazi ya Ligi ikinyatia kuparamia kileleni kabla ya siku kuu za X-masi.

Balaa limeipata Hertha Berlin, timu ya jiji kuu ambayo msimu uliopita ilikua nusra ichukue ubingwa na ilicheza champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya.Msimu huu lakini, Berlin inaonesha inazama daraja ya pili ,kwani inaburura mkia wa Ligi.Kocha wa Berlin, Friedhelm Funkel, baada ya timu yake kuzabwa mabao 3-0 na Eintracht Frankfurt, anadai ingawa jahazi lake linakwenda mrama, bado halijazama:

"Hakuna hisia za kuteremshwa daraja ya pili.Kazi sasa itakua ngumu zaidi kujikomboa kutoka mkiani mwa Ligi.Lakini, yule alieanguka chini,hana budi, bali kunyanyuka na tutafanya hivyo."

Alisema Funkel, kocha wa Hertha Berlin.

Ama katika Premier League-Ligi ya Uingereza,Chelsea, imerudi kutamba kileleni baada ya kuikandika Arsenal mabao 3-0 katika Emirate Stadium jana.

Ushindi huo, umepanua mwanya wao na mahasimu wao Manchester United hadi pointi 5.Mabao 2 ya muivory Coast, Didier Drogba na 1 la Thomas Vermaelen,alilotia katika lango lake mwenyewe, yalitosha kupiga msumari wa moto juu ya donda la Arsenal London.Chelsea ambayo imeshaitimua Manu na Liverpool msimu huu, inaongoza Premier League kwa pointi 36-tano zaidi kuliko Manu.Katika La Liga,ligi ya Spain, FC Barcelona ,kwa bao la Mswede,Zlatan Ibrahimovic,ilitamba mbele ya Real Madrid .

Mwandishi: Ramadhan Ali/ RTRE

Mhariri:Abdul-Rahman